Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RUSSIA 2018: Wenye mabao yao huko Russia 2018

9309 ROMELU TZW

Sat, 16 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

MOSCOW, RUSSIA. ULE utamu ndo umeshaanza. Unauliza utamu gani? Ni Kombe la Dunia bana.

Russia kumenoga, jana Alhamisi utepe ulikwanza na mambo ndio yanazidi kunoga hadi hiyo Julai 15, itakayopigwa mechi ya mwisho ya fainali kukamilisha fainali hizo za Kombe la Dunia 2018.

Kama ilivyo kawaida, Kombe la Dunia halikosi vituko. Hispania wametimua kocha wao hata kabla ya fainali kuanza, kisha kajitangaza kuungana na Real Madrid msimu ujao kwamba anakwenda kuwa kocha wa timu hiyo ya Bernabeu baada ya Mfaransa Zinedine Zidane kubwaga manyanga. Wakati hayo yakiendelea na maswali mengi yakiulizwa kuhusu nani atakuwa bingwa, lakini swali jingine kubwa na maarufu linaloulizwa juu ya nani atabeba ile tuzo ya Mfungaji Bora kwenye fainali hizo za Russia?

Wazee wa kubeti wameshaweka mezani majina yao ambayo wanaamini piga ua, basi kinara wa kufunga kwenye fainali hizo za Russia basi hawezi kutoka nje ya orodha hiyo kutokana na ukweli kwamba ni wakali wa kupasia nyavu.

Luis Suarez

(Uruguay)

Straika huyo amekuwa na rekodi chafu kwenye michuano mikubwa hasa hii ya Kombe la Dunia. Mwaka 2010 alidaka mpira uliokuwa unatinga wavuni makusudi kabisa kwenye mechi dhidi ya Ghana, lakini kwenye fainali za 2014, alimng’ata beki wa kati wa Italia, Giorgio Chiellini na kujikuta akukumbana na adhabu ya kufungiwa miezi minne kujihusisha na kitu kinachohusu mpira. Lakini, hilo halina maana kwamba Suarez hafahamu namna ya kupasia mipira nyavuni na ndio maana anapewa nafasi kubwa ya kuwa mmoja watakaotikisa kwa mabao kwenye fainali hizo za Russia hasa kutakana na kile ambacho amekuwa akikifanya kwenye kikosi cha Barcelona.

Edinson Cavani

(Uruguay)

Kuna mwenye swali kuhusu uwezo wa Edinson Cavani anapokuwa mbele ya goli la wapinzani? Kitu kibaya zaidi kwa wapinzani watakaomkabili staa huyo huko Russia ni kwamba atakuwa akiunda pacha matata na mwenzake, Luis Suarez, wawili hao wote balaa. Cavani amekuwa na msimu bora kabisa huko Paris Saint-Germain na matarajio ni makubwa kwamba anaweza kwenda kuendeleza makali hayo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Baada ya kufunga mabao 40 katika michuano yote aliyocheza kwenye kikosi chake cha PSG msimu uliopita, Cavani anaweza kuweka akiba kubwa ya mabao hasa kutokana na wapinzani atakaokabiliana nao kwenye hatua ya makundi ambao ni Misri, Saudi Arabia na Russia.

Cristiano Ronaldo

(Ureno)

Akiwa na umri wa miaka 33, pengine hii inaweza kuwa nafasi ya mwisho kwa Ronaldo kushinda ubingwa wa dunia, kwa sababu baada ya hapo, hatarajiwi kama atakuwapo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, licha ya kwamba kwa namna anavyojiweka fiti, anaweza kuwa vizuri kwenda kucheza fainali hizo akiwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kwa sababu kipindi hicho atakuwa na umri wa miaka 37. Ronaldo anakwenda kwenye fainali za Russia akiwa amerudi kwenye ubora wake huku akichangizwa zaidi na ubingwa mara tatu mfululizo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Baada ya kuboronga kwenye fainali zilizopita huko Brazil, hiki kinaweza kuwa kipindi mwafaka kwa Ronaldo kufanya mambo tofauti.

Gabriel Jesus

(Brazil)

Uzuri wa Gabriel Jesus hatakwenda Russia akiwa na presha kubwa, hivyo anaweza kuwa na nafasi nzuri ya kufunga mabao na kujitengenezea mazingira ya kuwa kinara wa mabao kwenye fainali hizo. Kuhusu uwezo wa kupasia nyavu hilo halina mjadala, Jesus amekuwa akilifanya kwenye uwezo mkubwa sana. Baada ya kuisaidia Manchester City kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita, mshambuliaji huyo wa Kibrazili atakwenda kuisaidia taifa lake la Brazil huko kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Jesus ni mmoja wa wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kwenda kupiga mabao kwenye fainali hizo za Russia.

Romelu Lukaku (

Ubelgiji)

Akibarikiwa kasi na nguvu, Lukaku alikuwa jinamizi kubwa kwa mabeki wa Ligi Kuu England kwa miaka ya karibuni. Hakika ni mmoja wa mastaa wanaotengeneza kizazi cha dhahabu cha Ubelgiji, hivyo kinachosubiriwa kama ataweza kwenda kuhamishia makali yake kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Akiwa chini ya kocha Roberto Martinez, aliyewahi kufanya kazi naye huko Everton, Lukaku, ambaye ni mshambuliaji wa Manchester United anatarajiwa kwenda kutamba kwenye fainali za Russia huku akitajwa kwenye orodha ya wale ambao wanaweza kushindania Kiatu cha Dhahabu kwa kuongoza kwa mabao.

Harry Kane (

England)

Straika, Harry Kane ndiye nahodha wa England na maswali wanayojiuliza Waingereza wengi kama mshambuliaji huyo atakuwa Mwingereza wa pili kunyanyua juu taji la Kombe la Dunia baada ya kufanya hivyo Bobby Moore mwaka 1966. Nafasi ni finyu sana kutokana na ubota wa kikosi cha England ulivyo ukilinganisha na vikosi vingine vilivyopo kwenye fainali hizo. Kitu kizuri ni kwamba Kane anakwenda kwenye fainali hizo akiwa kwenye kiwango bora kabisa, yawezekana timu yake isipate mafanikio ya kubeba ubingwa, lakini kutokana na uhodari wake wa kutupia mipira wavuni, anaweza kufikiria mafanikio binafsi na kuwa kinara wa mabao.

Timo Werner

(Ujerumani)

Timo Werner anaweza kuwa staa mkubwa sana na kubamba dili la maana baada ya fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia. Kwenye michuano hiyo, mshambuliaji huyo wa Red Bull Leipzig atakuwa na kikosi cha Ujerumani na hasa ukizingatia kwamba anacheza na wakali wa kupiga pasi za mwisho kama Mesut Ozil na Toni Kroos, basi Werner anaweza kuwa mbaya zaidi kwenye kuwatesa makipa na hatimaye anaweza kujisogeza kwenye orodha ya wale ambao wataacha alama zao huko Russia kwa maana ya kujibebea Kiatu cha Dhahabu. Kiwango kizuri kinaweza kumpa dili matata ambapo Real Madrid wanahusishwa na mpango wa kumsajili.

Antoine Griezmann

(Ufaransa)

Mshindi wa Kiatu cha Dhahabu kwenye Euro 2016, Griezmann ameonekana kupevuka zaidi jambo ambalo linaweza kumfanya kwenye kuwa mtu hatari zaidi kwa kufunga mabao kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Ufaransa ya sasa ina wachezaji wengi sana na walio mahiri hasa kwenye sehemu yao ya ushambuliaji huko Griezmann akiwa mmoja wa wachezaji wanaotazamiwa kwenda kufanya mambo makubwa katika fainali hizo. Kuhusu kufunga hilo halijawahi kuwa jambo gumu kwa Griezmann na ndiyo maana anapewa nafasi ya kuwa mmoja wa wakali watakaotikisa nyavu kwa wingi huko Russia.

Lionel Messi

(Argentina)

Kama ilivyo tu kwa Cristiano Ronaldo, kushindwa kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka huu kunaweza kuwa fainali za mwisho kwa staa wa Kiargentina, Lionel Messi. Haionekani kama Messi atakuwa fiti kwa kiwango kinachopaswa kuwa wakati wa fainali za Qatar zitakapofika na ndio maana huu unaonekana kuwa ni wakati wake wa kuandika jina lake kwenye rekodi bora kabisa. Yawezekana kwamba Messi akashindwa kuipa ubingwa wa dunia Argentina, ambayo mara ya mwisho ilifanyika hivyo mwaka 1986, lakini anaweza kuondoka Russia na tuzo yake binafsi kwa maana ya kuwa kinara wa mabao.

Neymar

(Brazil)

Anabeba matumaini makubwa kwa Wabrazili na hasa kuwafuta machungu ya kuteswa wakati fainali hizo zilipofanyika kwenye ardhi ya kwao huko Brazil miaka minne iliyopita. Neymar ni mmoja wa wachezaji wenye vipaji bikubwa sana katika kufunga mabao na hilo ndilo linaloifanya Brazil iwe moja ya timu inayopewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa. Mahitaji ya Neymar pia ya kubeba tuzo ya Ballon d’Or inaweza kuwa chachu katika kumfanya afanye vizuri zaidi hasa kwenye kufunga mabao ili kulifanya jina lake kutokea kwenye orodha ya watakaokwenda kuwania tuzo hiyo bora kabisa kwa mchezaji.

Chanzo: mwananchi.co.tz