UPO uwezekano mkubwa wa panga lingine likapita kwa viongozi wa Yanga mara baada ya mchakato wa mabadiliko ya klabu kukamilika hivi karibuni.
Hiyo ikiwa ni siku chache zimepita tangu uongozi wa Yanga utangaze kuachana na aliyekuwa mhamasishaji wa klabu hiyo, Antonio Nugaz.
Klabu hiyo hivi karibuni ilipitisha katiba mpya katika mkutano wake uliofanyika kwenye Ukumbi wa DYCCC, uliopo Chang’ombe, Temeke jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Frederick Mwakalebela, alisema kuwa mara baada ya mchakato wa mabadiliko kukamilika, zipo baadhi ya nafasi zitaondolewa.
“Achana na Nugaz zipo baadhi ya nafasi zitakazoondolewa na kuongezwa haraka mara baada ya mfumo wa mabadiliko kukamilika.
“Nugaz ameondolewa baada ya mkataba wake ambao ulikuwa wa miaka miwili kumalizika lakini pia kwa sasa tupo kwenye mchakato wa mabadiliko ya klabu.
“Hiyo inatokana na rasimu ya mabadiliko ya katiba ambayo ilipitishwa na wanachama kwenye mkutano mkuu wa klabu ambao ulifanyika hivi karibuni kuonyesha kila kitu ambacho kinapaswa kuwepo kwenye klabu,” alisema Mwakalebela na kuongeza:
“Kuhusu nafasi ya Manara (Haji) ndani ya klabu itajulikana hivi karibuni kwani mwenye dhamana ya kumpangia nafasi yake hivi sasa ni bosi wake mpya ambaye ni Mtendaji Mkuu wa klabu (CEO), Senzo (Mazingisa).”