Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyoni atibua hesabu za Simba kimataifa

35346 Pic+nyoni Nyoni atibua hesabu za Simba kimataifa

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Zanzibar/Dar. Simba ina kila sababu ya kuteswa na majeraha ya goti ya beki kisiki na mchezaji wake kiraka, Erasto Nyoni aliyeumia katika mechi ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya KMKM, juzi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Majeraha ya goti aliyopata Nyoni baada ya kugongana na beki wa KMKM, Hafidh Mohammed, yatamuweka nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki tatu hatua itakayomfanya akose mechi kadhaa za Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

Miongoni mwa mechi ambazo Nyoni atakosa ni zile za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria, Januari 12 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Januari 19 mjini Kinshasa.

Kukosekana kwa Nyoni katika mechi mbili kunaiweka Simba kwenye kiza kinene kutokana na sababu kadhaa za msingi ambazo ni vigumu kuziepuka kutokana na uhalisia wa namna beki huyo alivyo na mchango mkubwa katika safu ya ulinzi.

Sababu ya kwanza ni uzoefu wa Nyoni ambao umekuwa ukimpa fursa ya kucheza mechi kubwa za ushandani kama hizo bila presha kubwa kulinganisha na kundi kubwa la mabeki ambao miongoni mwao mmoja huenda akaziba pengo hilo.

Ukiondoa Mganda Juuko Murshid ambaye anaonekana ni beki wa kati mwenye uzoefu anayeweza kupewa mikoba ya Nyoni, waliobaki Yusuph Mlipili na Paul Bukaba wanaangushwa na kigezo cha uzoefu katika mechi za mashindano makubwa.

Nyoni amecheza idadi kubwa ya mechi za kimataifa akiwa na kikosi cha Taifa Stars na kile cha Azam FC aliyoitumikia kwa ustadi kabla ya kujiunga na Simba.

Nyoni amejenga safu yenye uelewano mzuri akicheza pacha na Paschal Wawa ambaye aliwahi kucheza naye Azam, hivyo kukosekana kwake kunaweza kuiteteresha Simba kwa kuwa mabeki wengine wa kati hawana uzoefu wa kucheza na raia huyo wa Ivory Coast.

Pamoja na uzoefu wake ambao amepata kwa kucheza mechi ngumu akiwa na jezi ya timu ya Taifa ya Uganda, Juuko huenda akapata wakati mgumu akipangwa na Wawa kwasababu wawili hao wana aina ya ukabaji inayofanana na hakuna anayeweza kuziba makosa ya mwenzake kama anavyofanya Nyoni.

Sababu nyingine ni udhaifu wa ufanisi unaoweza kutokea endapo benchi la ufundi la Simba litaamua kufanya mabadiliko kadhaa ya kiufundi kwa ajili ya kuziba pengo la Nyoni kwa kumpanga Juuko au kumrudisha nyuma kiungo James Kotei.

Nyoni ni mchezaji mwenye nidhamu uwanjani, hivyo kukosekana kwake kunaweza kuwapa wakati mgumu Wawa na Juuko ambao ni mabeki wanaocheza kwa kukamia.

“Naendelea vizuri, mashabiki wasiwe na hofu nitakuwa fiti muda siyo mrefu, kuna wachezaji wenzangu wenye uwezo wa kucheza kwa ufanisi naamini watafanya vizuri mechi ijayo,” alisema Nyoni.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems amekiri kumkosa Nyoni ni pigo kubwa, lakini anamuandaa Juuko kuziba pengo la mchezaji huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani.

“Hili ni pigo kubwa kwetu, Nyoni ni mchezaji hodari anayetegemewa katika kikosi na hata mechi ijayo alikuwa katika mipango yangu. Juuko ni mchezaji mzuri ila anapaswa kupambana kuitetea timu yake, kesho (leo Jumanne),” alisema Aussems

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema klabu itahakikisha beki huyo anapata matibabu stahiki ili apone haraka na kurejea uwanjani kuipigania Simba.



Chanzo: mwananchi.co.tz