Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu za Franco kukubali kufanya kazi Simba

Kocha Simba, Pablo Franco atoa sababu kukubali kutua Simba

Wed, 10 Nov 2021 Chanzo: ippmedia.com

HUKU mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wakieleza kurejea kwa wachezaji wao watatu waliokuwa majeruhi, Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo, Mhispania Pablo Franco, ameeleza furaha yake ya kujiunga nao na kuanika sababu zilizomvutia kukubali kutua kukinoa kikosi hicho.

Simba juzi ilitangaza kuingia mkataba wa miaka miwili na Franco ambaye aliwahi kuwa Kocha Msaidizi wa Real Madrid mwaka 2018, lakini mwaka 2015 akiinoa Getafe kama kocha mkuu kwa kuiongoza kwenye Ligi Kuu ya Hispania, LaLiga.

Hata hivyo, Franco ambaye ametua Simba akitokea Al-Qadsia ya Kuwait, hakuwahi kuzungumza chochote tangu akubali kuingia mkataba na Simba, lakini jana alitupia video fupi katika mtandao wa kijamii akieleza furaha yake ya kujiunga na mabingwa hao wa Tanzania Bara.

"Nimefurahi kujiunga na Simba, ni timu kubwa Afrika ina mashabiki wengi na ina matarajio makubwa jambo ambalo limenivutia. Simba Nguvu Moja," alisema Franco.

Hata hivyo, wakati mashabiki wa Simba wakifurahia kumpata kocha huyo wa daraja la juu kisoka, furaha hiyo itakuwa imeongezeka mara mbili zaidi baada ya habari njema ya kurejea kwa wachezaji wao watatu kati ya watano wa kikosi cha kwanza walikuwa majeruhi.

Chumba cha majeruhi cha Simba, kilikuwa na wachezaji watano muhimu wa kikosi cha kwanza, lakini sasa wamebaki wawili baada ya klabu hiyo kutangaza kurejea mazoezini kwa viungo Sadio Kanoute, Pape Ousmane Sakho na Mzamiru Yassin.

"Sadio Kanoute, Pape Ousmane Sakho na Mzamiru Yassin, wamepona majeraha yao na wamerudi uwanjani wakiwa fiti kwa asilimia 100," ilieleza taarifa hiyo ya Simba.

Tayari Kanoute na Sakho wameanza mazoezi pamoja na wenzao tangu juzi wakati Mzamiru amejiunga na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachojiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya DR Congo, mchezo utakaopigwa kesho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Wachezaji wengine waliokuwa majeruhi, Kiungo Taddeo Lwangwa, uongozi wa Simba ulieleza yeye bado anauguza jeraha na amepewa mapumziko ya wiki mbili kabla ya kurejea uwanjani kuuwahi mchezo dhidi ya Ruvu Shooting utakakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Novemba 19, mwaka huu.

Kuhusu mshambuliaji Chris Mugalu, "yeye ataendelea kukosekana kwa sababu ya jeraha linalomsumbua kutopona vizuri, hivyo amepewa muda ili awe fiti kwa asilimia 100".

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Kenya, 'Harambee Stars', Mturuki Engin Fırat, ameeleza changamoto anayoipitia baada ya kuwakosa mabeki wake watatu wa kati tegemeo aliowaita katika kikosi hicho kinachojiandaa na mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Uganda kesho, Alhamisi.

Fırat alisema katika mchezo huo atawakosa mabeki wa kati Joash Onyango wa Simba ambaye amekataa kujiunga na Harambee Stars baada ya kuamua kubaki na klabu yake.

"Nitawakosa Joseph Okumu [anayeichezea Gent ya Ubelgiji] ambaye ni majeruhi, pia Joash Onyango na Brian Mandela [Mamelodi Sundowns] wamegoma kujiunga na timu ya taifa baada ya kuamua kubaki na timu zao," alisema Fırat.

Chanzo: ippmedia.com