LIGI Kuu ya Tanzania Bara imeendelea tena jana kwa michezo miwili kupigwa katika mikoa miwili tofauti, Lindi katika Uwanja wa Majaliwa, Namungo waliwakaribisha Mtibwa Sugar , mkoani Mbeya, Ihefu walikuwa wenyeji wa Polisi Tanzania katika Uwanja wa Highland Estate.
Katika mchezo wa mapema Namungo wameutumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, bao lililofungwa na Ibrahim Abdallah katika dakika ya 20.
Mtibwa walilazimika kumaliza dakika 90 wakiwa pungufu baada ya beki Abubakar Ame, kuoneshwa kadi nyekundu dakika ya 75 kwa mchezo usiokuwa wa kiungwana.
Namungo, imefikisha pointi 35 na kupanda hadi nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Mkoani Mbeya baada ya kupata ushindi mara tatu mfululizo katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara wakiwa katika uwanja wa nyumbani, Ihefu imeshikwa shati baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Polisi Tanzania kutoka mjini Moshi.
Wenyeji walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 32 kupitia kwa kiungo Rafael Daud, Polisi walisawazisha bao hilo kupitia kwa Kassim Shaban, dakika ya 35, sare hiyo imeipeleka Ihefu hadi nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa imejikusanyia pointi 31 baada ya michezo 29.
Wakati huo huo Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mchezo mmoja, Mbeya City watakuwa nyumbani katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, watawakaribisha Ruvu Shooting kutoka Pwani.