Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyota Tanzania asimulia ishu ya kunyongwa

50418 YUSUPH+PIC

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

ALITAMBA kwenye ufungaji enzi zake. Na ukizungumzia wachezaji ambao wana macho ya kuliona goli, hutaacha kumtaja Yusuf Soka Abbas.

Hata hivyo, nyota yake ilizima ghafla na akaacha maswali mengi kwa wadau waliomfahamu hasa wakati anakipiga pale African Lyon katika kikosi kimoja na staa wa Genk, Mbwana Samatta.

Hiyo ilikuwa mwaka 2010, na kwa sababu soka alikuwa analijua, akiwa kijana mdogo alipata ‘dili’ la kwenda nchini Sweden kwa ajili ya kujiunga na Klabu ya Ligi Daraja la Nne ya AFC Eskilstuna.

Ilikuwa ni klabu ambayo alitakiwa akae wamlee na kumuuza kwenye timu kubwa, lakini mambo hayakwenda sawa.

Gazeti la Mwanaspoti linakuletea yote yaliyomsibu Mtanzania huyo hadi kuzua taarifa tofauti kwamba alifungwa jela miaka 30 huko ughaibuni na nyingine kwamba alinyongwa nchini Sweden.

KAULI YAKE YA KWANZA

“Kwanza nataka Watanzania watambue kuwa malengo yangu ni yale yale yaliyonileta Ulaya. Nataka kucheza mpira wa mafanikio. Nawaahidi watakuja kushuhudia mafanikio makubwa katika maisha yangu ya soka kwa sababu nimedhamiria na nataka kutimiza ndoto zangu huku,” anasema Soka.

Anasema, kutokana na hamasa kubwa aliyonayo, hawezi kurudi Tanzania kama hajafikia malengo yake kwa sababu kitu alichokifuata Sweden bado hajakipata.

“Nitakapopata kitu kilichonitoa nyumbani Tanzania kuja huku ndipo nitarudi. Na kitu hicho ni kucheza mpira wa mafanikio Ulaya. Nicheze Ligi ya Mabingwa Ulaya hata kuchukua ubingwa wa mashindano hayo,” anaeleza Soka.

“Ninaamini kwa sababu hakuna kinachoshindikana nitafanikiwa tu. Ulaya ni Ulaya tu na mpira ni ule ule. Leo nipo nacheza Ligi Daraja la Pili kesho nitakuwa timu kubwa. Naamini hilo kutokana na juhudi ninazofanya kuelekea malengo yangu.”

Anasema anajua wapo wengi watakaoona kwamba kauli zake ni za kujifariji tu na hatafanikiwa, lakini kwa sababu anajua anachokifanya, hayo mengine hayamsumbui: “(Ninayopitia) Ni mambo ya muda tu, tusubiri tuone.”

SABABU YA UKIMYA

“Baada ya matukio mengi kutokea niliamua kukaa kimya, sikutaka kuishi maisha ya kujionyesha kwa sababu sicho kilichonileta Sweden,” anasema Soka.

“Nilitaka pale nitakapofanikiwa ndipo nizungumze kwa sababu nitakuwa na cha kuzungumza. Maana kwa sasa hata ningetaka kuzungumza sina cha kusema, zaidi ningekuwa nadanganya tu, ndiyo maana nikahitaji muda wa kutulia na kukomalia malengo tu kwanza.”

Hata hivyo, anasema watu wake wa karibu walikuwa wanajua kila kitu kinachoendelea kwa sababu alikuwa na mawasiliano nao.

‘SAPRAIZI’ KWA WATANZANIA

Anasema, kitu ambacho alitaka ni kukaa kimya hadi siku moja ‘awasapraiz’ Watanzania kwa kufanya jambo kubwa, iwe ni kujiunga na klabu kubwa ama jambo jingine la kutajika katika mchezo huo.

“Nilitaka kuwaonyesha watu kwa vitendo na si maneno ambayo kila mtu anaweza kuzungumza, hata wewe (mwandishi) umeniwahi baada ya kunisumbua sana,” anasema Soka.

MIAKA 30 JELA, KUNYONGWA

Anasema kimya chake nchini Sweden kilizua mengi nyumbani Tanzania. Kila mtu alizusha lake.

Mwaka 2016 alirejea nyumbani kusalimia, miaka sita tangu alipoondoka mara ya kwanza. Ndugu na familia yake walifurahi na hawakuamini.

“Licha ya kuwa tulikuwa tunawasiliana kwenye simu lakini walikuwa hawajawahi kuniona baada ya kipindi kirefu kupita. Hapo ndipo nikapata taarifa nyingine zaidi ambazo watu walikuwa wakinizungumzia Tanzania,” anasema Soka.

“Nilisikia taarifa zote kuwa nimefungwa jela miaka 30, wengine walivumisha kuwa nilikamatwa na vitu visivyo halali nikanyongwa, mambo ambayo si kweli kabisa, na sijui yalitoka wapi. Kama ningekutwa na matukio hayo, hivi sasa tungekuwa tunazungumza?” Anahoji Soka.

“Imeniuma sana. Unajua licha ya kuwa si wote wanaoniheshimu lakini binafsi mimi nina watu wananiheshimu na kunitegemea, kiujumla hawakuwa na amani.”

Anasema, “Kwa wale ndugu na jamaa wa karibu walikuwa wanajua kwa sababu tulikuwa tunawasiliana kwa simu, lakini wale wa mbali iliwaumiza kwa sababu walikuwa hawajui kinachoendelea katika maisha yangu hivyo nikawa na kazi ya kufanya ziara ya kuwatafuta marafiki, ndugu na jamaa wengi kwa kadri niwezavyo: “Nilikwenda mikoani na sehemu tofauti, waliponiona wakaridhika.”

TAIFA STARS WAMSHANGAZA

Soka anasema, amekuwa akifuatilia soka la Tanzania na anajua Taifa Stars imeandika historia baada ya miaka 39. Itacheza fainali za Afrika (AFCON) zitakazofanyika Juni mwaka huu nchini Misri.

“Nawapongeza sana kwa kiwango walichokionyesha. Nilitamani sana kuangalia mechi lakini sikufanikiwa. Nilitafuta kila sehemu ambayo ningeweza kuangalia mechi ile lakini sikufanikiwa, nilichobahatika ni kuangalia vipande vidogodogo tu vya video za mechi kwenye simu,” anasema Soka.

“Nimewaona wamejituma kwani si kazi ndogo kufanikiwa kuingia kwenye mashindano makubwa kama hayo, lakini wanatakiwa wapambane zaidi ili mambo yaende sawa.”

AOMBA WANASAIKOLOJIA STARS

“Kuna mambo madogomadogo ambayo yamekuwa yakiwagharimu watu bila kutegemea hivyo watu wa saikolojia ni muhimu kwa wachezaji wa Taifa Stars ili waweze kujiamini zaidi,” anasema Soka.

Anasema, watu ambao wamesomea saikolojia wanahitajika kwenye kikosi hicho kwa sababu itawaongezea wachezaji hali ya kujiamini na kufanya mambo makubwa zaidi kwa sababu wana hamasa.

“Katika timu pamoja na mafanikio, kwa sababu ni mara ya kwanza, wapo wachezaji wanakuwa na woga, wengine viwango vinakuwa vimeshuka na wengine majeruhi sasa katika kuwasaidia ni watu hao wa saikolojia. Mtaalamu huyo awe anakaa na mchezji mmoja mmoja na kuzungumza naye,” anasema Soka.

AITAMANI TAIFA STARS

Soka anasema, kwa kiwango alicho nacho sasa, kama ataitwa Taifa Stars anaamini atatoa mchango mkubwa.

“Waniite tu na mimi niweze kutoa mchango wangu kwa timu. Nitajaribu kwa nafasi yangu kuonyesha kitu nilichonacho. Soka yule wa Afrika Lyon si huyu wa sasa. Kiwango kimekua. Kama unavyojua Ulaya ni Ulaya, viwango vya wachezaji wa huku si vya kupuuzwa,” anasema Soka.

Anasema, mchango wake unaweza kuwa uwanjani au hata nje ya uwanja kwa ushauri katika kulisaidia taifa lake.

HAJAUMISI UGALI

Anasema, baada ya kuishi muda mrefu na familia ya Kisweden alijifunza namna ya kupika na kuandaa chakula cha huko.

“Kwa kipindi kirefu nilichokaa hapa na walezi wangu, nilijifunza mengi hasa chakula ambacho kwa sasa nimekizoea na nina uwezo wa kukiandaa,” anasema Soka.

Alipoulizwa kama ameumisi ugali ambao ni chakula kinachotumiwa na Watanzania wengi, anasema: “Kusema kweli hata sijaumisi ugali kwa sababu hata hapa nikitaka kuuandaa ni kiasi cha kununua unga na kupika kwa sababu vitu kama hivyo vinapatikana madukani.”

“Nakula chakula cha huku huku. Si unajua chakula cha wenzetu baga, mbogamboga na nini, halafu hata Watanzania hivi yupo ambaye anakuwa anaumisi ugali, sijui,” anauliza Soka kwa mshangao.

BURUDANI YA MUZIKI ANAYOPENDA

“Huwa sipendi sana muziki lakini kidogo napenda wa utamaduni, kuna yule wa Hip Hop wa Bongo anaitwa One The Incredible huwa napenda kumsikiliza. Nampenda kwa sababu mashairi ya nyimbo zake huwa yana ujumbe,” anasema Soka.

Anasema, huwa hafuatilii nyimbo za wasanii ambao hawaimbi ujumbe kwa sababu ndiyo kitu anachopenda.

Hii ni sehemu ya kwanza ya masimulizi ya kusisimua ya mwanasoka Mtanzania Yusuf Soka anayeishi na kucheza soka huko Sweden. Usikose sehemu ya pili ambayo anazungumzia alivyokataa bunda la minoti ya Simba kwenye gari la matajiri wa timu hiyo ya Msimbazi na maisha yake ya mtaani Sweden baada ya kutemwa na wenyeji wake. Unajua alilolizua hadi akatemwa? Aliishije ughaibuni na viza imeisha?



Chanzo: mwananchi.co.tz