Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samatta afungua kampuni ya Utalii, amwaga ajira, agawa bajaj

45789 Pic+samata.png Samatta afungua kampuni ya Utalii, amwaga ajira, agawa bajaj

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

JANA katika mfululizo wa mahojiano maalumu ya baba yake Mbwana Samatta, Mzee Ally Samatta Pazi, juu ya maisha ya mwanaye nje ya soka, alianika namna alivyojitolea kwa jamii na ishu nzima ya kujenga msikiti na alivyoiboresha nyumba yake ya kisasa.

Mzee Samatta pia alifichua namna mwanaye alivyomwaga noti kuitengeneza nyumba yake iwe ya kisasa zaidi na kuweka ulinzi usio wa kawaida kama njia ya usalama.

Leo tunaendelea na mfululizo wa makala haya maalumu ambayo Mzee Samatta anafichua mwanaye alivyofungua kampuni ya Utalii ambayo ipo hatua ya mwisho kuanza kazi ikitegemea kumwaga ajira kwa vijana nchini, sambamba na kumpa daladala na kugawa Bajaj zake...Endelea nayo!

KAMPUNI YA UTALII

Mzee Samatta anasema katika kitu ambacho amefurahishwa na mwanaye ni jinsi alivyoamua kuwekeza kwenye vitega uchumi akitumia fedha zake zitokanazo na soka.

Anasema kwa sasa Samatta amefungua kampuni ya utalii inayojulikana kwa jina la Mbwana Samatta Tours & Safaris akidai kwa sasa ipo katika hatua za mwisho kabla ya kuanza kufanya kazi rasmi.

“Tayari imeshapata vibali vyote vya serikali kinachosubiriwa ni vitendea kazi, ili zianze rasmi na hili ni jambo linalonifurahisha kama mzazi. Maisha ya soka kama huwekezi chochote ukistaafu unaweza kuishi tofauti na ukubwa wa jina, lakini mwanangu ameliona mapema, nampongeza.”

Mzee Samatta amefunguka mikakati inayoendelea kuhusiana na kampuni hiyo inayotarajiwa kufanya kazi wakati wowote kuanzia sasa, alisema tayari gari moja limeishanunuliwa ni aina ya Toyota Alphard ambalo linaenda kubadilishwa namba kutoka kwenye usafiri wa kutembelea na kuwa la biashara.

“Hapa magari yanayosubiriwa ni matatu ambayo ni ya kitalii na yapo njiani tunasubiri muda wa kufika Tanzania. Samatta ameishamwajiri mkurugenzi mkuu anayeitwa Khamis Waziri ambaye ana uzoefu na kazi hiyo kwa muda wa miaka tisa, msaidizi wake ni Hazibun Habibu.

“Vituo vitakuwa viwili Arusha ambako ndiko atasimamia Mkurugenzi Mkuu (Waziri) na Dar es Salaam atasimamia msaidizi wake, Habib,”anasema.

Mzee Pazi anaendelea kulimwagia siri Mwanaspoti kwamba ajira zitakuwa nyingi kwenye kampuni hiyo kama kuajiri wapishi, wafanya usafi, walinzi, madereva, wapokea wageni ‘receptionist’ na katibu ikiwa ni sehemu ya mchango wa mwanae kwa jamii ya Kitanzania.

“Itaajiri watu wenye umri tofauti, hiyo ni ajira tosha kwa Watanzania wenzake pia yatakapofika hayo magari tutafanya ufunguzi kwa kualika watu mbalimbali wakiwemo kutoka serikalini ili kutia mkono wa baraka.

“Pia, katika uzinduzi huo ameniambia atakuja na wachezaji wenye majina makubwa duniani, lakini wa timu ambayo atakuwepo kwa wakati huo, hivyo hakutaka kufunguka majina yao,” anasema.

Mzee huyu anaongeza; “Ofisi ya Samatta itakuwa kwenye nyumba yake iliopo Kibada ambapo atakuwa anasikiliza mambo ya utalii pamoja na masuala ya mikataba ya wachezaji, hivyo kuna vitu vingi vikubwa anavyotaka kuvifanya.”

AMPA BABA MABASI

Mzee Samatta anafichua Samatta anaithamini sana familia yake kwani hata yeye amempa mabasi mawili ya kutumika kama daladala ili ayatumie kumuingiza fedha.

“Unajua hakuniambia moja kwa moja baada ya kununua ila baadaye akaja kusema baba utakuwa unapata vihela vya mbogamboga,” anasema baba Samatta kwa bashasha.

“Lakini pia kwenye daladala hizo kumeajiriwa watu ambao wanapata kipato cha kujikimu na maisha yao, naona bado anaendelea kujihusisha na jamii, ingawa sio msemaji sana wa mambo hayo,” anasema.

Anasema daladala hizo zinafanya kazi njia ya Buguruni- Chanika na Gerezani Kiponza na zimekuwa zikimuingiza fedha kiasi kwamba shida ndogondogo hana na anamshukuru Mungu kumjalia watoto wanaomthamini na kumjali, huku akiwaombea wazidi kupata neema zaidi duniani na ahera.

KAGAWA BAJAJ ZAKE

Mzee Samatta anasema, mwanaye alikuwa na Bajaj tano, lakini nne kati ya hizo amewapa kaka zake na moja kwa mtarajiwa wake ambaye amezaa naye watoto wawili Abdulkarim (4) na wa kike Isimini (2).

“Kuna vitu ambavyo ameamua kupunguza majukumu ndio maana amegawa hizo Bajaj kwa lengo la ndugu zake wajitegemee, wanazifanyia biashara hivyo yeye anahusika na vitu vikubwa vikubwa,” anasema.

KUMBE KAPANGA KWA RIDHIWANI

Licha ya kuwa na nyumba ambazo anafanya biashara ya kuzipangisha na mjengo wa maana aliyojenga, Samatta amepanga nyumba ya Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete iliopo Kijichi, anafichua mzee wake.

Samatta aliamua kumpangishia mzazi mwenzie na watoto na nyumba ikishakamilika ndipo watahamia hao kuishi kama familia kwa ujumla.

“Baada ya kukamilisha kila kitu, huku ndani ndipo atakapohamisha familia yake, ndio maana ameweka ulinzi wa kutosha na bila kibali ukifika hapa unaweza ukapata matatizo, lakini kwa sasa familia yake ameipangishia nyumbani kwa Ridhiwani Kikwete,” anasema.

Mzee Samatta anamalizia mambo ambayo Samatta amekuwa akiyafanya nje ya uwanja, kesho Jumapili tutaendelea na yale anayoyafanya uwanjani akiwatesa Wazungu, ambapo kocha wake atafunguka mengi kuhusu supastaa huyo wa Tanzania.

Je, unajua rafiki yake ni nani ndani ya klabu yake ya Genk na unafahamu kuwa, Samatta anaye shabiki ambaye humwambii kitu kwa nahodha huyo wa Taifa Stars?

Endelea nayo Jumapili upate uhondo kamili.

ITAENDELEA..!

 



Chanzo: mwananchi.co.tz