Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pyramids wamuibua Magori Simba, ashusha nondo Yanga

81178 Magori+pic Pyramids wamuibua Magori Simba, ashusha nondo Yanga

Tue, 22 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

YANGA kesho itashuka Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza katika dakika 90 za Ligi Kuu Bara, kisha itakuwa kazi moja tu kujiandaa dhidi ya Pyramids ya Misri katika mchezo wa kuwania makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kigogo mzito wa Simba ameichambua timu nzima kisha akawapa akili flani kutafuta matokeo.

Mtendaji mkuu wa zamani wa Simba, Crescentius Magori ndiye aliyefunguka hayo akisema hatua ya Yanga kuhamishia mchezo huo jijini Mwanza inaweza kuwasaidia endapo Waarabu watashindwa kuhimili ubora mdogo wa Uwanja wa Kirumba kulingana na mazoea ya kucheza katika viwanja vizuri.

Magori ameliambia Mwanaspoti katika mahojiano maalumu, endapo ubora wa CCM Kirumba utaisumbua Pyramids hiyo itakuwa faida kubwa kwa Yanga kama timu zote zitakuwa zikicheza sawa huku zikipambana katika ubora wa fiziki na stamina.

“Kwa mbinu Yanga iko sahihi kubadilisha uwanja na kwenda Kirumba sio mzuri kama unacheza na timu nzuri, ngumu na ambayo inacheza mpira mzuri kuliko wewe ukiipeleka katika uwanja ambao sio mzuri inamaana ule uzuri unauondoa mnabakia sasa mapambano ya fiziki na stamina hiyo inaweza kuwa faida kwao.

“Unajua timu mbili zikiwa zinatumia uwanja mbovu huwezi kirahisi kutofautisha ipi timu bora na isiyo bora, huwezi kupiga pasi tatu ukazunguka badala yake itakuwa pasi mbili inapigwa ndefu, hivyo yule bora atakosa ile ladha yake anayoijua.

“Kwa upande mwingine pia naona Yanga Kirumba itakuwa kama wageni kwa kuwa sio uwanja inaoutumia mara kwa mara kama ilivyokuwa Taifa, hivyo ikienda kucheza pale unajua ule ugeni ni kama wewe ukiingia nyumbani kwako unakuwa na akili ya kutawala.

Pia Soma

Advertisement
“Yanga ikiwa Taifa wachezaji wanajua kasi ya mpira kwa kuwa wanaujua uwanja lakini pale Kirumba haitakuwa hivyo, kwa hiyo hata uenyeji utakuwa kwa wingi tu wa mashabiki.”

Bosi huyo mwenye nguvu ndani ya Simba alisema jambo kubwa kuliko yote kwa Yanga kuelekea katika mchezo huo ni kuhakikisha inabadilisha mtazamo wake wa kwamba ikikosa matokeo nyumbani itashinda ugenini.

Alisema Yanga inatakiwa kuhakikisha inapata matokeo nyumbani kwani katika soka la Afrika ni vigumu kupata matokeo mazuri ugenini.

“Yanga ina tatizo la hisia, niliwahi kusema huwezi kusema unakwenda kushinda ugenini, kwamba sisi Yanga kawaida yetu tunakwenda kushinda ugenini hakuna mpira wa namna hiyo, unashinda kwa ubora bila mashaka ukiwa nyumbani, ukishindwa kushinda nyumbani huko unakokwenda muombe Mungu tu, kwani nafasi hiyo kwa vyovyote utaipoteza tu tena kwa mpira wa Afrika ndiyo mbaya kabisa.

“Yanga kushindwa kutumia uwanja wa nyumbani hilo ni tatizo kubwa sana, hata sijui kwa nini na huwezi kusema tatizo ni Simba kwani hata wao huwa wanazomea mechi zetu,” alisema Magori.

ACHAMBUA

JESHI LA ZAHERA

Akizungumzia ubora na mabadiliko ya kikosi cha Yanga, Magori alisema bado Yanga sio timu ya kubezwa kwani ina kikosi kizuri lakini changamoto iliyopo wapo mastaa wake wapya wamechelewa kuendana na mifumo ya kikosi hicho.

“Kuhusu kikosi chao, ninachokiona Yanga ina wachezaji wengi sana wapya ambao wamewasajili na kilichotokea wengi wameshindwa kuingia kile kikosi cha kwanza na kufanikiwa, huwezi kusema ni wachezaji wabaya kwasabu muda pia haukuwepo.

“Yanga mpaka inacheza mechi ya kwanza na Township Rollers sidhani kama ilikuwa imecheza mechi yoyote ya ushindani labda ile ya Kariobang Sharks ambayo ilikuwa siku ile ya Wiki ya Mwananchi,” alisema na kuongeza:

“Hivyo ratiba yenyewe iliwanyima nafasi ya kuwa sawa halafu ikawa tena na wachezaji wapya ambao pia walishindwa kuingia katika kikosi cha kwanza kwa utayari.

“Tatizo hilo ndilo linaloitesa Yanga wala haina kikosi kibovu kama wengi wanavyoikejeli.”

Magori atakuwa na muendelezo wake mrefu wa uwepo wake ndani ya Simba katika makala maalumu zitakazokuwa zinaeleza mambo mbalimbali ndani ya klabu hiyo zitakazoanza kesho Jumanne katika gazeti hili la Mwanaspoti. USIKOSE...!

Chanzo: mwananchi.co.tz