Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu tatu za Simba kuialika TP Mazembe "Simba Day"

Mazembe Pic Data Sababu tatu za Simba kuialika TP Mazembe "Simba Day"

Thu, 9 Sep 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

SIMBA imetaja sababu tatu za kuialika TP Mazembe kwenye kilele cha siku ya Simba Day, Septemba 19 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Simba itacheza na TP Mazembe mechi ya kimataifa ya kirafiki, timu ambayo ipo kambini ikikiwasha na waarabu nchini Morocco na sasa italazimika kupitiliza moja kwa moja Dar es Salaam.

Rais wa Simba Murtaza Mangungu amesema wameamua kucheza na Mazembe kwa kuwa ni miongoni mwa timu bora Afrika na ambayo msimu huu imefanya usajili wa aina yake.

Alisema mbali na kigezo hicho, pia walitaka kucheza na timu 10 bora za Afrika hivyo wanaamini itatoa upinzani wa kutosha kwa Simba kwani wako makini ndani na nje ya uwanja licha ya kejeli za mashabiki kwamba imechuja.

“Pia janga la corona limefanya mazingira ya timu kuingia na kutoka kwenye baadhi ya nchi kuwa magumu na kwenye baadhi ya nchi Ligi bado hazijamalizika,” alisema Mangungu huku akiwataka wanasimba kumiminika kwa wingi kwani Mazembe ni kipimo sahihi.

Alisema mbali na burudani ya soka, kwenye tamasha hilo mashabiki watapata zaidi ya burudani kwani Simba imesheheni na wachezaji wamepania kuonyesha uwezo mbele Mazembe ambao wamekuwa wagumu kufungika kwenye miezi ya hivikaribuni.

Mangungu alisema TP Mazembe watawasili nchini siku tatu kabla ya tamasha hilo ambalo wamepania msimu huu liwe na fleva za aina yake.

MASTAA WATOA NENO

Mastaa wa zamani wa Simba, wanatarajia kuona maajabu ya aina yake yatakayofanyika Septemba 19 kwenye siku ya klabu hiyo, yatakayoacha funzo kwa timu nyingine za Ligi Kuu Bara.

Kiungo Shaban Kisiga alicheza Simba Day, mwaka 2014 na 15, anazungumzia uzoefu wake katika tamasha hilo, linatoa taswira ya kujua mashabiki wao wanataka nini.

“Wachezaji wanakuwa wanapata muda wa kuonyesha uwezo mbele ya mashabiki wao, kwa hiyo tulikuwa tunajiandaa vilivyo kuitumia vyema siku hiyo, viongozi nao walijiandaa vya kutosha kulifanya linakuwa zuri,” alisema.

Aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Nassor Masoud ‘Chollo’ alisema mwanzilishi wa Simba Day, Hassan Dalali alikuwa na maono makubwa, hivyo anastahili kupewa heshima ya aina yake.

“Ni tamasha la aina yake ambalo linawakutanisha Wanasimba kwa pamoja, linajenga upendo, umoja na kupanga mipango ya msimu, kila mwaka linakuwa la aina yake, hilo la Septemba 19 naamini litakuwa la aina yake,” alisema.

Chollo alisema anatamani kuona Dalali anafanyiwa kitu cha kumpa heshima kitakachoacha alama kama alivyo acha alama ya tamasha hilo.

“Simba Day ni kati ya alama muhimu alizoziacha Dalali, Simba impe alama itakayokuwa ya kumbukumbu katika maisha yake kwa ubinifu aliokuwa nao wakati wa uongozi wake,” alisema.

Kwa upande wa Mussa Mgosi aliyekuwa nahodha wa timu hiyo na alikuwepo 2009 Simba Day ya kwanza, alisema anajisikia faraja kuona tamasha hilo linazidi kukua na kuwa mfano kwa timu nyingine.

“Ni tamasha la aina yake, nafurahia kuona linaendelea hadi leo ni jambo la kuwapongeza viongozi kwa kuliendeleza na kuwa kubwa na linajulikana hadi nje,” alisema.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz