Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pumzi, stamina tatizo Simba, Yanga

13796 Pic+pumzi TanzaniaWeb

Sat, 25 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya usajili na maandalizi ya gharama yaliyofanywa kabla ya msimu wa Ligi Kuu 2018/2019 kuanza, Simba na Yanga zina kazi kubwa ya kumaliza tatizo la kukosa pumzi na stamina kwa wachezaji wake kama zina nia ya kufanya vizuri msimu huu.

Vigogo hivyo vya soka nchini licha ya kuibuka na ushindi kwenye mechi zao za ufunguzi wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons zimeonyesha kutokuwa na uimara wa kucheza kwa kiwango bora kwenye dakika zote 90 za mchezo.

Katika mchezo ambao Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Jumatano na ule ambao Yanga ilijipatia ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Mtibwa, timu hizo kongwe zilijikuta kwenye wakati mgumu katika dakika 45 za pili.

Prisons na Mtibwa ambazo zilianza mechi hizo kwa kujilinda na kucheza kwa kasi ndogo, zilijikuta zikitanguliwa kufungwa mabao kwenye kipindi cha kwanza, lakini zote zilionyesha mabadiliko makubwa katika dakika 45 za kipindi cha pili na kuzilazimisha Simba na Yanga kupaki basi.

Kundi kubwa la wachezaji wa Simba lilionyesha kuchoka na kupoteza mipira kirahisi kipindi cha pili hivyo kuwapa mwanya wachezaji wa Prisons kutawala mchezo ikiongeza kasi iliyoonekana kuwa tatizo kwa Simba kila dakika zilivyokatika.

Kilichowakuta Simba ndicho kiliwatokea watani zao wa jadi, Yanga ambao nao katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, ambao walianza kwa kasi wakishambulia mfululizo lango la wapinzani wao kiasi cha kufunga mabao mawili na kwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao hadi umaliki wa mpira.

Hata hivyo ni wazi kuwa Yanga, pumzi ilikata katika dakika hizo 45 kwani kipindi cha pili hawakufurukuta na kuwaachia Mtibwa kutawala na kama sio kutokuwa makini kwa wachezaji wao bila shaka wangesawazisha nap engine kuondoka na ushindi.

Ni katika kipindi hicho cha pili ambapo Mtibwa walifunga bao la kufutia machozi baada ya kupoteza nafasi kadhaa za wazi kwa washambuliaji wake kukosa umakini.

Azam FC kwa upande wake, ni kati ya timu inayopewa nafasi kubwa kuchuana na miamba kuwania ubingwa wa msimu huu.

Azam iliifunga Mbeya City walioonekana kulala kipindi cha kwanza walichachamaa kipindi cha pili na kuwapa hofu wachezaji na mashabiki wa Azam.

Mbali na udhaifu huo wa kukata pumzi mapema na kutokuwa na muendelezo wa ubora kwa dakika 90 kamili za mchezo, safu zao za ushambuliaji zimeonyesha uimara na ufanisi wa hali ya juu katika kufumania nyavu kulingana na nafasi walizozitengeneza mwanzoni na ndilo jambo linaloweza kuzibeba msimu huu.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema ameridhishwa na matokeo ya mchezo wa kwanza pamoja na kiwango walichoonyesha ingawa wanapaswa kuimarika zaidi.

“Watu wanatakiwa kufahamu kwamba tupo kwenye mchakato wa kuwa na timu imara itakayofanya vizuri siku za usoni, hivyo waendelee kutupa sapoti,” alisema Aussems.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila alisema: “Tulicheza vizuri na kama mlivyoona tulifanikiwa kutengeneza nafasi ambazo hatukuzitumia vizuri, .

Naye Kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila alisema timu yake imepata matokeo iliyostahili kulingana na ubora walioonyesha katika mchezo huo.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa vigogo hivyo vitatu, Uwanja wa Mkwakani Tanga, mashabiki waliuza uwanja huo, ingawa imeelezwa kuwa wengi wao walimiminika sio kwa nia ya kuiona timu ya nyumbani, Coastal Union, bali walitaka kumshuhudia mshambuliaji mpya wa timu hiyo msanii wa bongo fleva, Ali Kiba ambaye yuko Canada kwa sasa.

Aidha ushindi wa ugenini ambao timu ngeni katika Ligi hiyo Biashara United kutoka Mara iliupata dhidi ya Singida United na ule wa Ndanda FC dhidi ya Ruvu Shooting yanabakia kuwa matokeo ya kushangaza zaidi katika mechi za ufunguzi wa Ligi Kuu 2018/2019.

Nayo Ndanda FC ‘Wana Kucheere’ iliiduwaza Ruvu Shooting ugenini baada ya kuifunga bao 1-0, Uwanja wa Mabatini Mlandizi.

Baada ya mechi hizo za mzunguko wa kwanza, matokeo yamedhihirisha kuwa timu zitarajie ushindani wa hali ya juu na kwamba dharau au uzembe kidogo unaweza kufanya yapatikane matokeo ambayo yasiyotarajiwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz