Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi ya Kagere, Makambo usipime

61239 Makambo+pic

Tue, 4 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Washambuliaji wa kigeni Meddie Kagere na Heritier Makambo ni majina makubwa yaliyotikisa katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Unapozungumzia mafanikio ya Simba huwezi kumuweka kando Kagere ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuiwezesha kutwaa ubingwa msimu huu kutokana na kasi yake ya kufunga mabao.

Pia Yanga iliyomaliza katika nafasi ya pili licha ya wengi kutoipa nafasi ya kutwaa ubingwa au kumaliza katika nafasi mbili za juu, ilitoa mshindani mkali kwa Simba katika mbio za kutwaa ubingwa.

Jeuri ya Yanga dhidi ya Simba ilichangiwa na Makambo anayetoka DR ya Congo ambaye ufanisi wake katika safu ya ushambuliaji ulikuwa chachu kwa timu hiyo ya Jangwani.

Lakini ikumbukwe wachezaji hao wote wawili wamefanya vizuri katika timu hizo ukiwa ni msimu wao kwanza baada ya kujiunga nazo kwenye dirisha kubwa la usajili baada ya kumalizika msimu wa Ligi Kuu 2017/2018.

Spoti Mikiki inakuletea tathimini namna Makambo aliyetua Yanga akitokea FC Lupopo na Kagere raia wa Rwanda aliyesajiliwa akitokea Gor Mahia walivyokuwa nguzo kwa miamba hiyo ya soka nchini.

Pia Soma

Kagere amemaliza akiwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao 23 katika mechi 31 alizocheza Simba kwenye ligi hiyo mbele ya Makambo na Salim Aiyee wa Mwadui ambao kila mmoja amefumania nyavu mara 17.

Kagere mwenye umri wa miaka 32, yeye pekee ameichangia Simba takribani pointi 22 sawa na asilimia 25.28 ya pointi zote 93 kutokana na mabao aliyoyafunga katika mechi nane (8) ambayo yaliweza kuamua mechi hizo na pengine asingeyafunga, Simba ingemaliza ligi ikiwa na pointi 69.

Nyavu za Uwanja wa Taifa ndizo zinaongozwa kutikiswa zaidi na Kagere kwani amefunga mabao tisa kwenye uwanja huo na unafuatiwa na ule wa Uhuru ambako Kagere amepachika mabao matano na unaofuatia ni Mkwakwani, Tanga alikofunga mabao manne na viwanja vya Sokoine Mbeya, Kambarage (Shinyanga), Namfua (Singida) na Samora Iringa, kila mmoja amepachika bao moja.

Kati ya timu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu msimu huu, 12 zimeonja makali ya Kagere baada ya kufumania nyavu dhidi yao nazo ni Lipuli, Yanga, Prisons, Singida United, Mbao, Mwadui, Ruvu Shooting, Azam, Ndanda, JKT Tanzania, Mbeya City na Coastal Union wakati timu saba ambazo Kagere hajafumania nyavu zao ni Kagera Sugar, Alliance, KMC, Stand United, African Lyon, Biashara United na Mtibwa Sugar.

Amefunga mabao 23 katika mechi 16 na mchango wake haukuishia katika kufunga mabao tu, kwani kati ya mechi 38 ambazo Simba ilicheza hadi sasa, mshambuliaji huyo raia wa Rwanda amecheza mechi 31 ambazo ni sawa na asilimia 86.11 ya mechi zote.

Makambo

Makambo alisajiliwa kwa Dola 15,000 (Sh34.2 milioni) akionekana si mchezaji ambaye atakuja kuwa na msaada kwa Yanga lakini baadaye aligeuka lulu na nyota muhimu akimaliza katika nafasi ya pili kwenye mbio za kusaka mfungaji bora akipachika mabao 17.

Silaha kubwa kwa Makambo katika kufunga ni kichwa chake ambapo amefunga mabao 10 ya vichwa na mguu wake wa kushoto ukifunga mabao sita huku mguu wa kulia akiutumia kufunga bao moja pekee.

Ni mchezaji anayejua vyema kukaa kwenye nafasi, kuwasumbua na ujanja wa kuwatoroka mabeki jambo ambalo limekuwa likiwapa taabu mabeki wa timu pinzani kumdhibiti hasa Yanga inapofanya shambulizi la kona au faulo.

Kati ya mabao 17 aliyofunga, hakuna hata moja la mkwaju wa penalti na hiyo imechangiwa na kutokuwa na rekodi nzuri ya upigaji penalti kwani ni penalti moja tu aliwahi kupiga dhidi ya Alliance Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambayo iliokolewa.

Kutokana na mchango na juhudi zake ndani ya uwanja, haikushangaza kuona klabu ya Horoya ya Guinea ikimnyakua kwa dau nono la Dola 100,000 ( sh 228 milioni) ili aitumikie kwa kwenye msimu ujao.

Chanzo: mwananchi.co.tz