Arusha . Rekodi iliyowekwa na mwanariadha maarufu wa Kenya Eliud Kipchoge kwenye mbio za Berlin Marathoni zimemwibua Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelim Gidabuday.
Akizungumza jana Jumanne, Gidabuday amesema Tanzania inapaswa kuiga mfano wa Kenya katika kuwekeza kwa wanariadha.
Katibu Mkuu huyo alisema Kipchoge ni matunda ya uwekezaji mzuri katika sekta ya michezo, hivyo alitoa raia kwa wadau ikiwemo Serikali kudhamini.
Kipchoge alitwaa medali ya dhahabu katika mbio zilizofanyika Ujerumani akitumia saa 2:01:40 na kuvuna dola 100,000 (Sh 220 Milioni).
Gidabuday alisema kuwa mwanariadha huyo alistahili kushinda kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali, makocha na wadau kulinganisha na Tanzania.
“Kenya wanastahili kuvunja rekodi wamefanya uwekezaji mkubwa na wanaungwa mkono na Serikali, pia wana makocha wazuri, kambi, vifaa na miundombinu ya mazoezi ipo kwenye kiwango bora,” alisema
Gidabuday.
Katika hatua nyingine, Gidabuday alisema timu ya Taifa imeanza mazoezi kujiandaa na mbio za nusu marathon za Jumuiya ya Mdola zitazofanyika katika mji wa Cardiff, Uingereza Oktoba 7.