Dar es Salaam. Kiungo wa Ghana, Joseph Paintsil amesema Mbwana Samatta ni mshambuliaji wa aina yake na mabao aliyofunga yamechangia kwa kiasi kikubwa kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji KRC Genk.
KRC Genk juzi usiku ilikabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Luminus, baada ya kucheza na Standard Liege katika mchezo wa kukamilisha ratiba waliotoka suluhu.
Akizungumza kwa simu jana, Paintsil alisema amejifunza mengi kutoka kwa Samatta na kila mmoja ana furaha naye kwa kuwa amefanya kazi kubwa msimu huu 2018/2019.
Paintsil alisema ana kipaji cha kufunga mabao kwa mpira wa kichwa kama aliyekuwa mshambuliaji wa Chelsea na Ivory Coas, Didier Drogba.
Samatta amekuwa akifunga mabao ya kichwa kutokana na mipira krosi inayopigwa na kiungo wa pembeni, Leandro Trossard, ambaye amekuwa akimtengenezea nafasi za kufunga.
“Ninachoweza kumtofautisha Samatta na washambuliaji wengine ni namna ya uchezaji wake, ana staili tofauti, anaweza kusimama mbele, anaweza kuwa mshambuliaji lakini pia akatokea pembeni,” alisema.
Pia Soma
- Kocha Simba ajipa ubingwa mapema
- Hesabu hizi Simba bingwa
- Mbappe aitega PSG, atoa kauli tata ya hatma yake
Samatta aliwahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka mwenye asili ya Afrika anayecheza soka la kulipwa Ubelgiji.
Tuzo hiyo ya pili kwa Samatta, mara ya kwanza alitwaa Januari 2016, Abuja, Nigeria alikotangazwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani wakati akijiandaa kuondoka TP Mazembe ya DR Congo kwenda KRC Genk. Genk imepata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.