Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namungo yaipania Simba Ngao ya Jamii

57e5fc6684461f02e489133dfac17104 Namungo yaipania Simba Ngao ya Jamii

Fri, 28 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TIMU ya Namungo imesema itahakikisha inatoa kipigo kitakatifu katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini hapa Jumapili ijayo.

Akizungumza na gazeti hili jana kuelekea mchezo huo, Katibu Mkuu wa Namungo, Ally Selemani, alisema maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yanakwenda vema na wanatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam leo Ijumaa wakiwa na wachezaji 28, benchi la ufundi likiwa na watu saba na viongozi watano na kwamba wataingia leo usiku jijini Arusha.

“Simba ni timu nzuri, lakini tutaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa ili kuibuka na ushindi na kutwaa Ngao ya Jamii,” alisema.

Timu hizo kwa mara ya mwisho zilikutana hivi karibuni katika fainali ya Kombe la Shiriksho la Azam, ambapo Simba ilishinda 2-1 na kutwaa taji hilo.

Wakati huohuo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza viingilio vitakavyotumika katika mchezo huo, ambapo cha juu ni Sh 30,000 na cha chini 10,000.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko wa TFF, Bonifance Wambura, alisema kutakuwa na aina tatu ya viingilio na hiyo ni kutokana na mzingira ya uwanja huo, ambapo jukwaa kuu ni Sh 30,000, jukwaa A na B Sh 15,000 na mzunguko ni 10,000.

“Utaratibu tiketi zitauzwa siku ya mchezo kwenye vituo mbalimbali hapa jijini Arusha, ambapo tutavitangaza baada ya kukutana na viongozi wa Chama cha Soka Arusha (ARFA) na zitatolewa mapema katika vituo vingi ili kuepusha msongamano.”

“Katika mchezo huo lazima mshindi apatikane, hivyo utaanza saa 9:30 alasiri ili uishe mapema endapo timu hizo zitaenda muda wa ziada, pia tunazingatia mashabiki wanaotoka nje ya Arusha ambao wanataka kuondoka siku hiyohiyo,” alisema Wambura.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Wambura alisema yapo katika hatua za mwisho kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa na waamuzi sita watachezesha mpambano huo.

Naye, Abbas Ally, mratibu wa timu ya Simba, alisema wako tayari kwa mchezo huo na kikosi chao kinatarajiwa kuingia Arusha leo jioni.

“Kimsingi tuko tayari na lengo letu ni kutetea Ngao ya Jamii ambayo tuliitwaa mwaka jana na tunataka kuendelea kuibeba.”

“Tunafahamu mchezo hautakuwa mwepesi kwani Namungo ni timu nzuri na tuna amini wamefanya usajili mzuri na tuna waheshimu, lakini na sisi tunataka kuanza vizuri,” alisema.

Alisema baada ya mchezo huo wataendela kubaki Arusha kwa siku tano na watacheza mchezo mmoja wa kirafiki.

Alisema wataweka wazi ni timu gani watakayocheza nayo na baada ya hapo wataondoka kwenda Mbeya kwa ajili ya msimu mpya wa ligi, ambao unatarajiwa kuanza Septemba 6 na Simba itacheza dhidi ya Ihefu.

Chanzo: habarileo.co.tz