Kocha wa Al Sadd Xavi Hernandez ametoa kauli ya kutamani kurejea kwenye klabu yake ya zamani ya Barcelona kurithi nafasi ya Mdachi Ronald Koeman aliyetimulia kazi wiki chache zilizopita.
Xavi mwenye umri wa miaka 41, amesema “natamani kurudi nyumbani,kurudi tena Barcelona ni kitu cha kujivunia na cha furaha mno “, huku akisisitiza “Nimekuwa na mazungumzo na Barcelona kwa siku kadhaa na kila kitu kipo sawa ,vilabu vyote vinajua msimamo wangu na matumaini yangu watafikia mwafaka kwa haraka sana” amesema Xavi.
Kiungo huyo wa zamani wa Barcelona alidumu kwa miaka 17 kati ya mwaka 1998 mpaka 2015 huku akicheza michezo 779 na kushinda mataji makubwa 25 kisha kutimkia AL Sadd kama mchezaji kisha kupewa nafasi ya kocha mkuu wa klabu hiyo ya Qatar.
Maofisa wa Barcelona Rafa Yuste na Mateu Alemany waliwasili mjini Doha siku ya jumanne kufanya mazungumzo na uongozi wa Al Sadd ingawaje mtendaji mkuu wa klabu hiyo Turki Al-Ali amesisitiza kutokuwa tayari kumuachia Xavi na kusema “msimamo wa klabu upo wazi toka mwanzo ,tunajitahidi kumbakisha Xavi kusalia na sisi “.
Barcelona ipo nafasi ya tisa kwenye msimamo wa La Liga baada ya kucheza michezo 11 na kushinda michezo 4 wakiwa nyuma ya vinara Real Sociedad wenye alama 9 huku wakiwa chini ya kocha wa muda Sergi Barjuan.