Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro, jana alishindwa kuingia uwanjani kutazama mechi ya Ligi Kuu nchini humo kati ya Santos na Gremio baada ya kuzuiwa kwa kuwa hajapata chanjo ya Corona.
Iko wazi duniani kote kuwa Bolsonaro amekuwa mstari wa mbele kupinga chanjo ya ugonjwa huo akisema hana imani nazo na mwili wake uko vizuri hata bila ya kuchanjwa.
Hivi karibuni, alilazimika kula ‘pizza’ yake akiwa kando ya barabara na hiyo ni baada ya kuzuiwa kuingia kwenye mgahawa jijini New York, Marekani, ambako kuchanjwa ni kipaumbele katika kupata huduma.
Akizungumza baada ya kuzuiwa kuingia uwanjani, kiongozi huyo amesema: “Kwanini niwe na hati ya chanjo (ya COVID-19)? Nilitaka kutazama mechi ya Santos lakini nikaambiwa nichanje. Kwanini iwe hivyo?”