Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Riadha taifa ni vita ya makocha

Imani Pic Data uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha

Thu, 7 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Achana na ushindani wa ndani ya uwanja kwenye mashindano ya Taifa ya riadha yanayofunguliwa kesho jijini Arusha, mchuano mwingine utahamia kwa  makocha wa baadhi ya timu za mikoa ambao wanamategeneo ya kuendeleza rekodi.

Mashindano ya taifa yatafunguliwa kesho saa 4 Asubuhi na mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongella kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa.

Tayari timu zimeanza kuwasili ikiwamo Dar es Salaam, Kusini Pemba na Pwani huku timu za mikoa mingine zikitarajiwa kuwasili wakati wowote kuanzia sasa.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Silas Isangi amesema timu za mikoa yote nchini zitashiriki kwenye mashindano hayo ya siku mbili.

Mbali na mchuamo mastaa wa riadha nchini wakiongozwa na Emmanuel Giniki, Ally Gulam, Regina Mpigachai, Gabriel Geay na wengineo, mchuano mwingine utakuwa kwa makocha wa baadhi ya timu ambao wana mategemeo ya kuendeleza rekodi zao.

Miongoni mwao ni kocha Ron Davis aliyewahi kuinoa timu ya Tanzania iliyoshinda medali ya za Olimpiki ya 1980 na msimu uliopita aliiongoza timu ya Pwani kutwaa ubingwa wa Taifa.

Mwingine ni Samson Ramadhan bingwa narathoni wa michezo ya madola ya 2006 ambaye anakinoa kikosi cha Arusha.

Kocha  mwingine ni Jambau Madai, kocha aliyeibua kipaji cha Alphonce Simbu, Jackline Sakilu, Marco Joseph na wanariadha wengine wengi wazaliwa wa Singida waliotamba na wanaoendelea kutamba nchini.

Jambau atakiongoza kikosi cha Singida kusaka ubingwa msimu huu wakati mwanariadha wa kike, Zakia Mrisho akionyesha ubora wake wa mbinu na ufundi akiwa miongoni mwa makocha wachache wa kike hivi sasa waliokimbia kwa mafanikio enzi zake.

Kwa nyakati tofauti makocha hao wameeleza namna walivyojipanga kwa ushindi kutokana na maandalizi waliyoyafanya kambini.

Arusha yenye wanariadha 35 inaamini itabakisha ubingwa nyumbani huku Samson akisisitiza kwamba mkoa huo ni nyumba ya vipaji.

Ron Davis kocha pekee wa kigeni kwenye mashindano hayo anasema aina ya timu aliyonayo, ubora na hamasa ya kikosi chake watachukua ubingwa kwa mara nyingine.

Wakati Jambau kocha mwenye rekodi ya pekee mkoani Singida akisisitiza kwamba ubingwa wa msimu huu hauna mwenyewe yeyote anaweza kushinda.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz