Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nahodha Yondani, Kakolanya waibua mapya

28062 Pic+yondani TanzaniaWeb

Wed, 21 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/ Mwanza. Wakati Yanga ikitarajiwa kucheza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara nje ya Mkoa wa Dar es Salaam hapo kesho, nahodha Kelvin Yondani na kipa chaguo la kwanza Beno Kakolanya wamegoma kuongozana na kikosi hicho.

Yanga kesho inatarajiwa kucheza na Mwadui FC, katika mchezo wa raundi ya 11 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Yanga iliwasili Mwanza saa 1:30 asubuhi kwa Ndege ya Air Tanzania na kupata mapokezi kabambe kutoka kwa mashabiki waliokuwa kwenye magari na pikipiki.

Yondani na Kakolanya waliwasili juzi wakitokea Lesotho walipokuwa na Taifa Stars ambapo walipewa ruhusa ya kwenda kuonana na familia zao kabla kukutana na wenzao wa Yanga kwa safari ya Kanda ya Ziwa.

Hata hivyo, ilipofika saa sita usiku wachezaji hao hawakuwepo katika msafara wa Yanga uliokuwa tayari kwa safari ya kwenda Mwanza na baadaye Shinyanga.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Chanzo cha karibu na wachezaji hao kilidokeza Yondani na Kakolanya wamegoma kwenda Shinyanga ili kushinikiza kwa uongozi kulipwa fedha zao.

Chanzo hicho kilichoomba hifadhi ya jina lake, alisema wachezaji hao wanadai sehemu ya fedha za usajili wa msimu huu, hivyo wameweka ngumu kucheza mechi za Ligi Kuu hadi walipwe.

Hii siyo mara ya kwanza wachezaji hao kugoma kushinikiza uongozi wa klabu hiyo kuwalipa sehemu ya fedha za usajili, posho na malimbikizo ya mishahara.

Juhudi za gazeti hili kuwatafuta Yondani na Kakolanya ziligonga mwamba kwa kuwa hadi tunakwenda mtamboni, simu zao za mkono zilikuwa zimezimwa kutwa nzima.

Akizungumza jana, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kwa ufupi hana taarifa ya kukosekana kwa wachezaji hao katika msafara uliokwenda Shinyanga.

“Sina taarifa za Yondani na Kakolanya kutokwenda Shinyanga, waulize wenyewe ndio wanajua,” alisema Saleh kwa kifupi kabla ya kukata simu.

Wachezaji wengine waliokuwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ambao wamekwenda Shinyanga ni Andrew Vincent ‘Dante’ Feisal Salum na Gadiel Michael.

Meneja wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema mchezo utakuwa mgumu, lakini wamefanya maandalizi ya kutosha ili kupata ushindi.

“Tunaiheshimu Mwadui kutokana na upinzani wao lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda, ni mchezo muhimu kwetu kwasababu ndiyo wa kwanza kucheza nje ya Dar es Salaam,” alisema.

Mwenyekiti wa Yanga Mkoa wa Mwanza, Saleh Akida alisema matawi yote ya klabu hiyo mkoani humo yamejipanga kuiunga mkono katika mechi zote za Kanda ya Ziwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz