Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Piga ua Kasumba anakuja

31149 Pic+kasumba TanzaniaWeb

Wed, 12 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

HUKO Jangwani unaambiwa kwa sasa ni shangwe tupu. Kwanza timu yao imezidi kutembeza vichapo kwa wapinzani wao Ligi Kuu, pia vigogo wa klabu hiyo wameonyesha wamepania kwelikweli katika ishu nzima ya usajili.

Yanga juzi ilipindua meza kwa Biashara United kwa kutoka nyuma na kufunga mabao mawili ndani ya dakika 20 na kuendeleza ubabe wao ikiwa moja ya timu mbili ambazo hazijapoteza mechi ikiwamo Azam FC ambayo jana ilibanwa na KMC na kutoka sare ya 2-2.

Lakini baada ya mechi hiyo ya juzi usiku, unaambiwa vigogo wa klabu hiyo ya Jangwani waliitana katika kikao kizito faragha kisha kupitisha bajeti ya kusajili vifaa vitatu vya maana akiwemo Umar Kasumba, huku mmoja wao akijibebesha zigo kumshusha straika huyo iwe isiwe.

Hata hivyo, wakati vigogo hao wakipeana jukumu ili kuwahi siku chache za kufungwa dirisha la usajili, Kocha mmoja Mkenya, ametahadharisha timu pinzani za Yanga Ligi Kuu zikiwamo Simba na Azam kuwa, kama Kasambu ataungana na Heritier Makambo basi Yanga itaua mtu.

Ebu tuanze na kikao cha usiku wa manane. Mabosi hao wa Yanga waliamua kuitana usiku usiku katika kikao cha wima wakijadiliana juu ya uhamisho wa Kasumba na fasta mmoja wa vigogo hao (jina tunalo) akaamua kubebesha zigo zito kwa kuchukua jukumu zima la kumshusha raia huyo wa Uganda.

Uamuzi wa tajiri huyo kubeba jukumu hilo ni kugawana majukumu, huku akiwaachia wenzake kupambana na vifaa vingine vinavyotakiwa kusajiliwa, akiwamo kipa wa timu ya taifa ya Kenya, Farouk Shikalo.

Yanga imepanga kabla ya dirisha kufungwa wakimbilie Kenya ili kumalizana na Kasumba aliyewahi kukipiga Polisi Uganda na SC Villa. Inaelezwa kuwa, straika huyo ameshakaa tayari kuja nchini, ila anasubiri tu mabosi wa Yanga ili aende Nairobi kumalizia kazi ya kumng’oa Sofapaka inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

“Kilichotukwamisha kumfuata kwa kumalizia maamuzi yetu ni wenzetu kuwa na kikao na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dk. Harrison Mwakyembe leo (jana) asubuhi.

“Nafikiri kila kitu kipo sawa tutamalizana naye kwa sababu kwa sasa suala lililosalia ni mtu kumfuata tu maana bajeti yake imeshamalizwa.”

Mmoja wa vigogo hao aliidokeza Mwanaspoti, kigogo mwenzao amekubali kutoa si chini ya Dola 15,000 ambazo ni zaidi ya Sh34.5milioni ili kuhakikisha Kasumba anatua Jangwani ili kuongeza shangwe zinazoendelea kwa sasa nchini.

Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi ikiwa na alama 41 baada ya kucheza mechi 15 bila kupoteza, ikiwa juu ya Azam iliyocheza mechi 16 na kukusanya alama 40, jambo linalowapa furaha mashabiki wake, huku Makambo akiwa ameshatupia nyavuni mabao nane mpaka sasa..

“Jamaa kakubali kulipia kila kitu na dau la mchezaji huyo si chini ya Dola 15,000, hivyo kilichobaki kwetu wengine ni kuona tunashusha majembe mengine mawili ya mwisho katika makubaliano ya bajeti yetu akiwamo kipa,” kilisema chanzo kilichokataa kuandikwa jina gazetini.

MKENYA AONYA

Katika hatua nyingine, Kocha wa zamani wa Yanga, Mkenya Razack Siwa mara aliposikia taarifa za mabosi wa Jangwani kumtaka Kasumba akatoa tahadhari mapema kwa timu pinzani za Ligi Kuu kwa kudai kama Yanga ikimpata Kasumba kisha akacheza sambamba na Makambo basi Yanga itakuwa na safu bora zaidi ya ushambuliaji. Siwa ambaye aliwahi kufanya kazi Yanga kama kocha wa makipa na Kaimu Kocha Mkuu, alisema Yanga ikimnasa Kasumba italamba dume kutokana na ubora wake ukiongeza na ufundi wa Makambo safu yao itakuwa hatari.

Alisema kwa jinsi Yanga inavyocheza sasa ikiwa na Makambo kisha akapata msaidizi kama Kasumba kisha wakacheza sambamba mabeki wa timu pinzani watakuwa katika wakati mgumu kuweza kuwazuia wawili hao kufunga.

“Nimesikia hapa kuwa Kasumba anataka kuja huko Tanzania na Yanga naangalia sana mechi zao kama wakimpata na akacheza sambamba na yule Makambo watakuwa wameongeza kitu kikubwa katika safu yao ya ushambuliaji,” alisema Siwa.

“Yule Kasumba sio mtu mwepesi kuzuilika anapambana sana sasa ukiongeza na yule Makambo anavyojua kutumia akili Yanga watakuwa wameiboresha timu yao kule mbele, hapo sijamtaja Ibrahim Ajibu wala nini, wapinzani wa Yanga wajipange,” alisema kocha huyo wa zamani.



Chanzo: mwananchi.co.tz