Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ng’anzi, kinda anayepeleka makali Ligi Kuu Marekani

46122 PIC+NGAZI Ng’anzi, kinda anayepeleka makali Ligi Kuu Marekani

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Maisha ni safari ndefu. Hakuna njia ya mkato kupata mafanikio katika jambo lolote unalokusudia kufanya katika maisha.

Idadi kubwa ya watu waliopata mafanikio wakiwemo wachezaji wamepitia changamoto kubwa kabla ya kuanza kula matunda yaliyotokana na jasho lao.

Vivyo hivyo, usemi huu umemtokea mchezaji kinda Mtanzania Ally Ng’anzi ambaye ana historia ya kuvutia kuhusu maisha yake ya soka akipanda milima na mabonde.

Baada ya kupambana muda mrefu katika soka ya mchangani, hatimaye Nganzi ametua rasmi Minnesota United inayoshiriki Ligi Kuu Marekani.

Ni dhahiri Ng’anzi atacheza ligi moja na nahodha na mshambuliaji nyota wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney anayecheza klabu ya DC United.

Akizungumza na gazet hili katika makala maalumu, mchezaji huyo amefunguka kuhusu mikasa aliyokumbana nayo tangu akiwa Jamhuri ya Czech. Ng’anzi mwenye miaka 18 aliyetua Minnesota United Jumatatu ya wiki iliyopita baada ya kufuzu vipimo vya afya, amejiunga kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea MFK Vyskov ya Daraja la Pili Jamhuri ya Czech.

Anasema mkopo huo una kipengele cha kununuliwa moja kwa moja endapo atafanya vyema katika klabu hiyo yenye maskani Minneapolis State. “Najisikia furaha sana kila kitu kimekamilika najiona kama nipo nyumbani kutokana na raia wengi wa huku tuna asili ya Afrika. “Pale Czech kuna wakati nilijiona mpweke ilikuwa mara chache sana kukutana na watu wenye asili ya Afrika,”anasema kinda huyo.

Ng’anzi ambaye alikuwa sehemu ya timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’ iliyoshiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika, ‘Afcon 2017’ , Gabon, anasema hawezi kusahau namna alivyotua Czech na magumu ambayo alikutana nayo.

Czech

Ng’anzi anasema baada ya kikamilika usajili wake alitua Jamhuri ya Czech na kukutana na mapokezi mazuri ambayo hakutegemea huku akishangaa uzuri wa Taifa hilo.

“Nilianza kucheza Kikosi B nilikuwa nikiangaliwa uwezo na kocha msaidizi nilicheza mechi kama tatu, alikubali uwezo wangu wakaamua kunipeleka kikosi cha kwanza,” anasema kinda huyo.Kiungo huyo anasema mchezo wa kwanza alikuwa katika benchi dhidi ya Rymarov Oktoba 20 mwaka jana lakini hakucheza.

“Tulifungwa mabao 2-1. Mchezo wa pili pia sikupata nafasi ya kucheza safari hiyo tulishinda 2-1, mchezo wa tatu pia sikupata nafasi, lakini nashukuru Mungu ilikuwa Novemba 10 tukiwa nyumbani nilicheza kwa dakika 17.

“Dakika zile zilitosha kocha kunikubali kwa sababu nilichokuwa nakifanya ni kuhakikisha natoa sapoti kwa mabeki wa kati pia nilikuwa nikiachia mipira kwa haraka, penye ulazima wa kukaa nao nilifanya hivyo na kupiga mashuti,” anasema Ng’anzi.

Ng’anzi anasema walishinda mabao 4-1 mchezo uliokuwa wa mwisho kwake kabla ya kurejea nchini kwa mapumziko ya muda mrefu baada ya ligi kusimama kwa muda.

Simba, Yanga

Ndoto ya idadi kubwa ya wachezaji wa Tanzania ni kucheza Simba au Yanga, lakini kwa Ng’azi imekuwa tofauti anataka kucheza soka Ulaya. Pia anamtaja kiungo Mudathir Yahya wa Azam ni mchezaji anayemvutia katika soka la Tanzania.

Lugha

Mbali na Kingereza ambacho kimekuwa kikitumika kwa mataifa mengi ya Ulaya, Ng’anzi anasema hakuna kitu kinachomuumiza kichwa kama lugha ambayo imekuwa ikitumika nchini humo ambayo ni Kislovak.

Chakula

Pamoja na kukumbuka vyakula vya nyumbani ambavyo ndivyo vilivyomlea hadi anatimiza miaka 18, Ng’anzi anasema chakula cha Jamhuri ya Czech hakimpi taabu.

Chanzo: mwananchi.co.tz