Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Netiboli yapambana kurudi kimataifa, Filbert Bayi atajwa

Net Ball Netiboli yapambana kurudi kimataifa

Thu, 3 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Baada ya kupoteza ramani kwa zaidi ya miaka minane, Chama cha Netiboli Tanzania 'Chaneta' kimeanza kupambana kurudisha makali kwenye anga za kimataifa huku ikimtaja mwanariadha nyota, Filbert Bayi kujitoa kuwasaidia.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kimataifa ya makocha na waamuzi 48 wa mchezo huo nchini yanayoendelea kwenye kituo cha Filbert Bayi, Kibaha Mkuza mkoani Pwani, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Chaneta, Shukuru Mohammed Kiwege amesema mkakati uliopo ni kuirudisha Tanzania kwenye ramani ya kimataifa.

Kiwege ambaye ni mratibu wa mafunzo hayo amesema yanakwenda kutoa mwanga mpya kwa makocha na waamuzi watakaohitimu.

"Wamefanya mtihani leo, washindi wa daraja la kwanza ambao kwenye netiboli tunawaita wa ngazi ya dhahabu hawa watatunukiwa leseni za Afrika level one, hivyo wataweza kufundisha na kuchezesha mashindano ya kimataifa kwenye timu za Afrika.

"Pia kutakuwa na wahitimu wa daraja la fedha na shaba ambao kila mmoja atakuwa na levo yake ya ufundishaji kwa makocha na uchezeshaji kwa waamuzi.

"Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwa na wataalamu wengi ambao wataendeleza mchezo huu nchini na kusapoti mpango wa Chaneta wa kurudi kwa nguvu mpya kwenye ramani ya kimataifa," amesema.

Amesema licha ya mafunzo hayo kuratibiwa na Chaneta lakini wameweza kutumia vifaa mbalimbali ikiwa viwanja vya kisasa kwenye kituo cha Filbert Bayi.

"Ni kama anatusaidia tu, kwani hapa tunalipia Sh 15,000 kwa siku kwa mtu mmoja, ambayo ni gharama ya malazi, na chakula kuanzia asubuhi hadi jioni tena vya kiwango bora.

"Achilia mbali viwanja vya kisasa vilivyoko katika 'complex' hii, huyu mzee ni kama anatupa tu msaada, kama Chaneta hatuna cha kumlipa, ila tunamuombea azidi kuwa na moyo huu wa kusaidia familia ya michezo," amesema.

Kocha wa timu ya taifa, Hafidh Tindwa ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo amesema, hamasa ya ushiriki imeongezeka na kusisitiza kwamba kama kila mmoja atayatumia mafunzo hayo kwa ukamilifu, Tanzania inarudisha hamasa ya mchezo huo.

"Ni mafunzo ambayo kila mshiriki ameyafurahia, kuanzia darasani, uwanjani na hata mazingira ya viwanja ambayo ni ya levo ya kimataifa," amesema.

Mwamuzi Beatrice Selemani ambaye pia ni mwalimu kitaaluma kutoka Morogoro amesema kwa mara ya kwanza ameshiriki mafunzo yenye hadhi ya kimataifa.

"Binafsi kama ningeweza ningewashauri Chaneta kufanya kituo hiki kuwa kambi yao ya kudumu miaka yote, kuna viwanja vya kisasa, hosteli na mazingira rafiki kwa wanamichezo," amesema.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Mery Waya anayetambuliwa na  Shirikisho la Netiboli la Kimataifa (IFN), amesema yatatoa fursa kwa makocha na waamuzi watakaofaulu mtihani kwa daraja la kwanza kupata leseni za Netiboli Afrika.

Waya aliyewahi kuwa kocha mkuu wa Taifa Queens amesema kama kutakuwa na madaraja manne tofauti ya ufaulu na wale wa daraja la gold ndiyo wataweza kupata leseni ya Afrika.

"Mpaka sasa sijajua yupi atafaulu kwa levo ya dhahabu au vinginevyo, lakini wote makocha 25 na waamuzi 23 ambao hao wananolewa na mwenzangu kutoka Malawi pia, Dk Rebecca Dulanya wameonyesha jitihada.

"Naikumbuka Tanzania ilivyokuwa juu wakati Chaneta ikiongozwa na Anna Bayi (sasa ni marehemu) kulikuwa na mashindano mengi sana, hivyo natarajia kasi ile inakaribia kurejea tena," amesema.

Ofisa michezo wa Halmashauri ya Kibaha, Burwan Tulusubya amesema mafunzo hayo yanakwenda kuleta mwanga kwenye mchezo huo.

"Japo Kibaha tuna changamoto ya viwanja vya netiboli, ukiondoa huu wa Filbert Bayi na wa Shirika la Elimu ambavyo ni vya kusasa, bado tunaamini wahitimu wetu watapambana kuhakikisha vijana wanajua sheria na wanapopata nafasi ta kutumia viwanja vya kisasa basi tutashirikiana na mdau wetu Filbert Bayi kwenye hilo na bahati nzuri amekuwa akijitoa,".

Mafunzo hayo yanashirikisha waamuzi na makocha 48 kutoka mikoa mbalimbali nchini ambayo yanatarajiwa kufungwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Abbas Hassan.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz