***Kinachozungumzwa na vyombo vya habari kunihusisha na klabu nyingine ni kunikosea heshima...
CRISTIANO Ronaldo amezishutumu ripoti za vyombo vya habari kumhusisha yeye na mpango wa kuondoka Juventus. Katika ujumbe aliouweka kwenye ukurasa wake wa Instagram hakuonyesha kukataa au kukubali uwezekano wa kubaki kwa miamba hao wa Italia.
Lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36, amesema kwa sasa "akili yangu ni kazi" licha ya uvumi kumhusisha na Real Madrid, Paris Saint-Germain na Manchester City.
Nahodha huyo wa Ureno ameuita uvumi huo kuwa "dharau kwangu kama mtu na kama mchezaji.”
Aliongeza: "Hebu tuzungumze na tufanye kazi, hilo limekuwa mwongozo wangu tangu nilipoanza maisha ya soka. "Hata hivyo, kila kitu kilichoandikwa na kuzungumzwa hivi karibuni, sijakizingatia kwa sasa.
"Kile kinachozungumzwa na vyombo vya habari kuhusu majaliwa yangu na kunihusisha na klabu nyingine ni kunikosea heshima."
Mapema Jumanne, kocha mpya wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, alijibu uvumi kuhusu kumtaka Ronaldo kupitia kwenye tweeter, akikanusha kuhusishwa na kumwania Ronaldo katika klabu yake.
"Cristiano ni mchezaji gwiji wa Real Madrid na ana mapenzi na heshima zote. Sijawahi kufikiria kumsajili yeye. Tunaangalia mbele,” aliandika Ancelotti.
Ancelotti alijibu uvumi huo baada ya Televisheni ya El Chiringuito ya nchini Hispania kuripoti kwamba, kumekuwa na mazungumzo kati ya Real Madrid na Ronaldo kuhusu uwezekano wa kumsajili katika klabu hiyo aliyoondoka miaka mitatu iliyopita na kutua Juventus kwa pauni milioni 99.2.
Ronaldo alijiunga na Real akitokea Manchester United Julai mwaka 2009 na alifunga mabao 450 katika mechi 438 kwa kipindi cha misimu tisa aliyokaa hapo.