Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pluijm, Kim wapo tayari kumrithi Zahera Yanga

82072 Pic+pluijim Pluijm, Kim wapo tayari kumrithi Zahera Yanga

Tue, 29 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Makocha Hans der Pluijm na Kim Poulsen wamesema hawana tatizo na kuchukua mikoba ya Mwinyi Zahera iwapo viongozi wa Yanga watawafuata.

Makocha hao Pluijm na Kim kwa nyakati tofauti wamezungumzia kuhusishwa kwao na kutaka kujiunga na Yanga kuchukua nafasi ya Zahera ambaye yupo katika wakati mgumu.

Kim aliyewahi kuifundisha timu ya Taifa Tanzania akizungumzia suala hilo alisema lolote linaweza kutokea.

"Kwa muda huu sina mpango wa kurejea Tanzania, lakini kuhusu suala la Yanga sote hatujui nini kitatokea mbele," alisema Kim.

Kim aliongeza kwa kusema yupo tayari kuja iwapo viongozi wa Yanga wakimtafuta.

Kocha Pluijm alisema anaweza kurejea kukinoa kikosi hicho endapo viongozi wa klabu hiyo, wataona kuna umuhimu wa kumrudisha kwa mara nyingine tena Tanzania.

Pia Soma

Advertisement
Pluijm alisema amekuwa akipokea jumbe mbalimbali kutoka kwa mashabiki wa Yanga hasa kipindi hiki wakimtaka arejee nchini kwa lengo la kuirejesha Yanga katika kasi yake ya ushindani.

Kocha huyo, alisema yupo tayari kurejea muda wowote, "Nimesikia kwa sasa timu haina mwenendo mzuri. Katika mpira kuna nyakati ambazo lazima timu ipitie, inahitaji nguvu ya ziada kupita salama hasa kipindi ambacho matokeo huwa tofauti na matarajio.

"Naipenda Tanzania hilo siwezi kuficha na ninaweza kurudi tena kwa sababu sikuondoka kwa matatizo, nilijitahidi kwa uwezo wangu wote kuipa mataji Yanga, tulifurahi na kucheka pamoja, lakini ulifika muda wa kumpisha mwingine, aendelee pale nilipoishia."

Pluijm alisema kuwa ni mambo ya kawaida kwa kocha kutoka na kurudi, mabadiliko ya uongozi anaamini pengine Yanga inaweza kuendana na soka la kisasa ambalo linahitaji mtiririko mzuri kuanzia ngazi ya chini.

Bado Mholanzi huyo, anaamini katika soka safi la kushambulia kwa pasi fupi fupi huku akitumia zaidi viungo wabunifu licha ya kuwapo kwa staili tofauti za kushambulia ambazo zimekuwa zikiibuka kila kukicha.

"Kuna kipindi timu ilisimama na tukawa na uelekeo mzuri ila changamoto ilikuwa katika subra ni ngumu kutawala soka la Afrika kama ilivyokuwa ikitakiwa kwa kipindi kifupi. Tunaweza kushikamana na kutengeneza upya," alisema kocha huyo.

MAFANIKIO YAKE YANGA

Pluijm aliisaidia Yanga kutwaa mataji ya Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili mfululizo katika msimu ya 2014/15 na 2015/16 na kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.

Chanzo: mwananchi.co.tz