Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu za Simba SC kung'oka CAF

Kungoka Pic Data Sababu za Simba SC kung'oka CAF

Wed, 27 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

SIMBA imepata mshtuko kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya juzi kukubali kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Matokeo hayo sio tu kwamba yamewatupa nje Simba kwenye michuano hiyo, pia yamevunja rekodi yao ya kutopoteza nyumbani katika mashindano ya Afrika tangu walipopoteza mara ya mwisho 2013 na Libolo ya Angola hatua.

Mashabiki wa Simba wameumizwa na matokeo hayo wakikumbuka kwamba kikosi chao kilitangulia kushinda ugenini mabao 2-0 nchini Botswana kisha kutangulia mbele bao 1-0 hadi mapumziko kisha hali kubadilika kipindi cha pili wakikubali kipigo cha mabao hayo 3-1.

Kelele zipo nyingi juu ya kupoteza kwa Simba, lakini yapo makosa maeneo matatu juu yaliyosababisha mabingwa hao watetezi wakapoteza ambayo ni lazima yafanyiwe kazi haraka kwa kuwa bado kikosi hicho kinaangukia Kombe la Shirikisho Afrika.

mastaa waliridhika

Baada ya ushindi wa mabao 2-0 kisha kutangulia kupata bao moja nyumbani, Simba walionekana kurudi kipindi cha pili juzi wakiwa wa kawaida sana. Wachezaji hawakuwa na njaa ya ushindi mkubwa na waliona kama wamemaliza mechi, Bernard Morrison akianza kuchezea mpira hata kupanda juu, jambo ambalo liliwapa nafasi wapinzani wao.

Mabadiliko ya kuingia Peter Banda kuchukua nafasi ya Hassan Dilunga hayakuwa na mchango mkubwa kwa Simba walioonekana kushindwa kutengeneza nafasi zaidi na pia walishindwa kumalizia nafasi. Mbaya zaidi hakuwa na mchango katika kupokonya mipira.

Benchi la ufundi kukariri

Benchi la ufundi la Simba haliwezi kukwepa lawama, kwani Simba iliyocheza Botswana ndio ileile iliyocheza Uwanja wa Mkapa na mbinu zilezile na kibaya zaidi ilionekana imeridhika na ushindi wa ugenini ikisahau kuwaheshimu wapinzani wao.

Kocha Didier Gomes na Thierry Hitimana baada ya dakika 45 za kipindi cha pili kuanza na Galaxy kupata bao walitakiwa kubadilika haraka na kuwatoa wachezaji ambao walionekana kucheza kawaida wakiwamo mabeki Pascal Wawa, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na hata Shomari Kapombe walioonekana kusahau majukumu yao ya kukaba na kasi yao ya kuzuia ilikuwa ndogo wakati

Galaxy wakitengeneza

mashambulizi.

Ni wakati wa haraka sasa Simba hasa makocha kuanza kubadilika kwa kuangalia kupewa nafasi wachezaji kama Kennedy Juma, Gadiel Michael na hata Israel Mwenda ambao Mwanaspoti linafahamu kwamba wamekuwa bora mazoezini, lakini nafasi hawapati.

Kennedy ni beki mzuri katika mapambano ya mipira ya juu kwa ubora alionao isingekuwa rahisi kufanya makosa ambayo Wawa na Enock Inonga ‘Varane’ walikuwa wakifanya.

Pia, wakati mwingi Kapombe na

Tshabalala walionekana kuelekeza akili zao katika kushambulia zaidi na sio kulinda ambalo ndilo jukumu lao la kwanza, lakini Simba ikiwatumia Gadiel na Mwenda ingepata faida kubwa ya kulinda ushindi wao kutokana na ubora wa mabeki hao katika kukaba.

mMakocha Gomes na Hitimana lazima wakae pamoja na kujitathimini juu ya mbinu zao kwani zimeanza kuzoeleka kwa wapinzani wao, ingawa zipo taarifa kwamba Hitimana alitaka kumtoa Wawa, lakini Gomes akazuia. Hii inaonyesha kwamba kuna utofauti katika utoaji wa uamuzi ukizingatia wanafanya kazi wakiwa na umbali uwanjani katika michuano ya Caf wakitumia simu kuelekezana na kushauriana.

Kocha wa Galaxy, Morena Ramoreboli inawezekana mwili wake ulimfanya adharauliwe, lakini rekodi yake ya kuwa hata kocha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini ilipaswa aheshimike. Alitumia makosa ya Gomes na Hitimana kufanya matokeo kubadilika kwa haraka, akiwaingiza wachezaji ambao walimpa heshima ugenini akijua makosa ya Simba ni yapi.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha Mkuu wa Biashara, Patrick Odhiambo anasema kilichowaponza Simba ni kuingia na matokeo uwanjani baada ya kupata ushindi ugenini wakiwachukulia wapinzani wao ni dhaifu.

“Wapinzani walitumia kigezo cha kukubali kushindwa na kucheza na akili ya wenyeji kwamba wamekuja kukamilisha ratiba, lakini haikuwa hivyo, kwani walifanya kitu tofauti, walicheza mchezo kwa haraka haraka kama wapo nyumbani tofauti na Simba ambao mchezo wao ulikuwa ni wa taratibu, pasi fupifupi lakini hazina madhara,” alisema.

“Ubora wa wapinzani ni kuamini kuwa wanaweza na kucheza mpira wa harakaharaka ambao uliwaamsha Simba muda ukiwa umekwisha na kujikuta wanacheza pasi ndefu ambazo ni rahisi kuokolewa na mpinzani.”

Naye kocha wa zamani wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema uzembe wa mabeki na kutojiandaa kitimu kuwakabili wapinzani wao ndilo kosa kubwa lililowaangusha.

“Simba hawakujiandaa kwa mchezo huo, waliamini katika kushinda kutokana na kupata matokeo ugenini. Sijajua kwanini hawakupata funzo kutoka UD Songo ambao ugenini waliwafunga bao, lakini nyumbani walikomaa na kupata sare kujiamini na kuwapuuza wapinzani wao ndio kilichowaponza,” alisema.

Kwa upande wake, kocha wa Mwadui FC, Adolf Rishard alisema kukosa umakini na kujiamini kupita kiasi ni changamoto iliyowanyima matokeo Simba baada ya kupata bao la mapema kipindi cha kwanza wakiamini wametinga hatua inayofuata.

“Waliruhusu mabao ya kizembe, walicheza vizuri kipindi ambacho wamefunga bao, baada ya hapo waliiona nafasi yao hatua ya makundi na kusahau kuwa bado mpira haujamalizika,” alisema. “Baada ya kufungwa mabao mawili ya haraka ndio wakakumbuka kuwa mpira unachezwa, lakini walikuwa tayari wamechelewa kwani wapinzani walikuwa wamepata moto na wanacheza pasi za harakaharaka tofauti na Simba ambao walikuwa wanacheza pasi ndefu ambazo ni rahisi kuokolewa.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz