Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndanda yaitishia nyau Simba

17444 Ndanda+pic TanzaniaWeb

Sun, 16 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Mtwara. Simba ilitua Mtwara kwa mbwembwe kubwa lakini imekutana na mkwara wa wenyeji Ndanda ambao wanakutana nayo leo kwa kuwaambia safari hii hawachomoki.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara watashuka dimbani kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara kuikabili Ndanda wakiwa na rekodi bora ya kushinda michezo yote waliyocheza kwenye uwanja huo dhidi ya timu hiyo.

Timu hiyo imekutana na Ndanda katika michezo minne kwenye uwanja huo na yote imepata ushindi. Michezo mitatu ikishinda kuanzia mabao mawili na mmoja ikishinda bao moja

Mikwara ya Ndanda

Kocha wa Ndanda, Malale Hamsini alisema wako tayari kufuta uteja na kuhakikisha wanaifunga Simba na wala timu hiyo haiwapi presha.

Malale aliliambia gazeti hili kuwa hawaangalii historia bali wanataka kuanza upya kwa kuhakikisha wanafuta uteja dhidi ya Simba na kusisitiza kuwa leo hawatatoka salama.

“Hivi sasa hatutaki kuangalia historia ya nyuma bali tunajipanga ili kumaliza hali ya kutopata ushindi dhidi ya Simba.Tutapambana kuhakikisha tunashinda mchezo huo”alisema Malale.

“Simba ni wazuri lakini ukiingalia machoni kwani bado hawachezi kitimu ila ni wazuri sana kwa uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.

Muhimu ni kuhakikisha sisi tunacheza kwa ushirikiano kila eneo ili kuwabana wapinzani wetu wasilete madhara”alisema Malale.

Simba

Kikosi cha Simba kilifanya mazoezi mapesi ya mwisho jana katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona hapa Mtwara.

Kocha wa Simba Patrick Aussems amewaka mipango yake hadharani kuwa pointi tatu ndio wamezifata katika mechi hii na si jambo lingine.

Alisema kikosi chake kipo kamili na uwepo wa mastraika wake watatu Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi tena ni jambo zuri.

“Katika mechi zote ambazo tumecheza Kagere, Bocco na Okwi hawajacheza wote katika mechi moja lakini katika mechi hii wana nafasi kubwa ya kucheza pamoja “

“Kagere ameshafunga mabao matatu katika mechi mbili za ligi kwahiyo atacheza kwa kujiamini na na imani kubwa atakuwa na kiu ya kuendelea kufunga”alisema Aussems

Aliongeza “ Katika mechi mbili zote Bocco amecheza lakini hajafunga na Okwi hajacheza hata mechi moja kwa kuwa alikuwa majeruhi kwa maana hiyo nawapa nafasi kubwa ya kufunga katika mechi hii.

“Maandalizi ya kutosha ambayo tumeyafanya kabla ya mechi hii ndio yananipa imani na matumaini makubwa ya kumaliza mechi kuondoka na pointi zote muhimu kwetu, “ alisema Aussems.

Azam yakabwa Shinyanga

Azam FC imelazimishwa sare ya 1-1 na Mwadui FC katika mchezo wa jana Ijumaa uliopigwa Uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga.

Azam ilikuwa ya kwanza kupachika bao katika dakika ya 55, kupitia kwa Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ aliyeunganisha pasi ya Ramadhani Singano ‘Mess’ na dakika ya 71, Edwin Innocent alisawazishia Mwadui. Mchezo mwingine jana jioni Coastal Union ilikuwa ikicheza na Lyon.

Ligi hiyo inaendelea leo kwa michezo kati ya Lipuli na Mtibwa wakati Prisons inacheza na Ruvu Shooting. Mbao itaialika JKT Tanzania na KMC dhidi ya Singida United.

Chanzo: mwananchi.co.tz