Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngorongoro yaweka rekodi tatu ikitwaa ubingwa Chalenji

78682 Ngoro+pic

Mon, 7 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jinja. Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ imetwaa ubingwa wa mashindano ya Cecafa Chalenji baada ya kuifunga Kenya bao 1-0, huku Kelvin John akiibuka mfungaji bora na mchezaji bora wa mashindano hayo.

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Kituo cha Ufundi cha Fufa Jinja, bao la Ngorongoro Heroes lilitokana na beki wa Kenya, Onyango Otieno kujifunga katika dakika ya 46 wakati akiokoa mpira wa faulo uliopigwa na Israel Mwenda.

Kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na Ngorongoro kwenye mashindano kilikuwa chachu ya kutwaa ubingwa huku safu ya ushambuliaji ikitikisa.

Tangu hatua ya makundi Ngorongoro Heroes imecheza michezo sita, imeshinda mitano na kutoka sare mmoja, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 18 na kuruhusu matano katika michezo yote. Katika mchezo wa jana, timu zote zilianza kwa kushambuliana kwa zamu, lakini safu za ulinzi zilikuwa imara.

Dakika ya 46, Kelvin John alifanyiwa madhambi umbali wa mita 20 kutoka goli la Kenya na Israel Mwenda kupiga faulo, na wakati Otieno akiruka kuokoa alijikuta akiusukumiza wavuni kwa kichwa.

Ngorongoro Heroes na Kenya zilicheza fainali zikiwa zinafahamiana kwani zilikutana awali kwenye hatua ya makundi na kutoka sare ya mabao 2-2.

Pia Soma

Advertisement
Baada ya mchezo huo, Kelvin alitangazwa kuwa mfungaji bora wa mashindano akiwa amepachika mabao saba akimzidi moja mshambuliaji mwenzake Andrew Simchimba aliyefunga sita.

Pia mchezaji huyo ambaye anahusishwa kujiunga na timu ya vijana ya Genk ya Ubelgiji alitangazwa mchezaji bora wa mashindano.

Tuzo ya kipa bora ilikwenda kwa Okoth Brian wa Kenya ambaye ameruhusu mabao manne ikiwa ndio timu iliyoruhusu mabao machache sawa na Sudan Kusini ambayo ilitolewa kwenye hatu ya robo fainali.

Pia, Uganda ambao ndio walikuwa wenyeji wa mashindano walitangazwa timu bora yenye nidhamu.

Katwila amwaga pongezi

Kocha wa Ngorongoro Heroes, Zubery Katwila akionekana mwenye furaha aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kutwaa ubingwa.

“Haikuwa kazi rahisi kucheza na Kenya kwani tulishacheza nao kwenye makundi, hivyo tulijuana, lakini tulijipanga kiufundi kuwakabili na kufanikiwa kushinda na kutwaa ubingwa,” alisema.

Naye kocha wa Kenya, Stanley Okumbi aliwapongeza Ngorongoro Heroes akisema wachezaji wake walishindwa kutumia nafasi walizopata hivyo wanarejea kwao kujipanga kwa ajili ya mashindano mengine.

Kikosi cha Ngorongoro: Abdul Seleman, Israel Mwenda, Gustapha Runkomba, Dickson Job, Oscar Masai, Tepsi Theonassy, Novatus Miroshi, Andrew Simchimba, Kelvin John, Razack Shekimweri na Kelvin Naftal.

Chanzo: mwananchi.co.tz