Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni Simba na Yanga fainali FA

190980bd3afc98b452f0de702034087e Ni Simba na Yanga fainali FA

Sat, 26 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BAO la dakika ya 89 lililofungwa na kiungo mshambuliaji Luis Miquissone, limeipeleka Simba fainali ya michuano ya Kombe la FA kufuatia ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Azam FC leo katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Simba kucheza fainali za michuano hiyo tangu kuanzishwa msimu wa 2016 na ni mara ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kutinga na kutwaa taji hilo mbele ya Namungo FC ya Lindi.

Ushindi huo unaifanya Simba kukutana na Yanga, kwenye mchezo wa fainali, ambao utapigwa Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma na hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa miamba hiyo ya soka kukutana katika hatua ya fainali baada ya msimu uliopita kukutana nusu fainali na Simba kushinda kwa mabao 4-1.

Katika mchezo huo, timu zote mbili zilionesha kukamiana na kusababisha ladha ya mchezo iliyokuwa ikitarajia kupotea kutokana na rafu zilizosababisha mwamuzi kutoa kadi nyingi za njano kwa wachezaji wa pande zote mbili.

Simba walitengeneza nafasi moja ya wazi kipindi cha kwanza, lakini shuti lililopigwa na Mzamiru Yassin ulitoka nje kidogo ya lango la Azam, lakini dakika chache baadaye kiungo wa Azam Salum Abubakar ‘Sure Boy’ naye alimjaribu kipa wa Simba Aishi Manula, lakini alikuwa makini kwa kuutoa nje na kuwa kona.

Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa bado hazijafungana huku wachezaji Daniel Amoah wa Azam akioneshwa kadi ya njano mapema dakika ya 14 , wakati kwa upande wa Simba, Taddeo Lwanga aliadhibiwa na mwamuzi wa mchezo huo baada ya kumchezea vibaya Idd Seleman ‘Nado.

Kipindi cha pili, Simba walikianza kwa kufanya mabadiliko ya kumtoa Mzamiru na kumuingiza Meddie Kagere ambaye alikwenda kushirikiana na John Bocco, lakini kutokana na timu zote kucheza kimbinu zaidi mshambuliaji huyo hakuweza kuwa na madhara kama ilivyozoeleka.

Sure Boy alipoteza nafasi ya wazi ya kuifungia Azam bao la kuongoza baada ya kumpora mpira Joashi Onyango, lakini alishindwa kuitumia vyema nafasi kutokana na papara iliyopelekea shuti alilopiga kushindwa kulenga lango.

Kocha wa Simba, Didier Gomes baada ya kuona mambo magumu alifanya mabadiliko mengine kwa kumuingiza Bernard Morrison kuchukua nafasi ya Rally Bwalya, ambapo mchezaji huyo alichangamsha mchezo na kuwasumbua walinzi wa Azam FC ambao alionesha kukosa mbinu za kumdhibiti.

Wakati mashabiki waliokuwa wakiufatilia mchezo huo wakiamini kwamba timu hizo zitaongezwa dakika 30 kabla kwenda kwenye mikwaju ya penalti kama zingeshindwa kufungana beki wa Azam FC Bruce Kangwa alimchezea rafu Morrison na mwamuzi kuamuru ipigwe faulo ambayo wachezaji wa Simba aliitumia kufunga bao hilo pekee lililowapeleka fainali ya michuano hiyo ikiwa ni mara ya pili mfululizo.

Morrison aliuanzisha mpira haraka kumuanzia Miquissone kabla walinzi wa Azam hawajajipanga na mchezaji huyo kufunga bao jepesi jambo ambalo wachezaji wa Azam walionekana kutokubaliana na utaratibu huo na kuanza kumzonga mwamuzi kitu kilichosababisha wachezaji Obrey Chirwa na Bryson Rafel kuoneshwa kadi za njano kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz