Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndolanga kuzikwa leo Kibaha

97024 Ndolanga+pic Ndolanga kuzikwa leo Kibaha

Sun, 19 Sep 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mwili wa Muhidin Ndolanga utapumzishwa leo saa saba mchana kwenye nyumba yake ya milele, Kibaha Mkuza mkoani Pwani.

Ndolanga mwenyekiti wa zamani wa Chama cha soka Tanzania (FAT sasa TFF) alifariki jana kwenye hospitali ya TMJalikokuwa amelazwa akisumbuliwa na tatizo la moyo.

Hadi mauti inamkuta, Ndolanga alikuwa rais wa heshima wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Binamu wa marehemu, Khatib Abdallah amesema kaka yake atazikwa kwenye eneo lake lililopo Mkuza ambako ndipo mwili wa mkewe umezikwa.

"Enzi za uhai wake aliomba azikwe jirani na kaburi la mkewe ambaye alifariki miaka ya nyuma na kuzikwa kwenye shamba lake lililopo Mkuza," amesema.

Amesema mwili wa Ndolanga uko nyumbani kwake Mikocheni ambako ulipelekwa baada ya kuandaliwa kwa imani yake ya Kiislamu kwenye hospitali ya Lugalo na safari ya kuelekea makaburini itaanza saa 6 mchana kuelekea Kibaha Mkuza.

Ndolanga, anakumbukwa kwa misimamo thabiti enzi ya uongozi wake FAT (sasa TFF), na namna alivyonusurika kifungo baada ya hakimu kumwambia hana hatia, akimuacha mahakamani katibu wake mkuu, Ismael Aden Rage na Yonaza Seleki, aliyekuwa mhazini.

Moja ya mahojiano yake na gazeti hili enzi za uhai wake aliwahi kueleza namna alivyoikumbuka keshi hiyo ambayo alipoambiwa hana hatia jakutaka  hata kugeuka nyuma japo aliamini ilikuwa ni kesi ya kumchafua baada ya majaribio kadhaa ya kupinduliwa FAT kukwama.

“Serikali kupitia Kurugenzi ya Maendeleo ya Michezo ndiyo ilinishtaki. Ilikuwa ni kesi ya kunichafua baada ya kuona kila njia ya kuniondoa madarakani imeshindikana ndipo wakanipa kesi ile,” aliwahi kusema Ndolanga enzi za uhai wake akibainisha kwamba alishtakiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za FAT ambazo alitumia kulipa huduma ya simu.

Katika utawala wake, mara kadhaa Serikali iliingilia kati masuala ya soka, ikiwa ni pamoja na kumuengua madarakani, lakini baadaye Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) likatishia kuivua Tanzania uanachama.

Hata ulipoundwa uongozi wa muda, Ndolanga aliupinga na baadaye Fifa kutoa maelekezo ya jinsi ya kuunda kamati ya uongozi iliyoshirikisha pande zote mbili zilizokuwa katika mgogoro.

Juhudi nyingine za kumtoa Ndolanga kwa kura zilishindikana kutokana na wapigakura kumuunga mkono hadi idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu ilipoongezeka na kura kulazimika kupigwa mara mbili ndipo alipoanguka.

Kiongozi huyo wa zamani wa Pan African atakumbukwa namna uongozi wake FAT ulivyoondolewa siku ya hafla ya kuiaga Prisons kwa ajili ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.

Makamu wa rais, Dk Omari Ally Juma alikuwa mgeni rasmi wakati wa kuiaga timu. Katika hotuba yake alisema FAT ni uozo mtupu, baada ya hafla ile Juma Kapuya (aliyekuwa waziri mwenye dhamana na michezo) alimuagiza Leonard Thadeo kuitisha mkutano wa kuijadili FAT.

Uongozi wa FAT Uliitwa Morogoro, katika mkutano Kapuya alitangaza kuifuta Kamati ya Utendaji ya FAT, na Ndolanga alituma fax Fifa kuhusu kilichotokea na Serikali kuingilia masuala ya michezo.

Siku iliyofuatia mapema Fifa ilijibu kwa kuifungia Tanzania kutokana na tukio hilo, nchini iundwa kamati ya watu watatu ambao ni Anna Abdallah, Joseph Mungai na Profesa Phillemon Sarungi kuchunguza jambo hilo na kupata mwafaka, na kuzungumza na Ndolanga akataka Kapuya aiondoe kamati yake aliyoiweka FAT akidai hicho ndicho chanzo cha Tanzania kufungiwa na Fifa, akafanya hivyo na Tanzania ikafunguliwa.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz