Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samatta atikisa vigogo Ulaya

10301 Pic+samatta TanzaniaWeb

Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Nyota ya mshambuliaji wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta, imezidi kung’ara baada ya klabu za Mainz 05 na Hertha Berlin kuingia vitani kuwania saini yake katika usajili wa majira ya kiangazi.

Taarifa za Mainz na Hertha Berlin kuwania saini ya nyota huyo anayecheza KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji, zimekuja wiki moja tu tangu klabu za Levante ya Hispania na CSKA Moscow kutoka Russia kutangaza kumwania.

Gazeti maarufu la michezo nchini Ufaransa, L’Equipe jana liliripoti kuwa klabu hizo mbili za Ujerumani zimevutiwa na kiwango cha nahodha huyo wa Taifa Stars, baada ya kung’ara katika Ligi Kuu Ubelgiji.

Klabu zote nne zimeongeza kasi ya kuwania saini ya Samatta kabla ya dirisha la usajili kufungwa huku zikiwa zimebaki siku chache.

Licha ya Samatta kushindwa kuwa na mwendelezo wa ubora wake katika kufunga mabao msimu uliopita nchini Ubegiji, klabu hizo zimeonyesha imani kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon, Simba na TP Mazembe Englebert zikiamini atasaidia kuimarisha safu ya ushambuliaji.

Pamoja na kutokupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Genk, tangu Samatta alipoanza kuitumikia timu hiyo akitokea TP Mazembe kwa ada ya Euro 800,000 (Sh 2.1 bilioni) hadi sasa ameifungia mabao 21 katika Ligi Kuu Ubelgiji na mashindano ya Europa League ambayo Genk iliishia hatua ya mtoano msimu wa 2016/2017.

Klabu hizo mbili za Ujerumani zina kazi kubwa ya kumshawishi Samatta ajiunge nazo kwa kuwa mshambuliaji huyo muda mrefu amekuwa na ndoto ya kucheza Ligi Kuu Hispania jambo ambalo linaiweka Levante katika nafasi nzuri kumnasa.

Pia Samatta ana ndoto ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya hivyo kutokana na Levante kutokuwa na nafasi ya kushiriki mashindano hayo msimu ujao, kuna uwezekano mkubwa CSKA ikawa kipaumbele cha kwanza kwa nahodha huyo ambaye amekuwa akipata mafanikio tangu alipoondoka Simba na kujiunga na TP Mazembe mwaka 2012.

TP Mazembe ilivutiwa na uwezo wa Samatta katika mechi mbili za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2012 ilizocheza na Simba ambapo mshambuliaji huyo alifunga mabao mawili jambo lililowafanya wamnunue kwa kitita cha fedha kinachokadiriwa kuwa Sh150 milioni.

Akiwa TP Mazembe, Samatta aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015, pia aliiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa mashindano hayo na kama hiyo haitoshi, alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani mwaka 2015.

Baada ya mafanikio hayo, aliingia kwenye rada za klabu za Ulaya hasa Sochaux ya Ufaransa, lakini ilikuwa Genk iliyofika dau ambalo TP Mazembe ililoweka kwenye kipengele cha mauzo ya mshambuliaji huyo katika mkataba wake.

Chanzo: mwananchi.co.tz