Dar es Salaam. Baada ya Mwanariadha Failuna Abdi kuishia njiani katika mbio za marathoni (kilomita 42) katika mashindano ya dunia, Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) limeeleza sababu za mwanariadha huyo kushiriki mashindano hayo bila kocha.
Failuna alichuana Ijumaa iliyopita kwenye mashindano ya dunia yaliyofunguliwa siku hiyo kwenye uwanja wa Khalifa mjini Doha, Qatar.
Katika mbio hizo Mtanzania huyo alishindwa kumaliza na kuishia njiani akiwa amekimbia umbali wa kilomita 21, huku ikielezwa kuwa alikimbia bila kuwa na kocha mkuu wa timu hiyo, Andrew Panga ambaye amebaki nchini.
Katibu Mkuu wa RT, Wilhelim Gidabuday alisema Panga ameachwa nchini kwa kuwa anawasimamia wanariadha wa timu ya wanaume ambao pia watachuana Oktoba 6.
Wanariadha hao ni Alphonce Simbu, Agostino Sulle na Stephano Huche ambao watachuana siku ya kufungwa mashindano hayo katika mbio za marathoni.
"Kocha alibaki Tanzania kuwasimamia kina Simbu kwenye mazoezi yao, hivyo Failuna niliondoka naye mimi na ameshindwa si sababu ya kocha, tatizo ni hali ya hewa ya joto kali huku," alisema Gidabuday.
Pia Soma
- Mabadiliko kikosi cha simba, Aussems aanzisha maproo wawili tu kuivaa Biashara United
- Yanga, UD Songo, KCCA zatangulia Shirikisho Afrika
- Walcott aruhusiwa kutoka hospitali baada ya kuumia uwanjani