Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nkongo: Marefa wanajipa presha Simba na Yanga

34545 Pic+nkongo Tanzania Web Photo

Wed, 2 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwamuzi wa Kimataifa wa Tanzania, Israel Nkongo amestaafu kuchezesha soka, lakini akasema hakuna mechi nyepesi kuchezesha kama za Simba na Yanga.

Nkongo aliyestaafu, juzi ilikuwa siku yake ya mwisho kutumikia soka kama mwamuzi, kwani kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), umri wa mwisho kwa mwamuzi kusimama katikati ya dimba isizidi miaka 45.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi hasa ugumu wa kuchezesha mechi za Simba na Yanga, Nkongo alisema: “Mechi za Simba na Yanga huwa hazina ugumu wowote, presha ya mchezo husababishwa na marefa wenyewe wanaopangwa kuzichezesha.

“Kutokana na ukubwa wa maandalizi ya mechi, tayari mwamuzi naye anapata presha lakini hakuna mechi nyepesi kuchezesha kama Simba na Yanga isipokuwa mechi zinazokutanisha timu ndogo ndizo huwa ngumu.

“Mechi ngumu ni zile zinazokutanisha timu ndogo mfano nikiwa naenda kuchezesha Mbao na Ndanda au Prisons na Mtibwa najiandaa kwelikweli kwani unaweza kujikuta unakimbizwa hadi unalala na viatu.

“Sijawahi kusumbuliwa na mechi hizo na mchezo pekee niliowahi kusumbuliwa nao ulikuwa ni baina ya Zambia na Somalia,” alisema Nkongo ambaye kitaaluma ni mwalimu wa hisabati.

Alisema: “Unapokuwa mwamuzi lazima uheshimike. Uwanjani ni kazini ila tukiwa huku nje ya uwanja tutaniane. Kwa hiyo mimi siyo mkali ila ni umakini katika kazi yangu.

“Unapokuwa uwanjani lazima uwe juu ya watu wote. Unalazimika uonyeshe kwamba una mamlaka na ujiamini kitu ambacho sasa hivi kinawashinda waamuzi wengi. Unaona kabisa mwamuzi anachezewa na wachezaji sio jambo zuri,” alisema Nkongo aliyeanza uamuzi mwaka 1994.

Kuhusu kuwa na mahaba na Simba au Yanga, Nkongo amefichua kuwa hana mapenzi na Simba wala Yanga kwa hapa nchini bali timu yoyote inayocheza kwa nidhamu ingawa barani Ulaya yeye ni mpenzi wa Liverpool.

Mwamuzi huyo aliyejizolea umaarufu mkubwa mwaka 2014 baada ya kufanyiwa vurugu na baadhi ya wachezaji wa Yanga, sasa amegeukia katika ukufunzi wa waamuzi wa soka na yeye ni mkufunzi wa kimataifa anayetambulika na Fifa pamoja na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

“Mimi ni mkufunzi wa kimataifa wa waamuzi na nafurahi kuona ninaondoka nikiwa nimewatengeneza waamuzi wengi vijana ambao ninaamini watafika mbali,” alisema Nkongo.

Mwenyekiti wa kamati ya waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Chama alisema Nkongo ni mwamuzi wa mfano wa kuigwa.

“Ni jambo la kipekee na la kufurahisha kuona Nkongo amevaa beji ya Fifa kwa miaka 10 mfululizo lakini pia ikumbukwe yeye ndiye mwamuzi aliyeweka rekodi ya kutwaa tuzo ya mwamuzi bora wa Ligi Kuu mara nne.

“Sisi kama shirikisho tunampongeza na tunaamini waamuzi wengine wataiga mfano wake na kuitumikia vyema fani ya uamuzi ili waje kututoa kimasomaso kama Nkongo alivyofanya,” alisema Chama.

Refa bora wa Ligi Kuu katika misimu miwili mfululizo ya 2016/2017 na 2017/2018, Heri Sasii aliliambia gazeti hili kuwa Nkongo anabakia kuwa alama muhimu kwao.

“Nkongo hakuwa mwalimu tu bali tunamtazama kama baba yetu katika fani hii ya uamuzi wa soka na kwa kweli hatuna cha kumlipa kwa jinsi ambavyo amekuwa akitujenga na kutusaidia tuweze kupiga hatua,” alisema Sasii

Historia ya Nkongo

Alimaliza elimu ya msingi mwaka 1985 na mwaka 1986 na baadaye elimu ya sekondari ambayo alihitimu kwenye shule ya vipaji maalum ya Kibaha mwaka 1989. Mwaka 1990 alijiunga na Shule ya Sekondari Mazengo kwa elimu ya kidato cha sita aliyomaliza mwaka 1992 na mwaka 1993 hadi 1994 alifanya mafunzo kwa mujibu wa sheria katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika Kambi ya Makutupora, Dodoma.

Septemba 1995 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikopata Shahada ya Elimu na mwaka 1999 baada ya kumaliza masomo yake ya Chuo Kikuu aliajiriwa na Wizara ya Elimu kama mwalimu. Mwaka 1994 alifanya mitihani ya uamuzi wa soka na kujiunga rasmi na fani hiyo na alianza kuchezesha rasmi Ligi Kuu mwaka 2004 huku beji ya FIFA akiipata mwaka 2009 na mchezo wake wa kwanza wa kimataifa ulikuwa ni baina ya Kenya na Uganda kwenye Mashindano ya Kombe la Chalenji.

Ana mke na watoto wawili na mbali na soka amekuwa akipendelea michezo ya riadha, mbio za magari na mieleka.

Chanzo: mwananchi.co.tz