Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndayirajige ameingia kitanzini Taifa Stars

66655 Pic+stars

Sun, 14 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumtangaza, Etienne Ndayiragije kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars akichukua nafasi ya Emmanuel Amunike aliyetimuliwa, baadhi wa makocha nchini wamesema kocha huyo “ameingia kwenye kitanzi baada ya mtangulizi wake kutolewa kafara”.

Ndayiragije ameteuliwa kukaimu nafasi hiyo baada ya TFF kuachana na Amunike, nyota wa zamani wa Barcelona na timu ya Taifa ya Nigeria, ikiwa ni siku kadhaa baada ya Stars kurejea kutoka Misri kwenye fainali za mataifa ya Afrika (Afcon).

Katika fainali hizo, Stars ilifungwa mabao 2-0 dhidi ya Senegal na 3-0 dhidi ya Algeria, timu ambazo zimetinga nusu-fainali ya mashindano hayo, sanjari na kupoteza kwa mabao 3-2 dhidi yaKenya katika hatua za makundi.

Baada ya kuachana na Amunike, TFF imempa ‘mikoba’ Ndayiragije ambaye amependekeza benchi lake la ufundi kusaidiwa na kocha Juma Mgunda wa Coastal Union na Suleiman Matola wa Polisi Tanzania sanjari na Meneja, Nadir Haroub Cannavaro nafasi ambazo wakati wa Amunike, msaidizi wake alikuwa Hemed Morocco na Daniel Msangimeneja.

Ndayirajige aliyewahi kuzinoa klabu za Mbao, KMC na sasa Azam ataiongoza Stars katika mchezo wa kufuzu fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) ambapo Stars itafungua dimba dhidi ya Harambee Stars ya Kenya Julai 28.

Wakizungumiza uteuzi huo, baadhi ya makocha wamesema Ndayiragije pia ameingia kwenye ‘kitanzi’ cha TFF kwani kuna tofauti kati ya kufundisha klabu na timu ya Taifa.

Pia Soma

Aliyewahi kuwa kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa alisema, Ndayiragije atakutana na changamoto nyingi kwenye kikosi cha Stars.

“Unajua mafanikio kwenye klabu ni tofauti kidogo na timu ya Taifa, kwenye klabu wachezaji unakuwa nao kila siku, kwenye timu ya Taifa huwezi kupata muda kurekebisha vitu vingi na bahati mbaya wachezaji wetu wengi wao bado sio profesheno,” alisema Mkwasa.

Kocha Kenny Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema kuteuliwa kwa Ndayiragije hakumaanishi kwamba Amunike aliishindwa Stars.

“Naweza kusema Amunike amefanikiwa kwa asilimia 90, lakini ni kama wamemtoa ‘kafara’ tu, hivyo tusubiri kuona maajabu kwa Ndayirajige,” alisema Mwaisabula na kuendelea.

“Bila malengo ya muda mrefu hata Ndayiragije tutamlaumu tu, tumezoea kumuona kocha huyo akifundisha klabu, huko ni tofauti na kufundisha timu ya Taifa.

“Hata Mourinho anaweza kuwa kocha mzuri kwenye klabu na si timu ya Taifa, kwenye klabu mchezaji unakuwa naye muda wote, unaweza kubadili mazoezi utakavyo, lakini si katika timu ya taifa, hivyo ni kama Ndayiragije ameingia kitanzini,” alisema.

Kocha Abdallah Kibadeni alisema ni suala la kupewa muda tu kwa Ndayiragije, japo naye ameungana na watangulizi wake kusisitiza kuwa kuna tofauti kubwa kati ya kufundisha klabu na timu ya Taifa.

“Kikubwa ni Watanzania wamuamini, na kocha apewe muda wa kutosha kuandaa kikosi, kila mmoja anapenda mafanikio katika soka la Tanzania na tuna matumaini tutaanza vema kwenye Chan,” alisema.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao katika moja ya mahojiano na gazeti hili alisema kocha huyo ataiongoza Stars kwenye Chan wakati mchakato wa kupata mrithi wa Amunike ukiendelea.

“Chan iko karibu, hivyo ni ngumu kupata kocha, mchakato huo unahitaji muda na utulivu, hivyo kocha atakayeteuliwa ataiongoza timu kwenye Chan wakati mchakato wa kupata kocha mkuu ukiendelea,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz