Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi za kibabe zinazobamba Simba

70225 Rekodi+pic

Wed, 7 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

WAKATI Simba ikitimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Tamasha lao la Simba Day linalofanyika Agosti 6, timu hiyo imeendelea kushikilia rekodi tamu za kusisimua katika historia ya soka Afrika Mashariki.

Simba itahitimisha kilele cha Simba Day leo kwa kucheza na Power Dynamos ya Zambia katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kuipiga Yanga bao 6-0

Bado Simba inashikilia rekodi hii ya kuwa timu iliyoichapa Yanga mabao mengi zaidi katika mechi ya watani wa jadi mpaka sasa. Julai 19, 1977 iliiifunga Yanga mabao 6-0 ikiwa kama kulipa kisasi cha miaka tisa cha kufungwa mabao 5-0 na watoto hao wa Jangwani katika mchezo uliofanyika Juni Mosi mwaka 1968.

Katika mchezo huo, Abdallah Kibadeni aliweka rekodi ya kufunga mabao matatu ‘hat trick’ huku mabao mengine yakifungwa na Jumanne Hassan ‘Masimenti’ aliyefunga mawili na lingine likifungwa na Selemani Sanga wa Yanga aliyejifunga.

Yaipiga tena Yanga tano

Simba iliendeleza ubabe kwa Yanga baada ya kuifunga mabao 5-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Mei 6, 2012.

Mabao ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na Emmanuel Okwi aliyefunga mawili huku mengine yakifungwa na Patrick Mafisango (marehemu), kipa Juma Kaseja na Felix Sunzu. Tangu wakati huo Yanga haijawahi kulipa kisasi kwa Simba, hivyo Wekundu wa Msimbazi kuendelea kushikilia rekodi hii.

Vinara wa Kagame

Simba ndio timu pekee mpaka sasa imechukua mara nyingi ubingwa wa Kombe la Kagame tangu mashindano hayo yaanzishwe ikiwa imechukua mara sita. Timu hiyo imechukua ubingwa mwaka 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002 - rekodi ambazo mpaka sasa hakuna ambaye ameivunja.

Baadhi ya timu kama Yanga, Gor Mahia, FC Leopard zote za Kenya zimewahi kuchukua mara tano tu.

Pia Simba ndio timu ya kwanza kutwaa kombe hilo pindi tu lilipoanzishwa mwaka 1974 huku ikiongoza kucheza mara nyingi fainali za kombe la Kagame, ikiwa imecheza mara 11.

Rekodi za kibabe zinazobamba Simba

Kwenye Tusker pia wamo

Sio vinara wa Kagame tu, pia Wekundu wa Msimbazi ni vinara wa kuchukua mara nyingi Kombe la Tusker. Simba imechukua kombe hilo mara tano 2001, 2002, 2003, 2004 na 2005.

Ligi ya Mabingwa

Simba imeshiriki mara 17 Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwemo wakati huo likijulikana kama Kombe la Mabingwa wa Afrika na kuweka rekodi ya kutinga robo fainali ya mashindano hayo mwaka jana.

ni mara ya pili Simba ilifika hatua hiyo baada ya kufanya hivyo pia mwaka 1994.Pia imewahi kutinga hatua ya makundi mwaka 2003 ilipowatoa mabingwa watetezi Zamaleki ya Misri.

Kombe la Caf

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wamewahi kuweka rekodi ya kutinga fainali ya Kombe la Caf mwaka 1993 na kuwazidi watani zao Yanga, ambao mara mbili walitolewa katika hatua ya awali katika mashindano hayo.

Chanzo: mwananchi.co.tz