Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Riadha Taifa yakwama uwanja wa ndege

Riadha Taifaa Riadha Taifa yakwama uwanja wa ndege

Fri, 29 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wachezaji wa timu ya taifa ya Riadha ya Mbio za Nyika wamekubwa na simanzi baada ya safari ya kwenda kushiriki mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika kuahirishwa ghafla wakiwa Uwanja wa Ndege.

Mashindano hayo yanatazamiwa kufanyika kesho Machi 30,2024 mjini Belgrade, Serbia na Tanzania ilikuwa iwakilishwe na wachezaji tisa, nane wenye uzoefu na mmoja kijana wa U-20.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Jackson Ndaweka ameliambia Mwanaspoti mwanzo hadi mwisho sababu iliyokwamisha timu hiyo kusafiri kwenda Serbia, wakati wakiwa wapo tayari Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Ndaweka amesema awali timu hiyo ilitakiwa kuondoka juzi Jumatano (Machi 27, 2024) lakini ikashindikana kutokana na changamoto ya baadhi ya wachezaji kukosa visa za kuingia Serbia na wakiwa njiani kwenda KIA walilazimika kuahirisha safari ili timu iondoke jana Alhamisi (Machi 28).

"RT ilifanya taratibu za kuomba visa tangu Machi 8, pasipoti za wachezaji wote zilitumwa ubalozi wa Serbia ulipopo Nairobi, Kenya lakini hadi kufikia Machi 21 bado tulikuwa hatujafanikiwa kuzipata visa hizo," amesema Ndaweka.

Ameongeza baada ya hapo, waliamua kumtuma kiongozi kutoka Chama cha Riadha Mkoa wa Arusha (ARAA), aliyesafiri hadi jijini Nairobi kufuatilia visa hizo kwa zaidi ya siku tano lakini hadi kufikia juzi Jumatano ni visa za wachezaji watano tu ndizo zilikuwa zimepatikana.

“Wakati tunazipata hizo visa juzi muda wa safari ulikuwa umeshapita, hivyo tukasema basi hao wachezaji watano bora waondoke jana wakati tukiwa tunajaribu tena kufuatilia visa za wengine waliobaki,” amesema Ndaweka.

Ameweka wazi bahati jana ndege iliyokuwa iondoke na wachezaji ilipaswa kuondoka saa 3:50 usiku, lakini ikafika KIA saa 6:40 usiku na ikawa imepangwa iondoke KIA saa 7:50 usiku kwenda Entebbe, Uganda baada ya hapo ndio ipae hadi Amsterdam Uholanzi na ingefika leo saa 8 mchana wakati huo ndege yao ya kuunganisha kwenda Serbia ratiba ilionyesha inaondoka saa nne asubuhi.

“Maana yake ni kwamba kama tungeruhusu wachezaji hao kupanda hiyo ndege wangeenda kufika Amsterdam wakati ndege yao ya kuunganisha kwenda Serbia itakuwa imekwishaondoka,” amesema Ndaweka.

Katibu huyo amesema walizungumza na wasimamizi wa ndege hiyo na waliweka wazi wanaweza kutoa huduma za malazi kwa wanariadha pale Amsterdam, lakini kama RT wakaona hakuna maana tena kwani timu itafika Serbia mashindano yamekwisha tayari.

“Tumelazimika kuchukua maamuzi magumu baada ya kukaa na wachezaji wenyewe tukaona kweli hakuna sababu ya timu hiyo kwenda Serbia tena,” amesema Ndaweka.

Decta Teziforse ni mchezaji aliyetarajia kwenda kushiriki mbio hizo amesema ameumia lakini hakuna namna yoyote ambayo anaweza kufanya, ishatokea na atajipanga tena kwa mbio zingine.

“Dah! Nimeumia sana, ilikuwa ndiyo mashindano yangu ya kwanza na nilijiandaa vyema kuiwakilisha nchi yangu, kiukweli imeniumiza sana lakini hakuna namna nyingine ya kufanya,” amesema Decta.

Mbali ya Decta Teziforse, wachezaji wengine wa timu hiyo ya taifa waliokwama kusafiri ni; Hamida Nassor Mussa, Mau Hando, Anastazia Dolomongo, Neema Festo, Enestina Mngolage, Herman Vitali, Boay Dawi na John Nahhay pamoja na kocha Marcelina Gwandu.

Chanzo: Mwanaspoti