Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Salum Lupepo: Dogo kidato cha kwanza anayetisha Serengeti Boys

49344 Salum+pic

Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kikosi cha Timu ya Taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kipo kambini kikijiandaa na Fainali za Afcon ambazo zitaanza kupigwa nchini Novemba 14.

Mwananchi lilipata nafasi ya kufanya mahojiano na vijana hao kutaka kufahamu ndoto zao na jinsi walivyopata nafasi ya kuingia katika kikosi hicho.

Salum Lupepo Abubakari anayecheza beki katika kikosi hicho kinachonolewa na Oscar Milambo, alifunguka mengi ya kumhusu.

Lupepo alisema haikuwa rahisi kwake kuingia Serengeti Boys kwani kulikuwa na vijana wengi waliokuwa wanapigania nafasi hiyo.

“Nakumbuka mwaka 2015 yalifanyika mashindano kwa vijana chini ya miaka 13. Wakati huo nilikuwa mkoani Mwanza nikiichezea Alliance Academy. Nilifanya vizuri sana na ndipo nikachaguliwa, haikuwa rahisi kwasababu vijana wengi walikuwa na uwezo,” alisema.

Aliongeza kwamba baada ya kuchaguliwa waliwekwa kambini kwa muda kabla ya kuletwa Dar es Salaam ili kuungana na wachezaji wengine waliopatikana katika michuano mbalimbali ya kusaka vipaji.

Lupepo ambaye ametokea katika maisha ya shule na moja kwa moja kuingia katika kikosi cha Serengeti Boys, alisema kuna tofauti kubwa kwenye maisha ya soka pande zote mbili alizocheza.

“Alliance ile ni shule ya vipaji kwahiyo tulikuwa tunaishi kama tupo shule, JMK (Jakaya Mrisho Kikwete, Kidongo Chekundu) tunafanya mazoezi usiku na kurudi nyumbani, lakini Serengeti Boys ni tofauti kidogo kwa sababu tunafanya mazoezi asubuhi na jioni na tunakaa kambini, tunakuwa tupo fiti zaidi,” alisema.

Aliongeza kutokana na mazingira ambayo anaishi katika kikosi cha Serengeti Boys, amejikuta hajutii kuwapo katika kikosi hicho tangu ajiunge.

Baada ya kufanikiwa kuingia katika kikosi cha Serengeti Boys kinachoshiriki fainali za Afcon, Lupepo aliliambia gazeti hili kwamba mipango yake hivi sasa ni kukipiga nje ya nchi.

“Malengo yangu mimi ni kucheza soka la kulipwa nchini Hispania kwasababu ni sehemu ambayo ninaipenda kutokana na soka lao lilivyo, ikitokea Bongo sawa lakini akili yangu inawaza nje tu,” alisema.

Lupepo ambaye anacheza nafasi ya beki wa kati, alisema kwa hapa nyumbani, amekuwa akivutiwa na jinsi beki wa kati wa Yanga, Andrew Vicent ‘Dante’, anavyocheza.

“Kibongo bongo nampenda sana Dante kwa jinsi anavyocheza, lakini kwa nje nampenda Sergio Ramos wa Real Madrid, anajua kukaba, ni mtu anayejua kutumia nguvu na akili kwa wakati mmoja,” alisema dogo huyo anayemkubali msanii Mwana Fa kupitia kibao chake cha ‘Dume Suruali’.

MSOSI WAKE NOMA

Lupepo aliliambia gazeti hili kwamba katika misosi humwambii kitu kuhusu ugali dagaa na juisi ya embe.

“Napenda sana kula ugali uwe wa sembe au dona lakini lazima uwe na dagaa, hapo hunitoi hata kidogo, huwa nakipendelea sana chakula hicho,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz