Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu tano Bocco kukosa penalti Taifa

51066 Pic+bocco

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mshambuliaji nguli wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ‘Tekelo’ ametoa sababu tano zilizochangia nahodha wa Simba, John Bocco kukosa penalti dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.

Bocco ameibua mjadala baada ya mkwaju wake wa penalti aliopiga dakika ya 59 kupaa juu ya lango la TP Mazembe.

Simba ililazimishwa suluhu na TP Mazembe katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, kinara huyo wa zamani wa mabao alisema ingawa penalti haina ‘mwenyewe’, lakini mambo matano yalimvuruga Bocco kabla ya kupiga pigo hilo.

Mziba alisema sababu ya kwanza iliyochangia Bocco kukosa penalti ni umbo la miraba minne la kipa wa TP Mazembe, Sylvain Gbohouo raia wa Ivory Coast.

“Kwanza umbo la kipa wa Mazembe lilimchanganya kwa uzoefu wangu katika soka washambuliaji wengi wanapokutana na makipa wenye maumbo makubwa kama yule wanababaika wapige vipi na ndicho kilichomtokea Bocco,” alisema Mziba.

Nguli huyo alisema jambo jingine lililochangia mshambuliaji huyo kushindwa kufunga imetokana na kutofanya uamuzi sahihi wakati wa kupiga kiki yake.

“Siku zote Bocco hapigi penalti za juu, lakini alifanya vile akitaka kukadiria kupiga juu ambako yule kipa hataweza kupangua kutokana na umbo lake kubwa, lakini hesabu zake zikafeli,” alisema Mziba.

Pia alisema Bocco alitumia mbinu dhaifu ya kumuhadaa kipa huyo kwa kuwa kabla ya kupiga alimuangalia na aliinama akitaka kumdanganya, lakini pigo lake lilipoteza mwelekeo.

“Vilevile hakuwa na uamuzi wa penalti gani apige, hakuwa na uamuzi wa mapema inaonyesha hata wazo la kupiga juu hakuwa amepanga, isipokuwa lilimjia akiwa tayari katika muvu ya kupiga mpira,” alisema Mziba.

Nguli huyo alisema sababu nyingine iliyochangia ni hesabu mbovu katika upigaji, aliamini akipiga chini kipa atadaka jambo ambalo halikuwa kweli.



Chanzo: mwananchi.co.tz