Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nani wa kuizuia Yanga?

34071 YANGA+PIC Tanzania Web Photo

Mon, 31 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Yanga imeonyesha kweli haitanii msimu huu baada ya jana kuendeleza ubabe wa ushindi wa Ligi Kuu Bara baada ya kuilaza Mbeya City mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Matokeo hayo yameifanya Yanga kuendelea kujikita kileleni ikifikisha pointi 50 huku ikijivunia hazina yake ya mabao 35.

Yanga imebakia timu pekee ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja kwani Azam FC jana ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.

Yanga ilipata mabao yake mawili yaliyowekwa kimiani na Heritier Makambo.

Alianza kufunga bao dakika ya 17’ akimalizia mpira wa faulo wa Ibrahim Ajibu. Mpira huo unamfanya Ajibu kufikisha asisti 13 zilizotengeneza mabao kwenye mechi hizo za Ligi Kuu.

Hata hivyo, Mbeya City wakiongozwa na Eliud Ambokile walitumia dakika saba tu kukomboa bao hilo kwani Idd Seleman ‘Nado’ alifunga bao hilo dakika ya 24 .

Makambo ambaye hakuwahi kufunga mabao mawili katika mechi moja, aliiandikia Yanga bao la pili dakika ya 41 kwa kichwa akimalizia krosi ndefu ya beki Paul Godfrey. Makambo alifunga bao hilo akiwa mbele ya mabeki watatu wa City na kipa wao Bakar Fikirini. Licha ya ushindi huo, lakini Yanga haikupata urahisi mbele ya City kwa namna mchezo ulivyokuwa, kwani mabeki wa Yanga walipata kazi ya kuzuia mashambulizi ya Nado, Mohammed Samatta, Victor Hangaya na Ambokile ambaye hata hivyo aliumia na kuwahishwa hospitali. Nafasi yake ilijazwa na Peter Mapunda.

Matokeo hayo ya jana yameifanya Yanga kuiacha Azam kwa pointi 10 na alama 20 zaidi ya Simba (kabla ya mchezo wao wa usiku dhidi ya Singida Utd) na kutengeneza mazingira ya kutwaa taji msimu huu.

Mechi nyingine za jana, Ruvu Shooting iliilaza Biashara bao 1-0 wakati Lipuli ilitoka suluhu na Ndanda FC mjini Iringa matokeo sawa na African Lyon dhidi ya Mwadui.



Chanzo: mwananchi.co.tz