Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais RT aitaka mikoa kuandaa mashindano kupata timu za U18, U-20

Rais RT Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Silas Isangi

Fri, 3 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Silas Isangi ameitaka mikoa yote nchini kuhakikisha inaandaa mashindano kwa ajili ya kuchagua timu ya taifa chini ya umri wa miaka 18 na 20.

Isangi ametoa agizo hilo leo Ijumaa Februari 3, 2023 jijini Mwanza katika mkutano na waandishi wa habari, huku akisisitiza kila chama cha riadha cha mkoa lazima kufanya mashindano ngazi ya mkoa ili mashindano ya taifa yawe na tija.

Wito huo umekuja huku Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Afrika Mashariki kwa vijana chini ya miaka 18 na 20 yatakayofanyika Dar es Salaam Machi 10-11, mwaka huu.

Pia Tanzania inajiandaa kushiriki mashindano ya Afrika ya vijana chini ya miaka 18 na 20 yatakayofanyika Lusaka, Zambia kuanzia Aprili 27 hadi Mei 3 na yale ya Jumuiya ya Madola kwa vijana chini ya miaka 18 yatakayofanyika Trinidad and Tobago Agosti 4 hadi 11.

"Mashindano yote hatuwezi kufanya vizuri kama timu itachaguliwa kwa ngazi ya taifa tu kwa maana wachezaji wanatokea huko mikoani na riadha taifa haina mchezaji wa kushiriki, lazima viongozi wa riadha kuanzia wilaya ambao ndiyo wenye klabu wajitume na kutimiza wajibu wao," anasema Isangi na kuongeza;

"Ni aibu mkoa kuleta mchezaji kwenye mashindano yenye hadhi ya kitaifa akiwa anakimbia kama (Joggers), wachezaji waandaliwe waje kushindana na siyo kuwa kama tiketi ya viongozi kuja kutembea mikoani."

RT imewaagiza pia viongozi wa vyama vya mikoa kuimarisha mchezo huo katika maeneo yao kwa kuandaa mashindano ya mikoa na mkutano mkuu.

Tanzania itashiriki pia mashindano ya mbio za nyika (Cross Country), Februari 18, Australia, All African Games na yale ya dunia yatakayofanyika kuanzia Julai 4, hadi 23, nchini Ghana.

Chanzo: Mwanaspoti