Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pablo kufyeka watatu Simba

Pablo Frano Arrows Pablo kufyeka watatu Simba

Fri, 17 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Simba itakuwa wageni wa Kagera Sugar keshokutwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Pablo akitaka kuendeleza rekodi tamu tangu ajiunge na timu hiyo mwezi uliopita kuchukua nafasi ya Didier Gomes aliyetimuliwa baada ya Simba kung’olewa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati kikosi kikiwa na mzuka baada ya juzi kuing’oa JKT Tanzania katika Kombe la Shirikisho (ASFC) kwa bao 1-0, Pablo amewasilisha ripoti kwa mabosi akiainisha wachezaji wanaotakiwa kutemwa na kuletwa majembe mapya matatu.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema aliwasilisha ripoti hiyo akiweka bayana alichokiona tangu alipotua, huku akitaja majina ya kufyekwa na vitu vinavyotakiwa kuboreshwa ikiwamo wachezaji wapya watatu ambao ni wakali kuliko waliopo kwa ajili ya michuano ya ndani na ya kimataifa.

Inaelezwa kuwa, huenda Simba ikaachana na wachezaji watatu wa kigeni wanaoweza kutolewa kwa mkopo ili nafasi zijazwe na majembe watatu wanaotakiwa, huku wanaotajwa kukalia kuti kavu ni pamoja na beki wa kati Pascal Wawa, Duncan Nyoni na Pape Ousmane Sakho.

Simba imetinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuing’oa Red Arrows ya Zambia na Kocha Pablo anataka kuhakikisha inafika mbali zaidi kuliko msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilipoishia ya robo fainali.

Advertisement Taarifa zaidi zinasema Pablo katika usajili wa dirisha dogo lililofunguliwa jana ametaka kiungo mshambuliaji (namba 8) mwenye uwezo zaidi wa Sadio Kanoute anayecheza nafasi hiyo mara kwa mara.

Pia amependekeza washambuliaji wa kati watakaocheza pacha yaani namba 9 na 10 wenye uwezo mkubwa wa kutupia nyavuni kuliko Meddie Kagere, John Bocco na Chriss Mugalu.

Kwa mujibu wa chanzo ndani ya klabu hiyo, Pablo katika kuhakikisha analitumia vyema dirisha hili la usajili, amewaelekeza mabosi wake kuwa hakuna mchezaji mpya atakayesajiliwa bila kutoa maoni yake.

Inaelezwa mabosi wa Simba wameanza kushughulikia ripoti hiyo na taarifa zilizonaswa na Mwanaspoti nyota wawili toka Zambia wameanza kufuatiliwa.

Pablo aliwaelekeza mabosi wake anahitaji wachezaji wapya ambao watakuwa na ruhusa ya kucheza mashindano ya ndani na Kombe la Shirikisho Afrika ili kufanya vizuri na kufikia malengo ya timu kucheza nusu fainali ya michuano hiyo.

ISHU YA CHAMA

Wakati hayo yakiendelea hivyo, kiungo fundi wa mpira wa RS Berkane ya Morocco, Clatous Chama aliyeichezea kwa mafanikio Simba kabla ya kuuzwa mwishoni mwa msimu uliopita, inaelezwa ameshamalizana kila kitu na timu yake hiyo ya zamani, ila wanasubiri kupata baraka kwa timu yake.

Chama amekuwa hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, huku ikielezwa mazingira ya Morocco yamemfanya Mzambia huyo kutaka kutimka Berkane iliyomsainisha mkataba wa miaka miwili na nusu.

Chama alipotafutwa na kuulizwa juu ya taarifa za kutaka kurejea Msimbazi, licha ya kutokuwa na nafasi ya kuitumikia Simba katika mechi za Kombe la Shirikisho Afrika, kiungo huyo alisema kwa ufupi: “Kuhusu suala la kurudi Simba wakati ukifika muda utaongea.”

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gozalez alisema ishu za usajili zinasubiri ripoti ya kocha wao ili kujua mahitaji yake.

“Lazima tufanye maamuzi magumu katika dirisha dogo la usajili ili kupata wachezaji bora kama ambavyo kocha wetu atahitaji kwa ajili ya kuifikisha timu kwenye malengo yake ya kufanya vizuri na kuchukua makombe mashindano ya ndani na nje ya nchi,” alisema Barbara.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz