Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi zaibeba Stars ikicheza na Burundi

74740 Stars+pic

Mon, 9 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakuna namna Burundi ni lazima wafugwe leo watakapoikabili timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, ingawa vijana wa kocha Etienne Ndayiragije wanatakiwa kuingia uwanjani kwa tahadhari licha ya rekodi kuwabeba.

Stars itapambana na Burundi ukiwa ni mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Septemba 4 mjini Bujumbura, timu hizo zilifungana bao 1-1.

Taifa Stars inahitaji ushindi au suluhu ili kusonga mbele kwenye hatua ya makundi ya kusaka nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2022, Qatar.

Rekodi zinaibeba Taifa Stars dhidi ya Burundi kwani katika mashindano yote tangu 1971 timu hizo zimekutana mara 18, Stars ikishinda michezo 11, imepoteza mitano na kutoa sare mitatu. Michezo hiyo inahusisha mechi za kirafiki, mashindano ya Cecafa Chalenji, kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia.

Pia katika michezo 12 waliyokutana kwenye ardhi ya Tanzania, Taifa Stars imeshinda mechi nane, Burundi ikashinda tatu na kutoka sare moja. Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kuwa timu hizo zimekuwa na viwango vinavyoshabihiana kwa miaka mitatu mfululizo, hivyo kuonyesha kuwa mechi ya leo haitakuwa rahisi.

Katika michezo 20 iliyocheza tangu 2017, Stars imeshinda minne, imetoka sare mara sita na kupoteza mechi 10 ilhali Burundi imecheza michezo 20, imeshinda minne, imetoa sare sita na kupoteza saba.

Pia Soma

Advertisement
Ushindi mkubwa ambao Taifa Stars imepata tangu mwaka huo ni wa mabao 3-0 ilipoifunga Uganda, Machi 24, mwaka huu na kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), wakati kipigo kikubwa ilichopata ni mabao 4-1 ilipochapwa na Algeria katika mechi ya kirafiki iliyofanyika Machi 22, mwaka jana.

Kwa upande wa Burundi, ushindi mkubwa ambao imewahi kupata tangu mwaka huo ni ilipoichapa Sudan mabao 5-2, Novemba 16, 2018 katika mchezo wa kuwania kufuzu Afcon na kipigo kikubwa ilikipata kwa kufungwa mabao 2-0 na Guinea kwenye fainali za Afcon huko Misri mwaka huu .

Vivutio uwanjani

Kuna vitu vilikuwa kivutio kikubwa katika mchezo wa kwanza baina ya Stars na Burundi uliofanyika mjini Bujumbura, Septemba 4 na vinatarajiwa kuwa kivutio hata katika mchezo wa leo.

Katika mchezo huo licha ya manahodha wa mataifa hayo, Mbwana Samatta (Tanzania) na Saido Berahino (Burundi) kucheza Ligi Kuu ya Ubelgiji, pia makipa wa timu hizo Juma Kaseja (Tanzania) na Jonathan Nahimana (Burundi) wanachezea KMC inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Jambo lingine ni makocha wakuu wa vikosi hivyo kuwa na uraia wa Burundi, Etienne Ndayiragije wa Taifa Stars na Olivier Niyungeko wakati wafungaji wa mchezo wa kwanza wote wanacheza Uarabuni, Cedric Amissi (Burundi) akikipiga Al-Taawoun FC ya Saud Arabia na Saimon Msuva akikiwasha Difaa El Jadida ya Morocco.

Stars, Burundi wanasemaje?

Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda alisema wameyafanyia kazi makosa yaliyotokea kwenye mchezo wa kwanza na wachezaji wake wako tayari kwa mchezo wa leo.

“Mechi iliyopita kulikuwa na upungufu hasa eneo la ulinzi na katika mazoezi yetu tumeufanyia kazi, hivyo ni jinsi gani tumejipanga kuhakikisha tunapata mabao na kuzuia tusifungwe pia,” alisema Mgunda.

Nahodha wa Stars, Mbwana Samatta alisema wana morali ya juu na anaamini watapata ushindi dhidi ya Burundi kwani watakuwa na sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki na Watanzania kwa ujumla.

“Kila mchezaji yuko tayari, morali iko juu sana kutokana na matokeo ya mechi ya kwanza na tunatarajia matokeo Jumapili yatakuwa mazuri,” alisema Samatta.

Kocha wa Burundi, Niyungeko alisema wamekuja kuangalia jinsi gani wataweza kupata ushindi dhidi ya Tanzania huku akikiri kuwa mechi itakuwa ngumu.

Chanzo: mwananchi.co.tz