Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rono, mkali wa riadha aliyeacha darasa la ‘kesho utaishije’

Riadhaaaaa Rono, mkali wa riadha aliyeacha darasa la ‘kesho utaishije’

Sat, 2 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mwanariadha mkongwe wa Kenya, Henry Rono aliyepata umaarufu wa kuweka rekodi nne za dunia aliaga dunia Februari 15, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 72 katika hospitali moja jijini Nairobi alikokuwa anapatiwa matibabu na kuacha kumbukumbu ya aina yake.

Rono hatasahaulika tu kwao Kenya, bali duniani kote kwa mafaniko katika riadha yaliyosaidia kuitangaza nchi hiyo kama Mkenya mwenzake Keipchoge Keino; Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na John Stphen wa Tanzania, Brendan Foster (Uingereza) Dick Quax (New Zealand), Mamo Walde, Abebe Bikila na Mius Yifter (Ethiopia).

Katika kipindi cha siku 81 mwaka 1978, Rono aliweka historia ya kuvunja rekodi nne za dunia za mbio za masafa ya kati. Rekodi ya kwanza ni ya mita 10,000 (akitumia dakika 27 na sekunde 22.5) baadaye ya mita 5,000 (dakika 13:08.4), mbio za mita 3,000 za kupita kwenye madimbwi ya maji (steeplechase) kwa dakika 8:5.4, na hatimaye rekodi ya mita 3,000 (7:32.1).

Mwaka huo pia alishinda medali za dhahabu za mbio za mita 5000 na 3000 steeplechase kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola na kuweka rekodi mpya.

Lakini baada ya mafanikio yake makubwa ya mwisho ya 1970, Rono alianza kutumia muda mwingi kunywa pombe na kumuongezea uzito na baadhi ya nyakati hadi saa chache kabla ya mashindano.

Hata hivyo, katika mwaka 1981 aliweka rekodi mpya ya dunia ya mita 5,000 kwa kuvunja rekodi yake ya zamani ya dunia ya mbio hizo kwa akitumia dakika 13:6.2.

Kilichowashangaza wengi ni usiku kabla ya mashindano alionekana akinywa pombe katika baa moja na baada ya kustaafu aliamua kuishi Marekani kwa miaka 20, huku akitumia fedha alizopata katika mashindano ya kimataifa kwa pombe na anasa.

Rono akawa hana kitu. Alilazimika kukaa katika nyumba za watu masikini wasiokuwa na makazi katika Jiji la Washington, Marekani. Nilipotembelea Marekani 1987 nilifika katika hoteli moja inayotembelewa sana na watu wa Afrika Mashariki iitwayo Kilimanjaro jijini Washington na nilikutana na Rono ambaye nilifahamiana naye.

Kwa kweli nilisikitika kwa jinsi nilivyomuona na nilipomuuliza nini kimemsibu, aliniambia: “Ndio dunia. Ukipanda ngazi ipo siku utashuka na haya ndio yaliyonikuta.” Nilipomtaka arudi nyumbani aliniambia alifikiria kufanya hivyo, lakini wakati ulikuwa haujafika.

Alisema hakukuwepo haja ya kufanya haraka kwa sababu kama ni kukimbia kwa haraka alifanya hivyo zamani na kuweka rekodi za dunia na kwa wakati ule aliona bora ajifunze kufanya mambo kwa mwendo wa polepole.

Rono alizaliwa katika familia ya watu masikini wa kabila la Nandi katika Bonde la Ufa la Rift Valley, Kenya na alipata ajali alipokuwa na miaka miwili na kusababisha kuvunjika miguu yote miwili na madaktari waliamini asingeweza kutembea tena katika maisha yake.

Kutokana na kufanya juhudi za kujilazimisha kutembea, alimudu vizuri baadaye na alipoanza kukimbia akawa hakamatiki.

Mafanikio yake yanakaribia na yale ya mwanamama Wilma Ralph wa Marekani ambaye miguu yake ilikuwa imepinda na alikuwa akitembea kwa magongo, lakini alipoamua kuyaacha alitembea vizuri na kuweka rekodi ya dunia ya mbio za mita 100 katika michezo ya Olimpiki iliyofanyika Roma, Italia, mwaka 1960.

Tukirejea kwa Rono. Miaka kama 10 iliyopita aliacha pombe na kuchukua mafunzo ya elimu maalumu kwa ajili ya kuwafundisha watu wenye ulemavu.

Alifundisha riadha wanafunzi wa sekondari katika Jiji la Albuquerque, New Mexico na baada ya kuwa mbali na mkewe Jennifer Jepkemboi waliungana tena na kuwasiliana na watoto wake, Calvin Kipkorir na Maureen Chepchumba. Mwaka 2014 aliandika kitabu cha maisha yake alichokiita ‘Ndoto ya Olimpiki’ na katika sehemu moja anaeleza: “Mimi ni Henry Rono, shujaa wa kabila la Nandi mtu mwenye umri wa miaka 56 niliyefanikiwa kuacha pombe ambayo ilinitawala."

Akazeleza kuwa, “licha ya kupambana na vizingiti vingi katika maisha yangu, ila nashuhukuru nimevivuka vyote salama, katika jamii yangu iliyonielea na kunitukuza nilipokuwa ninang’ara katika ulimwengu wa riadha mwaka 1978 na baadaye ikanitelekeza na kuwa sio mtu mwenye thamani, hivyo nashukuru nimefanikiwa kwa sababu mimi ni shujaa wa kabila la Nandi.”

Rono alikuja kujikuta katika hali mbaya baada ya pombe kumtawala na ilimbidi mwanariadha mkongwe wa Kenya, Kipchoge achangishe fedha na kuwatafuta watu wengine wasaidie kumkatia tiketi ya kurudi nyumbani baada ya kukaa Marekani kwa miaka mingi.

Mara nyingi maisha yake yalikuwa hatarini kwa kuvamiwa na majambazi wakati akifanya kazi ya ulinzi nyakati za usiku wa baridi kali na kupitia safu hii ni somo kwa wanamichezo wengine kujijengea maisha ya baadaye baada tu ya kustaafu.

Chanzo: Mwanaspoti