Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndumbaro, Rage waibuka uchaguzi Simba

18098 Pc+ndumbaro TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kusimamisha uchaguzi mkuu wa Klabu ya Simba, wadau wa michezo wametoa maoni tofauti kuhusu hatima ya kinyang’anyiro hicho.

Juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Revocatus Kuuli, alisema uchaguzi huo umesimamishwa kwa madai ya klabu hiyo kukiuka baadhi ya kanuni ndani ya katiba.

Simba ilitangaza kufanya uchaguzi Novemba 3, lakini wadau mbalimbali akiwemo mwanasheria mwenye uzoefu wa kutosha na masuala ya soka Dk Damas Ndumbaro, alisema anaunga mkono kauli ya Kuuli.

Akizungumza jana, Ndumbaro alisema Simba inapaswa kufuata kanuni za uchaguzi za TFF ili kuepuka mkanganyiko unaoweza kuibua sintofahamu baina ya pande hizo mbili.

Ndumbaro alisema Simba ni mwanachama wa TFF na haina kanuni za uchaguzi, hivyo inapaswa kufuata kikamilifu kanuni za uchaguzi za shirikisho hilo ili kupata viongozi halali.

“Kamati ya Uchaguzi ya Simba inapaswa kuheshimu kanuni za uchaguzi za TFF, inawezekana kamati ya uchaguzi ya sasa labda haina uzoefu lakini inapaswa kusoma vizuri kanuni kuzielewa na kuzifuata.

“Ingekuwa Simba ina kanuni zake ambazo zingepitishwa na TFF hilo lingekuwa jambo jingine, lakini kwa sababu haina inatakiwa kutii kile kilichoandikwa kwenye kanuni za uchaguzi za TFF,”alisema Dk Ndumbaro.

Pia alisema Simba inatakiwa kufuata kanuni kuhusu kiwango cha elimu na gharama za ununuzi wa fomu ya uchaguzi kama ulivyoanishwa na TFF.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema kipengele cha elimu kwa mgombea wa nafasi ya urais kuwa na shahada kinatakiwa kutupiwa jicho.

“Pamoja na kanuni ya elimu, lakini tukumbuke wazee walioongoza Simba hawakuwa na elimu ya digrii, lakini ndiyo hao wameondoka na hadi leo wametuachia kumbukumbu ya majengo,” alisema Rage.

Pia Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) sasa TFF, alisema kipengele hicho kinaacha maswali kwa kuwa hakijafafanua shahada ipi inayotakiwa kwa nafasi ya urais.

“Kipengele cha elimu hakijaainisha ni digrii ya nini inahitajika kwa kuwa wapo watu wana digrii ya dini na wengine ya ushonaji.

“Kuhusu bei ya fomu kuwa 500,000 siwezi kuizungumzia, lakini cha msingi nishauri wanachama wetu wa Simba wasome katiba na kuilewa,” alisema Rage.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Simba Boniphace Lyamwike alidai kuwa hajapata taarifa rasmi za kusimamishwa uchaguzi huo.

“Hatujapata taarifa rasmi kwa sababu hakuna mawasiliano yaliyofanyika kati ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF na Kamati ya Uchaguzi ya Simba.

Hata hivyo, Lyamwike alisema wanaendelea na mchakato wa uchaguzi hadi watakapopata taarifa rasmi kuhusu kusimamishwa uchaguzi.

“Hakuna tofauti kubwa Katiba ya Simba inaelekeza kama kutakuwa hakuna kanuni za uchaguzi za Simba tutatumia za TFF.

“Kimsingi hakuna kanuni za uchaguzi Simba moja kwa moja, katiba yetu imetuelekeza kwenda kwenye Kanuni za TFF na tumefuata kanuni za uchaguzi za TFF zinavyosema ikiwemo viwango walivyotoa na sisi tumepanga,” alisema mwenyekiti huyo.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF Wakili Revocatus Kuuli alisema uchaguzi wa klabu hiyo umesimamishwa kwa kukiuka baadhi ya kanuni za uchaguzi.

“Wamepanga ada kuwa Sh500,000 na sifa za mgombea wa nafasi ya mwenyekiti digrii, lakini kwa mujibu wa kanuni wanatakiwa kutumia kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF ambazo zinataka mgombea awe na elimu ya kuanzia kidato cha nne na gharama za kuchukua fomu kwa nafasi ya mwenyekiti Sh200,000 na nafasi nyingine Sh100,000,”alisema Kuuli.

Chanzo: mwananchi.co.tz