Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Njaa yanukia Ligi Kuu, TFF yahaha

12035 Pic+ligi TanzaniaWeb

Wed, 15 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ni kilio kila kona kwa klabu za Ligi Kuu Bara baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) kutangaza ligi hiyo msimu huu itaanza bila ya kuwa na mdhamini mkuu.

Hali hiyo inatokana na waliokuwa wadhamini wakuu wa ligi hiyo, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kushindwa kuongeza mkataba baada ya ule wa awali wa miaka mitatu wenye thamani ya Sh 6.6 bilioni kumalizika msimu uliopita. Kujiondoa kwa wadhamini hao kunazifanya klabu kukosa takribani Sh80 milioni kwa msimu, fedha hizo zilikuwa zikitolewa kwa awamu nne kwa mwaka, kila awamu timu zilikuwa zikipewa Sh20 milioni kabla ya ligi kuanza.

Katika udhamini huo, bingwa alipata Sh80.4 milioni, mshindi wa pili Sh40.2 milioni na wa tatu, Sh28.7 milioni. Mshindi wa nne Sh22 milioni na timu yenye nidhamu, Sh17 milioni.

Mchezaji bora na mfungaji bora, kila mmoja aliingiza kibindoni Sh 5.7 milioni, wakati kipa bora alituzwa Sh 5 milioni, kocha na mwamuzi bora kila mmoja alijipatia Sh8.6 milioni.

Hata hivyo, TFF imeweka wazi kuwa ligi hiyo imebaki na wadhamini wenza wawili ambao ni Azam Media wanaotoa Sh162 milioni kwa mwaka na Benki ya KCB itayotoa Sh 15 milioni kwa kila timu kwa mwaka.

Akizungumzia kadhia hiyo Rais wa TFF, Wallace Karia alisema bado wanazungumza na kampuni mbalimbali ili kufanikisha suala la udhamini mkuu.

Karia alisema kuwa TFF haijakata tamaa kusaka wadhamini na kuomba timu kujiandaa kukabiliana na hali hiyo na anaamini itamalizika muda sio mrefu.

“Bado tunatafuta wadhamini, wapo ambao tunazungumza nao, hatujalala, tunafanya kazi, tunaamini tutafanikiwa na kuondoa changamoto hii iliyojitokeza,” alisema Karia.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema kuwa bado wapo katika mazungumzo na wadhamini mbalimbali na watakapofanikisha watatangaza.

Klabu zalia ukata

Baadhi ya viongozi wa timu hizo wamekiri kupokea waraka kutoka Bodi ya Ligi ukielezea suala hilo wakati ligi ikiwa imebakiza wiki moja tu kabla ya kuanza ikiwa jumla ya timu 20 zitashiriki kwa mara ya kwanza.

Katibu Mkuu wa klabu ya Singida United, Abdulrahman Sima alisema wamepokea waraka kutoka TPLB kuhusiana na kukosekana kwa mdhamini mpaka sasa na kusema hali hiyo itawarudisha nyuma na kuwaweka katika hali ambayo haieleweki.

Sima alisema kuwa pamoja na kuwa na wadhamini, bado fedha ya udhamini mkuu na vifaa ambavyo walikuwa wanavipata vifaa vya mazoezi na mechi zilikuwa zinapunguza gharana mbalimbali ambazo zilikuwa zinawavusha kwa kiasi fulani.

“Msimu uliopita, tulipewa nauli kutoka kwa wadhamini, sasa kama msimu huu mambo bado, hali itakuwa tofauti, Singida United ipo Mwanza, tukitoka Mwanza, tutakwenda Mbeya, hii nauli tutaitoa wapi na muda unakaribia, je fedha hizi tutazitoa wapi,” alisema Sima.

Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema timu zitaathirika kukosekana kwa wadhamini wa Ligi Kuu lakini sio kwa kiwango cha kutisha kwa sababu hata wadhamini wa misimu ya hivi karibuni, Kampuni ya Vodacom Tanzania haikuwa ikitoa kiasi kikubwa cha fedha kwa klabu.

“Kukosekana kwa udhamini katika Ligi, haiwezi kupunguza morari kwa sababu hata hao Voda walikuwa hawazisaidii sana timu walikuwa wanatoa kiasi kidogo sana cha pesa Klabu zenyewe ndio zilikuwa zinajikamua, Mzigo utaongezeka lakini morali haitoshuka…” alisema.

Mmiliki wa timu ya African Lyon, Rahim Kagenzi ‘Zamunda’ naye alisema mpaka sasa wamechanganyikiwa kwani walitegemea kupata fedha za udhamini mkuu ili kufikia malengo yao.

Kagenzi alisema kuwa wanahitaji kuhangaika zaidi ili kupata fedha kwani hali bado siyo nzuri kabisa.

“Hii sasa ni ‘tough assignment’, matarajio yetu ni kupata fedha za mdhamini mkuu kama ilivyokuwa zamani ambapo tulikuwa tunapewa na vifaa, sasa hakuna hiyo,” alisema Kagenzi.

Mwenyekiti wa Klabu ya Mbao FC, Solly Njashi alisema kama Ligi Kuu itaendeshwa bila mdhamini mambo yatakuwa magumu kutokana na timu kukosa fedha, huku zikitarajiwa kutumia gharama kubwa.

“Japo hatujapata taarifa rasmi ya kutokuwapo kwa mdhamini lakini kama atakosekana mambo yatakuwa magumu kwa timu kwa sababu gharama ni kubwa mno, kuna suala la usafiri, posho, malazi na mengineyo,” alisema Njashi.

Meneje wa Biashara United, Aman Josiah alisema kama ligi hiyo itakosa mdhamini morari na ushindani vitashuka kwa klabu shiriki haswa kwa timu ndogo.

“Timu zitaathirika sana haswa hizi za kwetu changa, morari na ushindani vitapungua mno, ila kwa ujumla bado hatujapewa taarifa rasmi kama Ligi imekosa mdhamini kwa hiyo tunaendelea kusubiri,” alisema Josiah.

Naye Katibu Mkuu wa Mwadui FC, Ramadhan Kilao alisema kuwa ni mapema kuelezea suala hilo, kwani taarifa ya mwisho waliyopewa ilieleza kuwa TFF inaendelea kufanya mazungumzo na baadhi ya kampuni ziweze kudhamini.

Katibu Msaidizi wa Alliance FC, Hassan Kasembe alisema klabu changa kama wao watapata changamoto kubwa kama atakosekana mdhamini rasmi kutokana na gharama kubwa kuhitajika.

“Kwa Klabu kama zetu mambo yatakuwa magumu sana, tunahitaji pesa nyingi kuendeshea timu hata kama kutakuwepo na ufadhili kidogo, lakini uwepo wa mdhamini ni muhimu sana,” alisema Kasembe.

Katibu Mkuu wa Tanzania Prisons, Havintish Abdalah alisema hawajapokea barua yoyote ile kutoka kwa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) ikielezea kwamba msimu ujao wa Ligi Kuu Bara itachezwa bila ya kuwa na mdhamini.

“Hizo taarifa bado hatujapata, ila kama ikiwa hivyo, basi ligi itakuwa ngumu sana kwani hakuna klabu iliyokuwa imejiandaa kisaikolojia kucheza bila ya kuwa na mdhamini. Lakini pia ladha ya ligi haitakuwepo kabisa.”

Sauti ya wadau

Mchambuzi na mchezaji wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa, Ally Mayay alisema klabu zinatakiwa kujiandaa na changamoto kubwa ya gharama za kujiendesha kutokana na kutokuwa na uhakika wa kupatikana mdhamini mkuu mpaka sasa.

Mayay alisema kuwa pamoja na kuwa udhamini wa zamani wa Ligi Kuu ulikuwa hautoshi, lakini kukosekana kabisa imeleta zahama kubwa kwa wachezaji na viongozi wa klabu nyingi.

“Ni ngumu kuanza Ligi Kuu bila kuwa na mdhamini, TFF na TPLB zinahitajika kuongeza bidii ili kuhakikisha timu zinapunguziwa mzigo wa gharama, maana msimu uliopita ulikuwa na timu 16 na kucheza mechi 30, safari hii timu zimeongezeka na zinatakiwa kucheza mechi 38, zinahitajika kusafiri zaidi,” alisema Mayay.

Alisema kuwa kwa timu kama Simba, Yanga, Azam, Mtibwa Sugar, Kagera na zenye uhusiano na taasisi, hali inaweza kuwa nafuu, lakini bado watakutana na changamoto.

Deo Lucas, Meneja wa timu ya Taifa ya soka la ufukweni na mchezaji wa zamani wa Yanga alisema “Kitendo cha kujitoa kwa Vodacom kudhamini Ligi Kuu, kutapunguza upinzani kwa kiasi fulani kwani timu nyingi hazitakuwa na nguvu za kushindana kwa kutegemea mapato yao kwa kuwa timu nyingi hazina vyanzo vya mapato...hapa ndio utaona utofauti wa timu zile zenye uwezo na zisizo na uwezo.”

“Tatizo klabu nyingi zinaendeshwa kizamani ndio maana hata kuaminika kwa wadhamini imekuwa shida! Kwa kipindi kidogo kilichobaki ni ngumu kupata wadhamini kama walikuwa bado hawajafanya hivyo! Inatakiwa klabu zibadilike sasa... Waende kisasa zaidi na mafunzo, wajifunze kujua watumie njia gani kati ya walizozipata kwenye somo la klabu licence,” alisema Lucas.

Imeandaliwa na Majuto Omary, Saddam Sadick na Godfrey Kahango.

Chanzo: mwananchi.co.tz