Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nurkovic wa Kaizer aipigia saluti Simba

Samir  ED Nurkovic wa Kaizer aipigia saluti Simba

Mon, 24 May 2021 Chanzo: ippmedia.com

Akizungumza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi baada ya timu yake kufuzu hatua ya nusu fainali licha ya kuchapwa mabao 3-0, mchezaji huyo raia wa Serbia ambaye alifunga mabao mawili kwenye mechi ya kwanza wiki moja iliyopita nchini Afrika Kusini wakati wakishinda 4-0, alisema anashukuru kwa timu yake kufuzu, lakini wamepata ushindi huo kwa timu ngumu ya Simba ambayo iliwaelemea muda mwingi wa mchezo kwenye mechi hiyo ya marudiano, huku ikikosa nafasi nyingi za kufunga.

Alisema Simba ingeweza kuwatoa kwenye mashindano hayo kama wasingepata ushindi mkubwa kwenye mechi ya kwanza nyumbani katika Uwanja wa FNB.

“Tulitarajia mchezo mgumu, lakini kitu cha muhimu ni kwamba tumefuzu, tulishinda mchezo wa kwanza kwa kulazimisha, lakini wote tulijua Simba itacheza kwa kushambulia, lakini tumevuka,” alisema Nurkovic na kuongeza.

"Bila shaka, mara zote tunachukua mechi moja baada ya nyingine, na kuona kwa namna gani tutafika mbali, Simba ni timu nzuri sana na tulikuwa tunatarajia watakuja kwetu kwa presha kubwa, na kulazimisha sana kwetu, palikuwa hakuna cha kufanya zaidi ya kuzuia."

Nurkovic alisema, Simba walikuwa wapinzani waliostahili kwao, lakini ushindi wao katika mechi ya kwanza ndio ulioleta tofauti.

“Kwetu, ilikuwa muhimu sana kwamba tulitengeneza nafasi nyingi katika mechi ya kwanza nyumbani na tulizitumia na sasa tumeshinda kwa tofauti ya bao moja limetupeleka nusu fainali.”

Akiwazungumzia wapinzani wao, Simba, alisema ni timu nzuri sana na hawezi kukaa na kuwataja mchezaji mmoja mmoja, Nurkovic alisema yeye anaona kikosi chote ni kizuri na kinacheza kwa ushirikiano na kwa maelewano.

"Sijui sana habari ya ligi ya Tanzania, lakini naifahamu Simba kuwa ni timu nzuri na bora kabisa, yenye wachezaji wazuri, wanaocheza kwa ushirikiano na kwa maelewano. Kama wataendelea kukaa pamoja na kurekebisha vitu vichache msimu ujao wanaweza kufika mbali zaidi," alisema.

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, akizungumzia mechi hiyo, alisema wamesikitika kutolewa katika mashindano kwa sababu walistahili kushinda ila haikuwa bahati kwao kusonga mbele.

"Licha ya kutolewa, nina kila sababu ya kujivunia kuwa kocha wa Simba na aina ya wachezaji wangu kupambana hadi hatua ya mwisho, walijitolea sana na wamepigana vizuri sana yaliyotokea ni katika mpira.

"Ni kweli tulipoteza nafasi nyingi dakika 45 za kwanza ila sina shida na washambuliaji wangu, nina wafungaji wanaofanya vizuri sina hofu nao wakati mwingine huwa ni habati, kwa hii haikuwa kwetu," alisema Gomes.

Katika mchezo huo mabao ya Simba yalifungwa na John Bocco ambaye klabu yake ilimtangaza kuwa mchezaji bora wa mechi na kuzawadi Sh. milioni 2.5, huku la tatu likifungwa na Clatous Chama.

Kaize Chiefs sasa hatua ya nusu fainali itacheza na Wydad Casablanca ambayo juzi iliichapa MC Alger bao 1-0 nyumbani, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1, kufuatia sare ya bao 1-1 ugenini.

Imeandikwa na Adam Fungamwango na Saada Akida

Chanzo: ippmedia.com