Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndayiragije aipigia hesabu Libya Afcon

84961 Ndai+pic Ndayiragije aipigia hesabu Libya Afcon

Thu, 21 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ inateremka uwanjani kuikabili Libya, katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), utakaochezwa leo nchini Tunisia.

Baada ya kuifunga Guinea ya Ikweta mabao 2-1 na kushika nafasi ya pili katika Kundi J nyuma ya Tunisia, mchezo wa leo dhidi ya Libya utakuwa mgumu.

Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwa kuwa Libya itaingia uwanjani ikiwa imefungwa na Tunisia.

“Libya timu nzuri naamini itaingia kwa nguvu ili kurekebisha kilichotokea katika mechi ya kwanza.

“Naamini wachezaji watafanyia kazi mpango ambao tumeuandaa dhidi ya wapinzani wetu, tuna nafasi kubwa ya kupata matokeo mazuri ugenini,” alisema Ndayiragije.

Taifa Stars inapaswa kucheza kwa nidhamu hasa safu ya ulinzi licha ya Libya kupoteza kwa mabao 4-1 dhidi ya Tunisia katika mchezo wa kwanza.

Libya inaundwa na kundi la wachezaji wa daraja la juu wanaocheza soka la kasi wakitumia zaidi mbinu ya kupiga pasi fupi kwenda langoni mwa wapinzani.

Utulivu kwa Taifa Stars unahitajika hasa kipindi cha kwanza na dakika za lala salama za kipindi cha pili, muda ambao ni hatari kwa Libya kutafuta mabao.

Miongoni mwa washambuliaji wa Libya wamo Moataz Al Mehdi wa Al Nasri ya nchini humo na Mohamed Anis Saitou wa Etoile du Sahel ya Tunisia ambao ni nyota wanaopaswa kuchungwa.

Pia Libya ina nyota wanaocheza soka la kulipwa nje Muaid Ellafi (USM Alger), Ismael Tajouri-Shradi (New York City FC), Mohammed Sawlah (Al Muharraq FC), Hamdou Elhouni (Esperance), Al Musrati (Vitoria Guimares) na Ahmad Benali (Crotone).

Rekodi

Taifa Stars imezidiwa na Libya kwa nafasi 30 katika viwango vya ubora wa soka duniani na nafasi 15 Afrika. Taifa Stars ipo nafasi ya 133 kwa ubora duniani na 37 Afrika. Libya ipo nafasi ya 103 na 22 Afrika.

Katika mechi tano Taifa Stars imeshinda mechi tatu, imetoka sare moja imepoteza mara moja. Libya haikupata ushindi katika mechi tano za mwisho.

Chanzo: mwananchi.co.tz