Viungo tegemeo hivi sasa katika kikosi cha Simba, Ousmane Pape Sakho na Sadio Kanoute wote wapo fiti na vizuri kuwavaa Ruvu Shooting.
Nyota hao wote walipata majeraha katika mchezo uliopita wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa wikiendi iliyopita dhidi ya Asec Mimosas ya nchini Ivory Coast.
Kurejea kwa viungo hao kutaimarisha kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu Mhispania, Pablo Franco na msaidizi wake, Selemani Matola.
Meneja Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally alisema kuwa, viungo hao wote juzi Jumatatu walifanyiwa vipimo na kuonekana kutopata majeraha makubwa.
Ally alisema kuwa, baada ya vipimo walivyopatiwa viungo hao, madaktari wakashauri wapumzike kwa siku moja kabla ya leo Jumanne kuanza mazoezi ya pamoja na wenzao tayari kwa kuwavaa Ruvu.
Aliongeza kuwa kurejea kwa viungo hao kutaimarisha kikosi chao ambacho bado kina majeruhi wawili ambao bado hawajapona vizuri Chris Mugalu, Kibu Denis na Taddeo Lwanga wanaoendelea na mazoezi binafsi. “Sakho na Kanoute wote wapo fiti na leo (jana) wamejumuika kwenye mazoezi ya pamoja na wenzao kujiandaa na mchezo wa FA dhidi ya Ruvu Shooting.
“Hiyo ni baada ya uchunguzi wa daktari Sakho na Kanoute wakapewa mapumziko ya siku moja ambayo ni jana (juzi Jumatatu) kabla ya leo (jana) kurudi mazoezi kujiandaa na mchezo huo.
“Mchezo huu ni muhimu kwetu kupata matokeo mazuri kutokana na malengo yetu tuliyojiwekea kutetea mataji yote tunayoshindania katika msimu huu,” alisema Ally.