Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons, Biashara zaacha deni Uwanja wa Sokoine

51681 DENI+PIC

Thu, 11 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Kitendo cha mchezo kati ya Prisons na Biashara United kuingiza mapato ya Sh9,000 kimemuachia madeni meneja wa Uwanja wa Sokoine, Mbeya Modestus Mwaluka.

Prisons na Biashara United zilivaana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Jumamosi iliyopita na kuingiza kiasi hicho cha fedha, baada ya mashabiki watatu tu kukata tiketi kwa kiingilio cha Sh3,000.

Akizungumza jana, Mwaluka alisema baada ya mgawanyo wa mapato aliambulia Sh1,000 fedha ambazo zimemuweka katika mazingira magumu ya kulipa deni analodaiwa.

Mwaluka alisema alikopa vifaa vyenye thamani ya Sh150,000 za kuboresha uwanja na chokaa mifuko 10 ambapo kila mmoja Sh60,000 kwa ajili ya kuweka mistari ya uwanja. Meneja huyo alisema hadi sasa ameshindwa kulipa deni hilo baada ya kuambulia Sh1,000 za mapato yote.

“Inaniuma gharama zote nilizotumia kuandaa uwanja lakini nikaambulia Sh1,000. Ni kweli Prisons haina mashabiki wengi kama Mbeya City, lakini TFF ilipaswa kujipanga kwani siku ile kulikuwa na mechi ya Simba na TP Mazembe iliyochangia kukosa mashabiki,” alisema Mwaluka.

Alisema katika mechi zote zilizochezwa misimu miwili mfululizo mapato ya chini kuingiza kwenye uwanja huo yalikuwa si chini ya Sh150,000.

Naye Katibu Msaidizi wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya (MREFA), Lucas Kubaja alisema licha ya mechi hiyo kuingiza Sh9,000 haoni ajabu kutokana na rekodi ya uwanja huo.

“Fuatilia mapato ya mechi zote za klabu za mikoani utaniambia mapato yake, basi tu kwa vile haziwekwi hadharani kama ilivyo hii ya kwetu,” alisema Kubaja.

Katibu Mkuu wa Prisons, Ajabu Kifukwe alisema mapato kidogo wanayopata yamekuwa yakiathiri maendeleo ya klabu hiyo.

“Kama timu mwenyeji atakuwa hana vyanzo vingine vya mapato ni tatizo, tuchukulie kama hii ni changamoto kwa klabu zitafute vyanzo vingine vya fedha,” alisema Kifukwe.



Chanzo: mwananchi.co.tz