Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi zinaongea ufunguzi wa Ligi kuu

14081 Pic+rekodi TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hebu jiulize, si wageni wala wakongwe wa ligi, kuna timu imepigwa 3-0? Kuna timu imepigwa zaidi ya mabao mawili? jibu hakuna, matokeo ya mwisho ni timu kufungwa 2-0 lakini zaidi ya hapo ni mabao 2-1.

Majibu ya haraka haraka unaweza kusema ligi ya mwaka huu ni ngumu, kwa kuwa mwonekano wa asubuhi uko hivyo. Lakini kuna upande wa pili.

Unaweza kusema ni nguvu ya soda, kwa kuwa timu bado zina umotomoto wa ligi lakini moto ukipoa zinalegea. Ni jambo la kusubiri.

Mwanzo wa Ligi Kuu

Ligi Kuu Bara imeanza kwa kasi msimu huu huku timu nyingi zikionekana kujipanga vilivyo. Timu nane zimeanza kwa kisindo ligi hiyo kwa kupata ushindi wakati nne zikiambulia sare huku mabao 15 yakifungwa katika michezo ya kwanza.

Timu kama, Azam,Kagera Sugar,Yanga,Biashara United,Stand United, Prisons,Mtibwa,Mbao,Stand United na Mbeya City zilionyesha kiwango kizuri cha soka katika michezo yao wakati Simba, Ndanda,Coastal Union, Lipuli, JKT Tanzania, KMC, African Lyon, Alliance FC, Singida United na Mwadui zilionyesha kiwango cha wastani.

Meddy Kagere na rekodi murua

Mshambuliaji wa Simba, Meddy Kagere ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la mapema zaidi kwenye ligi msimu huu akiwa amefunga dakika ya pili tu na kuipa ushindi wa bao 1-0 timu yake dhidi ya Prisons.

Criff Buyoya na Ramadhan Malima-Kadi nyekundu

Criff Buyoya wa KMC na Ramadhan Malima wa Mbeya City hawa wamekuwa na mkosi wa msimu, kwani kuanza na kuanza, wamekuwa wachezaji wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu msimu huu.

Buyoya ndiye aliyeanza kuonyeshwa kadi katika mchezo ulioanza mapema kati ya KMC na JKT uliomalizika kwa suluhu akifuatiwa na Malima aliyeonyeshwa katika mchezo dhidi ya Azam uliomalizika kwa Mbeya City kulala kwa mabao 2-0.

Malima lipata kadi hiyo baada ya kumfanyia madhambu Tafadzwa Kutinyu katika mchezo ambao timu yake ililala kwa mabao 2-0 dhidi ya Azam.

Eliud Ambokile- Kukosa penalti

Mshambuliaji wa Mbeya City ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kukosa penalti. Mchezaji huyo alikosa penalti katika mchezo dhidi ya Azam ambao timu yake ililala kwa mabao 2-0.

Penalti hiyo ilitokana na kipa wa Azam, Razack Abalora kumwangusha Chunga Said wa Mbeya City wakati akitaka kuokoa mpira aliouanzisha vibaya ukanaswa na mchezaji huyo.

Yondani na rekodi ya penalti

Beki na nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga penalti.

Yondani alifunga penalti hiyo dakika ya 40 na kuipa ushindi wa mabao 2-1 timu yake dhidi ya Mtibwa Sugar.

Yanga imeonekana ni moto

Yanga ambayo ilikuwa ikipewa nafasi ndogo ya kufanya vizuri msimu huu kutokana na usajili wake kusuasua imeanza ligi kwa moto baada ya kuifunga timu ngumu ya Mtibwa Sugar mabao 2-1 hivyo kuungana na Azam kuwa timu zilizofunga mabao zaidi ya moja mwanzoni mwa ligi.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara walionyesha soka safi huku mshambuliaji Herietier Makambo akianza kuthibitisha kuwa atakuwa moto wa kuotea mbali kwenye ligi hiyo hivyo mabeki wa timu pinzani wajipange

Simba yawakera mashabiki.

Kama kuna timu ambayo ilifanya mbwembwe za usajili kabla ya msimu wa ligi kuanza basi ni mabingwa watetezi Simba.

Hata hivyo timu hiyo ambayo iliweka kambi Uturuki kwa ajili ya maandalizi msimu iliwakera mashabiki licha ya kupata ushindi wa kwanza wa ligi msimu huu kwa kuifunga bao 1-0 Prisons.

Kiwango kilichoonyeshwa na Simba katika mchezo huo hakikuwavutia mashabiki waliofika uwanjani siku hiyo na hivyo kuibua mijadala mikali kwenye mitandao ya kijamii wakiwaponda wachezaji na benchi la ufundi wakidai inakuwaje timu inashindwa kucheza soka la kueleweka na kupata mabao mengi.

Jambo hilo lilimtoa povu msemaji wa klabu hiyo Haji Manara ambaye alishusha utetezi mzito ingawa hata hivyo bado mashabiki waliendelea kumshambulia.

Kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems amejitetea kwa kusema kuwa hajali kutopata ushindi wa mabao mengi anachoangalia ni kuvuna pointi tatu.

“Nafikiri mashabiki wetu wanapaswa kutulia na kuendelea kuisapoti timu kwani ligi ndio kwanza imeanza.

“Muhimu katika mechi ni kupata pointi tatu iwe tumeshinda bao moja au zaidi. Ligi ni ngumu kila timu imejiandaa hakuna timu rahisi, muhimu ni kupambana kwa nguvu,” anasema Aussems.

Kagera yaendelea kuwa mbabe wa Mwadui

Kagera Sugar imeanza kwa rekodi ya aina yake, imeanza ligi kwa kuongoza huku imeendelea kuwa kiboko ya Mwadui kwenye Ligi Kuu Bara hasa inapocheza katika Uwanja wake wa nyumbani wa Kaitaba Bukoba.

Timu hiyo ilianza ligi msimu huu vizuri baada ya kuichapa Mwadui mabao 2-1 na hivyo kuendelea kuwa kiboko ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Tangu Mwadui ipande daraja kucheza Ligi Kuu mwaka 2015 haijawahi kupata ushindi au hata sare dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja huo.Hiyo inakuwa mara ya nne timu hizo kukutana tangu 2015 na mara zote Kagera Sugar ilishinda ikianza kwa bao 2-0,1-0,1-0 na sasa 2-1.

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amewapa tano wachezaji wake kwa kupata ushindi wa kwanza msimu huu dhidi ya Mwadui huku akikiri ligi ya msimu huu itakuwa moto .

“Hakuna kitu kizuri kama kuanza mchezo wa kwanza wa ligi kwa ushindi kwani inaongeza morali katika kikosi changu. Ligi ya msimu huu itakuwa ngumu sana kwani kila timu imejipanga,” anasema.

Jina la Makambo lachomoza

Wakati ligi inaanza, kuna majina ya wachezaji yalitajwatajwa mno. Majina ya Meddie Kagere, Kichuya, Adam Salamba (Simba), Mrisho Ngassa (Yanga) na Ali Kiba wa Coastal Union lakini jina la Harietier Makambo, limeweka rekodi kwa kutajwa zaidi.

Makambo alisajiliwa kutoka Lupopo ya DR Congo na kutajika kwa kiasi kikubwa kwenye mitandao ya kijamii, magazeti, televisheni na redio.

Makocha wanena.

Kocha wa Singida United, Hemedy Morocco amesema ligi ya msimu huu imeanza kwa kasi na imeonyesha timu zimejiandaa.

“Jinsi ligi ilivyoanza inaonesha kuwa msimu huu mambo yatakuwa balaa, ukizembea basi kazi unayo.

“Licha ya kwamba kuna changamoto ya kukosa mdhamini wa ligi lakini bado timu zote zinapambana kuhakikisha zinafanya vizuri. Kama tukiendelea hivi basi ligi itakuwa na ubora mkubwa,” anasema Morocco.

Naye kocha msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal’Billo’ anasema ligi ya msimu huu inaonekana itakuwa tofauti na mwaka jana kwani kila timu haitaki mchezo.

“Huu nimwanzo tu zinatoa picha jinsi mambo yatakavyokuwa magumu. Ukiangalia imeanza na mabao machache tofauti na msimu uliopita. Yaani timu unaona kabisa hata kama imepoteza mchezo basi ni bahati mbaya”alisema Billo.

Kocha wa JKT Ruvu, Bakari Shime anasema bado ni mapema kutabiri Ligi ya msimu huu itakuwaje kwani ndio kwanza kila timu imecheza mechi moja moja.

“Ni mapema sana, tusubiri labda hata tukicheza mechi tano kwa sababu ukiangali kuna timu bado ngeni zinacheza kwa presha, nyingine ni wazoefu wa ligi lakini bado hawajakaa sawa hivyo ni vigumu kutabiri”alisema Shime.

Kocha wa Mbeya City,Ramadhan Nswanzurwimo amelia na waamuzi wa Ligi Kuu kuwa wanatakiwa kuchezesha kwa haki na kuepuka kuwa na matokeo yao mfukoni.

“Ligi imeanza vizuri lakini ukiangalia tayari waamuzi wameshaanza mambo yao ya kuingia kuchezesha wakiwa na matokeo yao jambo ambalo sio zuri. Wafuate sheria na wachezeshe kwa haki ili ligi iwe bora na timu zionyeshe soka ili mwishoni mwa ligi bingwa apatikane kwa haki”alisema Nswanzurwimo.

Chanzo: mwananchi.co.tz