Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SAKATA LA ZAHERA: Yaliyopo nyuma ya pazia

82435 Zaherraa+pic SAKATA LA ZAHERA: Yaliyopo nyuma ya pazia

Fri, 1 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

MASHABIKI wa Yanga kwa sasa wamemkomalia kocha wao Mwinyi Zahera wakitaka atimuliwe Jangwani kwa kuonekana ameshindwa kazi, baada ya kuishuhudia timu yao ikilala mabao 2-1 mbele ya wageni wao Pyramids ya Misri katika mechi ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Uongozi wa Yanga umesisitiza kuwa, kwa sasa akili zao zipo kwenye mechi yao ya marudiano itakayopigwa wikiendi hii na msafara wa timu hiyo unatarajiwa kuondoka nchini leo kwenda Misri. Hata hivyo kumekuwa na mijadala kama Zahera anastahili lawama juu ya kipigo dhidi ya Pyramids.

Pyramids imezidiwa umri tu wa kuanzishwa kwake na Yanga kulinganisha na timu hiyo ya Jangwani iliyoasisiwa 1935 wakati Wamisri hao walizaliwa 2008, huku wakiwa na uwekezaji mkubwa wa kiuchumi na kuwa na kikosi chenye wachezaji wenye thamani na kiwango cha juu.

Kadhalika karibu wachezaji sita wa timu hiyo wameitwa timu ya taifa ya Misri - taifa ambalo linashikilia rekodi ya kutwaa taji la Afrika (Afcon) mara sita, kuonyesha licha ya uchanga wao siyo timu nyepesi kama inavyochukuliwa.

Hata hivyo, wakati mzozo wa Zahera aondoke ama la unaendelea, baadhi ya wadau wa soka wametoa maoni yao wakidai kuwa kama kocha, Zahera hawezi kukwepa mzigo wa lawama kwa matokeo mabaya ya timu yake kwani ni ndiye aliyeisajili na anayeisimamia.

Kipigo cha Jumapili iliyopita kimeiweka Yanga katika nafasi finyu ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, kwani inatakiwa ishinde ugenini si chini ya mabao 2-0. Wakizungumza na Mwanspoti, makocha na wachambuzi wa soka wamedai kwamba kabla hata ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, hakukuwa na dalili nzuri upande wa Zahera.

Wamedai kwamba pamoja na Yanga kujitahidi kufanya vizuri msimu uliopita, mchango wa kocha huyo haukuwa mkubwa kiufundi kwani alikuta kikosi kilicho tayari.

Kocha Joseph Kanakamfumu alisema kipigo kutoka kwa Pyramids FC ni kama hitimisho tu la udhaifu wa Zahera kwani kocha huyo alipaswa kuwajibishwa kabla ya hapo.

“Inawezekana kushinda mechi zile ni vile alivyokutana na wapinzani wake. Kimsingi wapinzani wengi msimu uliopita walikuwa dhaifu kasoro labda timu kama nne, tano hivi. Nyingine zilizobaki zilikuwa zikigombania kutoshuka daraja na siyo kuchukua ubingwa au kumaliza nafasi nne za juu,” alisema. “Jambo la pili, msimu uliopita aliwakuta wachezaji waliozoeana wamekaa pamoja kwa muda mrefu, labda ingizo jipya kwake lilikuwa Makambo (Heritier), Feisal (Salum) na Mrisho Ngasa hivyo kuunganisha timu ilikuwa sio kazi kubwa.

“Hii ya msimu huu ndio timu yake iwe hakusajili wachezaji wote au vipi, lakini kazi ya kocha ni kuwaunganisha wacheze soka la ushindani. Siamini kama Yanga ina wachezaji wa wastani kama anavyosema. Yanga ina wachezaji wazuri tu.”

Alisema, ndani ya kikosi chao kuna wachezaji zaidi ya sita wanaoweza kuitwa timu za Taifa, na kwamba ni wachezaji bora. “Moja ya kati ya udhaifu alionao Zahera ni kutojua kuchagua wachezaji kucheza kutokana na mechi husika.”

Kanakamfumu alishauri Yanga impe Zahera idadi chache ya mechi na kama timu isipofanya vizuri, aonyeshwe mlango wa kutokea.

Naye mchambuzi wa soka, Alex Kashasha alisema kabla hata ya kuvaana na Pyramids, Yanga ilikuwa na udhaifu.

“Kinachotokea kwa wapenzi wa Yanga ni sahihi kwani timu haionyeshi kuimarika,” alisema.

“Kufungwa sio shida ila tatizo linakuja timu inapokuwa haionyeshi kuimarika, pia timu inaonekana haina muunganiko mzuri. Sasa kama inafika muda wa miezi sita timu haipo sawa, usitegemee miujiza.

“Pia hata uwezo wa mchezaji mmojammoja unaonekana kupungua. Sasa hapa mwalimu hawezi kuepuka lawama.”

Kashasha alisema, “lakini hata hivyo, ukifuatilia kwa undani utakubaliana na mimi kwamba chanzo cha matatizo ya Yanga ni pale walipomtimua kocha Hans Pluijm aliyekuwa ameshaijenga timu na kueleweka kwa wachezaji, lakini ghafla akaletwa Lwandamina ambaye naye wakati anaanza kuiunganisha akaondoka ndipo akaja Zahera.”

“Kwa bahati mbaya, msimu huu kundi kubwa la wachezaji limesajiliwa, lakini kocha kwa takribani miezi sita sasa ameshindwa kuwaunganisha. Mbaya zaidi ikawa inacheza mechi za kirafiki dhidi ya timu dhaifu ambazo hazikuonyesha tatizo la Yanga, lakini msimu ulipoanza tumeona jinsi timu inavyocheza ovyo tena dhidi ya timu za kawaida.”

Kocha wa timu ya taifa ya soka la ufukweni, Boniface Pawasa alisema usajili uliofanywa na Yanga msimu huu ndio ulianza kumkaanga Zahera.

“Mwalimu anapaswa kukubali kuvaa joho la lawama. Ukiangalia usajili wa Yanga msimu huu, kwa zaidi ya asilimia 68 umetokana na mapendekezo ya kocha, lakini hadi sasa ameshindwa kutengeneza kikosi cha kwanza na sijawahi kuona timu imefanikiwa huku ikiwa haina kikosi cha kwanza,” alisema Pawasa.

“Lakini pia muda wa kocha kukaa na kuiandaa timu ulikuwa mdogo huku ikiwa na kibarua cha kucheza mashindano ya kimataifa.

“Kikubwa na cha msingi, Yanga wanapaswa kutulia na kutochukua uamuzi wa hasira kipindi hiki. Wakae chini na mwalimu na kujadiliana kisha watoe mustakabali ambao hautaleta madhara.”

Hata hivyo, Bakari Malima alisema kwamba Zahera hapaswi kuhukumiwa na badala yake anatakiwa kupewa muda.

“Watu wa Yanga wanatakiwa kuwa watulivu. Kikosi kilisajiliwa kwa ajili ya mahitaji ya Ligi Kuu na mashindano ya ndani na siyo mechi za kimataifa. Wenzetu wale Pyramids wamewekeza sana na lazima tuwe wakweli kwamba Yanga hawana kikosi cha kushindana na wale,” alisema Malima.

Nyota huyo wa zamani wa soka nchini alionya kwamba, “(Yanga) wakianza sasa hivi kuchanganyana, mambo yatakuwa mabaya na pia watakuwa hawamtendei haki Zahera.”

Chanzo: mwananchi.co.tz