Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais ameagiza mambo haya 10 kwa jeshi la polisi

94d53f92f892ed614fb7a12bd7ea2faf.jpeg Rais ameagiza mambo haya 10 kwa jeshi la polisi

Thu, 26 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo takribani 10 kwa Jeshi la Polisi nchini ikiwemo kuwataka kuangalia uwezekano wa kubadilisha sheria ya kuweka mtu mahabusu, kudhibiti matumizi ya nguvu katika vituo vya polisi pamoja na kusimamia haki na kuzingatia maadili ya kazi yao.

Rais Samia aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua kikao kazi cha maofisa wakuu wa makao makuu, makamanda wa mikoa na vikosi vya Jeshi la Polisi.

“Sote tunafahamu kwamba amani na usalama ndio msingi wa maendeleo katika nchi. Jeshi la Polisi limepewa jukumu la kusimamia utulivu na usalama wa raia na mali zao ndani ya nchi hii. Hili ni jukumu kubwa sana, ni jukumu ambalo likitendeka vizuri basi shughuli zote za kisiasa na kiuchumi na shughuli nyingine zote za kijamii zitakwenda vyema na nchi itapata maendeleo ya kutosha,” alisisitiza Rais Samia.

Alisema pamoja na Jeshi la Polisi kufanya vizuri katika mambo mengi, lakini bado kuna changamoto ya ucheleweshaji wa upelelezi pamoja na kukosekana au kupungua kwa uadilifu, nidhamu na maadili kwa baadhi ya askari.

Alisema kutokana na changamoto hiyo kesi zimekuwa zikikwama mahakamani kutokana na kucheleweshwa kwa upelelezi au kwamba hazina ushahidi na zikiwemo zile zinazoitwa za kubambikiza.

“Lakini nawapongeza kwa uamuzi wenu wa kuweka ukomo wa kufanya upelelezi kufikia miezi sita kesi ndogo na mwaka kesi kubwa, lakini bado tunaweza tukafanya vizuri zaidi. Kwa sababu kucheleweshwa kwa upelelezi kunaongeza mzigo mkubwa kwa serikali kuweka mahabusu jela,” alisema Rais Samia.

Alisema kwa mujibu wa takwimu hadi mwezi huu, idadi ya mahabusu katika jela ni karibu sawa na wafungwa ambapo kuna jumla ya wafungwa 16,542 na mahabusu 15,194.

“Sasa kwa hawa wapo waliokaa wiki, miaka mitatu na kila anayeguswa upelelezi haujakamilika,” alieleza.

Alitoa wito kwa jeshi hilo kuwa kama halina uhakika kwamba upelelezi hautakamilika katika kesi zilizopo, watu wanaoshikiliwa kuhusiana na kesi hizo waachiwe huru na kwa zile kesi ambazo wana uhakika upelelezi utatimia, upelelezi uharakishwe.

Aidha, aliagiza jeshi hilo kuangalia uwezekano wa kubadilisha sheria ya kuweka mtu mahabusu.

“Nchi nyingine mtu hakamatwi mpaka upelelezi umetimia, akikamatwa anawekwa ndani wiki, siku tatu, nne tayari mahakamani anahukumiwa anaendelea. Huwezi kukuta serikali inabeba mzigo wa mahabusu kwa maelfu walioko ndani ambao ushahidi au upelelezi haujakamilia angalieni hili ili tutoe huduma njema kwa watu wetu,” alisema.

Katika eneo la haki kwa jamii, Rais Samia alisema huo ni wajibu mkubwa kwa jeshi hilo, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya askari wamekuwa wakishutumiwa kwa kutofanya haki kwa jamii.

Alisema inapotokea askari kutuhumiwa kutotenda haki, jeshi hilo limekuwa likisimama na kujitetea haraka bila kuangalia haki za jamii.

Alitolea mfano, miezi miwili iliyopita kulikuwa na unyang’anyi wa nyama za watu uliofanywa na baadhi ya askari polisi.

“Mlivamia bucha mkachukua nyama walipolalamika mkasema mmefanya vile kwa sheria lakini kilichotendeka hakuna sheria hapo. Hebu jiangalieni tupo hapa kuangalia watu, si kudidimiza watu,” alieleza.

Pamoja na hayo, alisema suala la Polisi kutumia mabavu au mtuhumiwa kufa akiwa mikononi mwao ni jambo la kufanyiwa kazi lisijitokeze nchini.

“Umechukua huko umemburuza, umemchapa virungu vya kutosha, binadamu tupo tofauti kuna mwingine unamchapa virungu yupo ngangari mwingine vifimbo viwili yupo mbele ya haki. Kwa hiyo masuala ya matumizi makubwa ya nguvu na yenyewe muyatizame, kesi za kufa watu kwenye vituo vya polisi hazileti sifa nzuri kwa polisi na serikali naomba sana ndugu zangu tendeni haki,” alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia pamoja na kuupongeza wimbo maalumu wa jeshi hilo, alieleza kuwa kuna baadhi ya askari wanaharibu maneno ya wimbo huo kutokana na kufanya vitendo kinyume cha maadili jambo linalotia doa jeshi hilo.

Alisema alishawahi kueleza kuwa yai viza moja likiwa kwenye mayai mazima, kutokana na harufu yake huharibu pia mayai mengine na kufananisha mfano huo na vitendo vinavyotokea ndani ya Jeshi la Polisi.

“Wachache wakiharibu maadili ya jeshi la polisi yanatapakaa zaidi kuliko yale mazuri mnayoyafanya. Hakikisheni watu wenu wanafanya yale yaliyomo katika wimbo wenu. Naomba mwende na kiapo chenu,” alisema.

Aidha, amelitaka pia kusisitizia juu ya mafunzo ya mara kwa mara kwa askari wake ili kuendana na mabadiliko ya utandawazi ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

“Ni aibu kuona kwenye simu tunarushiwa clip (kipande cha video) askari anajadiliana na raia kuhusu rushwa hasa upande wa trafiki (Askari wa Usalama Barabarani). Askari anachukua rushwa bila aibu na mambo ya teknolojia mtu anakurekodi kwa kalamu tu. Zipo clip nyingi tu, aibu hii kaishughulikieni,” aliagiza.

Pamoja na hayo, alisema kutokana na kukua kwa utandawazi, pia uhalifu wa kimataifa wa kutumia mitandao unazidi kuongezeka ambapo kumekuwa na watu wengi wanaonyanyaswa kupitia mitandao hiyo.

Alisema mbaya zaidi anayenyanyasa anatumia laini ambayo hata akitafutwa hapatikani kwani laini husika husoma kuwa ni ya nchi za nje na kulitaka jeshi hilo kujipanga vyema kukabiliana na uhalifu wa aina hiyo kwani kama upo kwenye mitandao, usalama wa nchi wenyewe utakuwaje.

Sambamba na hayo, alisema dunia kwa sasa iko kwenye wimbi la nne la mapinduzi ya viwanda linaloongozwa na mifumo ya Tehama na kusisitiza kuwa lazima jeshi hilo lijipange katika mwelekeo wa kuendana na mifumo hiyo.

Alisema mfumo huo uliokuja duniani wa Tehama, umekuja na usalama lakini pia umekuja na makosa mengi. “Makosa mengi ni ya kuvuka mipaka, kwa hiyo Jeshi la Polisi lazima tujitayarishe kwa ndani na nje ya nchi pia, najua kuwa mnafanyakazi nzuri sana kushirikiana na majirani na vyombo vingine duniani vya ulinzi na usalama,” alieleza.

Alisema ni vema lijipange vizuri, ili kwenda sambamba na yale yanayokuja duniani kwani mfumo huo unakuza ugaidi kwa sababu magaidi sasa wana njia zote za urahisi za kuwasiliana na wana njia zote za urahisi za kupeana mipango.

Aidha, alisema pia biashara zote haramu, dawa za kulevya lakini pia usafirishaji wa watu na wenyewe unafanyika kimtandao zaidi pamoja na kwamba vyombo vinavyosafirisha watu ni vyombo vinavyoonekana, lakini mipango ya mambo hayo inakwenda kimtandao zaidi.

Kuhusu polisi kukaa kwenye makazi ya raia, alisema pamoja na kwamba inasaidia kuwa karibu na wananchi, lakini pia inasababisha baadghi ya askari kuwa karibu zaidi na jamii na kushindwa kufanya kazi yao

“Mfano Unguja na Pemba kutokana na upungufu wa nyumba za polisi, polisi wetu wanakaa ndani ya jamii, kupanga kwao kunawafanya wazoeleke sana na jamii na hata mhalifu ni jirani yake atasita sana kumsema kwamba ni mhalifu hili liangalieni. Njia nzuri ni kuwatenga polisi na makazi ya watu,” alisema.

Alihidi kushughulikia zaidi changamoto zao na kuboresha kila linalowezekana kulingana na hali ya kifedha ya serikali.

Alisema pia serikali itakuja na maamuzi mazuri hivi karibuni kuhusu mkataba wa Jeshi la Polisi wa kutekeleza mradi wa Oysterbay ambao utasaidia jeshi hilo kujiongezea kipato.

Aidha, ameliagiza pamoja na kwamba watu wanaoijaribu serikali wamedhibitiwa hali si shwari hasa mikoani na kulitaka kudhibiti matukio ya unyang’anyi na ujambazi.

Kuhusu Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa jeshi hilo, aliwataka waweke uratibu madhubuti wa kuhakikisha kila mkoa unafanya vizuri na mpango huo kusimamiwa ili kuendana na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Simon Sirro alisema pamoja na kwamba wanaendelea na mikakati ya kudhibiti makosa ya uhalifu, makosa mengi yamepungua ikiwemo ujambazi, unyang’anyi na ya barabarani.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene alielezea kikao kazi hicho cha maofisa wakuu wa jeshi hilo kwa ajili ya kujadili mikakati ya utekelezaji ya jeshi hilo.

Alimshukuru Rais kwa kutoa ajira 3,103 kwa ajili ya vyombo vya usalama na kuahidi kuwa watakaopatiwa ajira hizo ni wale wanaostahili na wenye sifa tu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz